Jumuiya ya Udugu wa Kiekumene katika Siasa Chemin Neuf ni jukwaa la majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa ajili ya ushuhuda wa upendo kwa maskini. Jumuiya ya Udugu wa Kiekumene katika Siasa Chemin Neuf ni jukwaa la majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa ajili ya ushuhuda wa upendo kwa maskini. 

Jumuiya ya Udugu wa Kiekumene Chombo Cha Injili ya Upendo

Katika ulimwengu mamboleo ambamo kuna mashindano makubwa ya kutafuta heshima na madaraka; uchu wa mali na fedha kuna hatari kubwa kwamba, maskini na wanyonge wakabezwa na kudhaniwa kwamba, wao “si mali kitu”. Lakini, huduma kwa maskini inayofumbatwa katika nguvu na tunu msingi za Kiinjili, inawawezesha maskini kupata haki ya maisha na matumaini thabiti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jumuiya ya Udugu wa Kiekumene ya Chemin Neuf, Kwa kifupi: CCN (Communauté “Chemin Neuf”) kilianzishwa kunako mwaka 1972 mjini Lione, Ufaransa na Padre Laurent Fabre, SJ. Kunako mwaka 1984 Jumuiya ikatambuliwa kwa ngazi ya Kijimbo. Na kuanzia mwaka 1992 ikaanza kujielekeza katika malezi na majiundo ya Kipadre. Ni Jumuiya ambayo ina mwelekeo wa kiekumene, kwa kuwaunganisha wamini kutoka Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili “Wote wawe na umoja” Rej. Yn.17. Lengo ni kuendeleza majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uhalisia wa maisha, umoja na udugu wa kibinadamu, huku wakisaidiana na kukamilishana katika maisha yao. Jumuiya ya Udugu wa Kiekume ya Chemin Neuf, imeenea katika nchi 20. Barani Afrika Jumuiya hii iko katika nchi 6, Mashariki ya Kati iko katika nchi 2, Amerika ya Kaskazini kuna Jumuiya 2 na huko Amerika ya Kusini kuna Jumuiya 1. Wote hawa wanaunda Jumuiya ya Kitume ya Chemin Neuf, kwa kuwa na wanachama zaidi ya 6, 000 na Makao makuu yake yakon chini Ufaransa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 30 Aprili 2021 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Uudugu wa Kiekumene ya Chemin Neuf, mjini Vatican. Katika hotuba yake, amekazia wito wa waamini walei katika kukuza na kudumisha Injili ya upendo katika: familia, jamii na siasa, kwa kujikita katika imani; kwa kuendelea kujenga udugu wa kibinadamu kwa ajili ya huduma kwa maskini inayofumbatwa katika wongofu wa kiekolojia. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa inayotekelezwa na Roho Mtakatifu na kushuhudiwa na Chama hiki cha Kitume katika hija ya maisha ya kiutu, kiroho na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Haya ni mapambano dhidi ya umaskini, ili kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na udugu wa kibinadamu.

Katika ulimwengu mamboleo ambamo kuna mashindano makubwa ya kutafuta heshima na madaraka; uchu wa mali na fedha kuna hatari kubwa kwamba, maskini na wanyonge wakabezwa na kudhaniwa kwamba, wao “si mali kitu”. Lakini, huduma kwa maskini inayofumbatwa katika nguvu na tunu msingi za Kiinjili, inawawezesha maskini kupata haki ya maisha na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi na wengi wanaofaidika ni vijana wa kizazi kipya. Wito wa waamini walei unakita mizizi yake katika Injili ya Upendo unaopaswa kumwilishwa katika familia, jamii na hata katika medani za kisiasa. Huu ni wajibu na dhamana inayopata chimbuko lake katika imani, ili kujenga ulimwengu mpya kwa kuzama zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Lengo ni kusaidia mchakato wa ujenzi haki, amani na usalama; kwa kujikita katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu na huruma, ili kujenga na kuendeleza Ufalme wa Mungu hapa duniani. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa mujibu wa majadiliano ya kiekumene kiini cha maisha na utume wao, unaowawezesha kuwapokea na kuwakaribisha watu kutoka katika tamaduni na Mapokeo ya Kikristo, ili hatimaye, kuleta mageuzi ya sura ya jamii ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, madaraja yanayowakutanisha watu, ili kubomoa kuta za utengano na ubaguzi dhidi ya watu wengine. Kwa njia ya maisha na utume wa Jumuiya ya Udugu wa kiekumene ya Chemin Neuf, wanaendelea kuwa ni mashuhuda wa Kanisa maskini kwa ajili pamoja na maskini, Kanisa linalotoka kifua mbele ili kujenga udugu wa kibinadamu na ujirani mwema kwa maskini na wale wote wanaoteseka kwa sababu mbalimbali katika maisha. Hawa ni wale wasiokuwa na fursa za ajira, wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Imani kwa Kristo Yesu aliyekuwa fukara, inawasukuma kuwa karibu zaidi na maskini, ili kuwashirikisha katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, kuna umuhimu kwa watu wa Mungu kujikita katika wongofu wa kiekolojia, ili kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea kuwafundisha watu wa Mungu kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja. Ni changamoto ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji, nyuma yake kuna historia na maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawataka wanajumuiya hawa kuendelea kuimarika katika imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kumtangaza na kumshuhudia kwamba, bado anaendelea kuishi na ni changamoto ya matumaini mapya kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo pamoja na wale wote wenye huzuni, hasa miongoni mwa jamii. Wajumbe wa chama hiki wajitahidi kujenga mahusiano na mafungamano ya urafiki na udugu wa kibinadamu ili kujenga ulimwengu ulio bora zaidi. Kristo Yesu anategemea na kuthamini sana ujasiri, ari na mwako mwao katika maisha na utume.

Udugu wa Kiekumene
30 April 2021, 16:36