Papa Francisko: Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika kunafsisha tunu msingi za maisha familia, umuhimu wa kazi pamoja na utu wema! Papa Francisko: Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika kunafsisha tunu msingi za maisha familia, umuhimu wa kazi pamoja na utu wema! 

Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume Wake Bikira Maria 19 Machi!

Papa: Yosefu ni kati ya watakatifu wakuu wanaoheshimiwa sana na Kanisa na ni mfano bora wa kuigwa. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na hekima na busara kama alivyokuwa Mtakatifu Yosefu, tayari kunafsisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora katika kuenzi tunu msingi za maisha ya kifamilia; umuhimu wa kazi na utu wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Yosefu anaitwa mtumishi mwaminifu wa Mungu, kwani uaminifu wake huo, ndio ambao unamshirikisha kwa namna iliyositirika katika historia nzima ya wokovu. Matendo yake ya kiimani hayaonekani kwa wazi sana katika Maandiko Matakatifu lakini yanapaswa kupewa uzito wa pekee, mathalani kwa kuwa mtii katika hali ya ukimya wakati wa kuitikia sauti ya Mungu. “Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye hekima”. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Machi 2021 amesema, Yosefu ni kati ya watakatifu wakuu wanaoheshimiwa sana na Mama Kanisa, mfano bora wa kuigwa. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na hekima na busara kama alivyokuwa Mtakatifu Yosefu, tayari kunafsisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao.

Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora katika kuenzi na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; maeneo ya kazi; wakati wa raha na shida, waamini kamwe wasisite kumwita katika sala. Kanisa linamwadhimisha Mtakatifu Yosefu katika maisha ya kila siku, katika juhudi, bidii na maarifa kazini zilizomwezesha kuihudumia Familia Takatifu ya Nazareti. Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Mwaka huu unatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu.

Papa anasema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Mei 2021 aliendelea kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, shuhuda wa maisha ya kila siku, anayeonesha uwepo wake mwanana. Yosefu Mtakatifu ni mtu asiyependa makuu, aliyetekeleza dhamana na wajibu wake katika Familia Takatifu kwa umakini mkubwa. Awe ni mfano bora wa kuigwa na mwombezi wa familia za Kikristo wakati wa raha na machungu, ili kamwe familia zisitindikiwe mafuta ya imani na furaha inayobubujika kwa kuungana na Mwenyezi Mungu.

Mtakatifu Yosefu
18 March 2021, 07:25