Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa kituo cha Wafranciskani kwa kukazia utendaji wa Mungu unaojidhihirisha katika: ukaribu, huruma, upendo na msamaha wa kweli. Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa kituo cha Wafranciskani kwa kukazia utendaji wa Mungu unaojidhihirisha katika: ukaribu, huruma, upendo na msamaha wa kweli. 

Papa: Utendaji wa Mungu: Ukaribu! Huruma, Upendo na Msamaha!

Papa Francisko asema: Mtindo wa utendaji wa Mwenyezi Mungu unajidhihirisha kwa namna ya pekee katika ukaribu unaounda ujirani mwema, huruma na upendo, mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na wafanyakazi katika Kituo cha Mshikamano wa Wafranciskani. Haya ni mambo msingi katika kutangaza, kushuhudia Injili sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kituo cha Mshikamano wa Wafranciskani kilianzishwa kunako mwaka 1983 kwa ushirikiano wa Familia tatu za Wafranciskani zinazotekeleza dhamana na utume wao Jimbo kuu la Firenze, Italia. Hawa ni Wafrancisko Wakapuchini, OFM Cap, Wafrancisko Wakonventuali, OFM Cov., na Wafrancisko, OFM. Tangu wakati huo, Kituo hiki kimeendelea kutoa huduma muhimu sana ya kusikiliza na ujirani mwema kwa watu wanaokabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kimekuwa ni msaada mkubwa wa huduma kwa wazee, walemavu na watu wasiojiweza; watu ambao kimsingi wanahitaji msaada pamoja na kusindikizwa katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mtindo wa utendaji wa Mwenyezi Mungu unajidhihirisha kwa namna ya pekee katika ukaribu unaounda ujirani mwema, huruma na upendo, mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na wafanyakazi katika Kituo cha Mshikamano wa Wafranciskani.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe Mosi, Machi 2021 wakati alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Kituo cha Mshikamano wa Wafranciskani. Ulimwengu mamboleo una mwendo kasi unaozalisha utajiri wa haraka haraka na kwa upande mwingine kuna ulimwengu unaozalisha maskini na ukosefu wa usawa! Kituo cha Mshikamano wa Wafranciskani kinatekeleza dhamana na wajibu wake kwa kujizamisha katika imani, huku wahudumu wake, wakipandikiza mbegu za Ufalme wa Mungu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake wa kutangaza Injili na kushuhudia ujenzi wa Ufalme wa Mungu, alionesha ukaribu na huruma kwa madonda ya binadamu. Kristo Yesu, akaonesha huruma na upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; watu waliokuwa hawaaminiki tena; waliotengwa na kunyanyaswa! Haya ndiyo matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama yanavyofafanuliwa katika Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo 25: 35.36.

Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma na moyo wa Mungu Baba anayetaka: kuhifadhi, kulinda na kuendeleza utu na heshima ya watoto wake wote kwa kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga mazingira bora zaidi ya kiutu, kijamii na kiuchumi, ili kamwe asiwepo mtu anayeteseka kwa kukosa mahitaji yake msingi au kwa kutumbukia katika upweke hasi! Baba Mtakatifu anasema, huu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika maisha na utume wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejitahidi kuhakikisha kwamba, anamwilisha udugu wa kibinadamu kwa watu wote! Akapandikiza mbegu ya amani na kutembea bega kwa bega na maskini, waliotelekezwa, wagonjwa na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa kufuata mfano wa maisha yake kwa takribani miaka 40 sasa, hii ni alama ya Injili ya matumaini inayokinzana na hali halisi ya mji wa Firenze. Huu ni mji ambao “una wagalagaza” na watu wengi kujikuta katika umaskini na upweke wao.

Hii ni hali inayopaswa kuamsha dhamiri nyofu, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na kuanza kujikita katika huruma kwa wale waliojeruhiwa; kwa kuinama kwa huruma na upendo, ili kuwahudumia wale wote wanaokandamizwa na mzigo mzito wa maisha. Huu ni utume unaopaswa kusongeshwa mbele kwa ujasiri. Baba Mtakatifu anasema, anawaombea ili kweli Mwenyezi Mungu aendelee kuwategemeza kwa sababu kwa moyo wa upendo na nguvu za kibinadamu “haziwezi kufua dafu”. Jambo la kwanza kwa maskini, ni kumwonesha ushuhuda wa upendo, ili aweze kujisikia kuwa pembeni mwake anao ndugu wanaomjali! Jambo hili linawezekana ikiwa kama mwamini anategemezwa na neema ya Kristo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia sala zake kwa Kristo Yesu ili kwamba, kwa njia ya maombezi ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aweze kuwazamisha katika furaha ya kuhudumia, furaha ya ujirani mwema na furaha ya upendo kwa maskini!

Papa Mshikamano
01 March 2021, 15:42