Tafuta

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, "WUCWO, UMOFC" limemtumia Papa Francisko ujumbe wa matashi mema katika maadhimisho ya kumbukizi la miaka 8 tangu kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, "WUCWO, UMOFC" limemtumia Papa Francisko ujumbe wa matashi mema katika maadhimisho ya kumbukizi la miaka 8 tangu kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. 

Ujumbe wa Wanawake Wakatoliki, "WUCWO" Kwa Papa Francisko!

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani lina mpongeza Papa Francisko kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Wanawake wanamwomba atambue na kuthamini mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; Ndoto ya wanawake wakatoliki kwa leo la kesho ya Kanisa la Kristo Yesu! Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maria Lia Zervino, Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC amemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha kumbukizi la miaka 8 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki hapo tarehe 13 Machi 2013 na kuanza utume wake rasmi tarehe 19 Machi 2013 wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria. Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani lina mpongeza Papa Francisko kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa, Ndoto ya wanawake wakatoliki kwa leo la kesho ya Kanisa la Kristo Yesu! Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapoendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kufanya kumbukizi la miaka nane tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tangu alipochaguliwa, kwa msaada wa Roho Mtakatifu, alipenda kunafsisha ndani mwake ari na moyo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Papa ameendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa sasa Kanisa linaendelea kujizatiti katika mchakato wa kutangaza Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” kwa kujikita zaidi katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa ajili ya watu wa Mungu katika Karne ya 21. Yote hayo yaliyotolewa kwa muhtasari yanapatikana kwenye Nyaraka zifuatazo: Mosi ni Wosia wa Kitume: “Evangelii gaudium” yaani Furaha ya Injili! Huu dira na mwongozo wa shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa. Ni ushuhuda wa furaha na upendo unaobubujika baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha na hivyo, hii inakuwa ni fursa ya kufanya mabadiliko makubwa katika maisha. Jambo la msingi hapa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama chachu ya uinjilishaji mpya ilivyoshuhudiwa na watu kama Maria Magdalena, baada ya kukutana mubashara na Kristo Mfufuka, siku ile ya kwanza ya juma.

Pili, utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Tatu ni Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unaopania pamoja na mambo mengine: Kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene!

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, linampongeza Baba Mtakatifu kwa kubainisha “magonjwa ya Kanisa” na kuanza kuyatafutia dawa. Ni kiongozi ambaye amejipambanua katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto ya kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha na kamwe watu wa Mungu wasikubali kumezwa na malimwengu. Katika janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kushikamana pamoja katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, wongofu wa ndani na mabadiliko yanayofumbatwa katika elimu shirikishi. Papa Francisko ni kiongozi ambaye anaendelea kulipyaisha Kanisa kwa nyuso za wanawake wanaoonesha na kushuhudia upendo wa dhati; ukaribu, ujirani mwema pamoja na msamaha!

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, linakazia umuhimu na mchango wa wanawake wakatoliki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa sababu hawa ni sehemu kubwa inayounda watu wa Familia ya Mungu. Kuna wanawake wenye sifa ambao wameshuhudia umahiri, weledi, uadilifu, nidhamu na uwajibikaji katika medani mbalimbali za maisha ya kijamii, hususan katika uchumi, afya, elimu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kutafuta, kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, bila kusahau malezi katika familia na katekesi makini kwa watoto. Wanawake wanaomba nafasi ya kulihudumia Kanisa, ili kuchangia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao kama wanawake katika masuala ya uongozi na malezi makini ndani ya Kanisa, ili kujenga na kuboresha mahusiano na mafungamano bora zaidi katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe zaidi katika vikao vinavyotoa maamuzi mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa.

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, linayo ndoto ya kutaka kuona kwamba: Wanawake wanateuliwa pia katika Mahakama zinazohusiana na masuala ya ndoa na talaka. Wanawake wanataka kushirikishwa katika malezi na makuzi ya majandokasisi; wawe ni walezi watakaowaongoza pia waseminari katika safari ya maisha yao ya kiroho! Wanawake waendelee kushirikishwa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Wafundwe vyema, ili waweze pia kujipambanua katika kusimamia haki msingi za binadamu! Hapa ni wanawake wote, yaani watawa na waamini walei. Ushiriki wa wanawake katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, uangaliwe upya, ili kuleta uwiano mzuri zaidi utakaosaidia kupokea maoni ya wanawake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo katika ujumla wake. Ni wakati muafaka wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Wanawake Wakatoliki
15 March 2021, 15:43