Tafuta

2021.03.28 SMisa ya Matawi na Malaika wa Bwana 2021.03.28 SMisa ya Matawi na Malaika wa Bwana  

Papa Francisko:Tawi la ushindi linapitia katika Mti wa Msalaba

Ikiwa imani inapoteza mshangao,inakuwa kiziwi.Haiwezi kusikia zaidi mshangao wa neema,haiwezi kusikia zaidi radha ya Mkate wa maisha na ya Neno, haiwezi kutambua uzuri zaidi wa ndugu na zawadi ya uumbaji.Ni katika mahubiri ya Papa Francisko wakati wa maadhimisho ya Dominika ya Matawi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Papa Francisko amehimiza kuomba neema ya kuwa na mshangao.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Jumapili tarehe 28 Machi 2021, ambapo Mama Kanisa ameingia katika kipindi kingine kikuu cha historia ya wokovu wa Kanisa kupitia Mateso ya Mkombozi wake kwa kufunguliwa na Siku Kuu ya Matawi. Katika fursa hiyo Papa Francisko ameadhimisha Misa Takatifu Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican. Akianza mahubiri Yake Papa amesema: Kwa adhimisho la Dominika hii ya Matawi tunaingia katika Juma Kuu ambamo ndani yake tunaadhimisha mafumbo makuu ya ukombozi wetu. Mfungo wetu wa Kwaresima, bidii ya kuishi katika maisha ya fadhila na matendo mema kwa njia ya sala, toba na wongofu vilikuwa pia na lengo la kutuandaa kushiriki kikamilifu maadhimisho haya makuu yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Kila mwaka katika Liturujia inaleta ndani mwetu tabia ya mshangao. Tunatoka katika furaha ya kumpokea Yesu ambaye anaingia Yerusalemu kuingia katika uchungu wa kumwona anahukumiwa kifo na kusulibishwa. Ni tabia ya kiundani ambayo itatusindikiza Juma zima kuu  Takatifu. Tunaingia kwa maana hiyo katika mshangao”.  

Kwa haraka Yesu anatushangaza. Watu wake walimpokea katika sikukuu kubwa lakini Yeye akaingia ndani ya Yerusalemu akiwa juu ya mwana punda mnyenyekevu. Watu wake walisubiri Pasaka ya kukombolewa na nguvu, lakini Yesu akatimiza Pasaka kwa kijitoa sadaka yake. Watu wake walikuwa wanasubiri kusheherekea ushindi dhidi ya Warumi na panga, lakini Yesu akaja kusheherekea ushindi wa Mungu na Msalaba. Je ni kitu gani kilitokea kwa watu wake ambao siku chache kabla walikuwa wanaimba Hosana Yesu hadi kufikia kupiga kelele kuwa asulibiwe?  Wale watu walikuwa wanafuata picha ya Masiha ambaye hakuwa Masiha, Papa amesisitiza. Walikuwa wanastaajabu, lakini  ustaajabu  huo unaweza kuwa wa kidunia kwa sababu unatafuta ladha zake na matarajio yake; mshangao kinyume chake unabaki umefunguliwa kwa mwingine na kwa mambo yake mapya. Hata leo hii wengi wanamstaajabia Yesu, wanazungumza vema juu yake, kwamba alipenda na kusamehe na mfano wake ulibadili historia… Wanataajabu lakini maisha yao hayabadiliki. Hii ni kwa sababu kustaajabia Yesu tu hakutoshi. Inahitaji kumfuata katika njia yake na kuacha uangazwe naye ili utoke katika tabia ya kutaajabia na kufikia mshangao wa kweli Papa amehimiza.

Ni kitu gani kikuu kinashangaza kwa Bwana na Pasaka yake? Ni kwamba Yeye alifikia utukufu kwa njia ya unyenyekevu. Yeye anashinda akikaribisha uchungu na kifo ambacho kwetu sisi tuliojazwa na mishangao ya mafanikio tungeweza kuzuia. Lakini Yesu kama alivyosema Mtakatifu Paulo “alijivua mwenyewe, akajinyenyekeza binafsi (Fil 2,7.8). Hii inatushangaza kuona Mwenyezi anakuwa hivyo. Kumwona Yeye ambaye ni Neno na kujua kila kitu, anatufundisha ukimya juu ya altare ya Msalaba. Kumwona Mfalme wa wafalme ambaye ametundikwa juu ya msalaba. Kumwona Yeye, wema wa mtu ambaye anakashfiwa na kukanyagwa. Je ni kwa nini unyenyekevu huo wote. Ni kwa nini Bwana umejiachia wafanye hayo yote watakayo? Papa Francisko kwa kujibu amesema kwamba alifanya hivyo kwa ajili yetu ili kutugusa hadi ukina wa uhalisi ya binadamu; ili tuweze kuondoka katika  maisha yetu yote na ubaya wetu wote. Kwa ajili ya kutukaribia na siyo kutuacha peke yetu katika uchungu na kifo; na Ili kuweza kurudi na kutukomboa. Yesu anapanda msalabani ili aweze kushuka katika mateso yetu. Anajaribu hata hisia zetu za ndani zilizo mbaya kama vile kutofanikiwa kwetu, kukataliwa na wote, kusalitiwa na yule wa kumtakia mema na hasa kuachwa na Mungu. Anafanya uzoefu wa mwili wake katika upinzaji wetu mbaya sana, na kwa maana hiyo anatukomboa na kutubadilisha. Upendo wake unakaribia udhaifu wetu, hadi kufikia mahali ambamo sisi tunakuwa na aibu zaidi. Na sasa tunajua kuwa sisi sio peke yetu. Mungu yupo pamoja nasi kwa kila jeraha, na kila hofu. Kwa manaa hiyo hakuna ubaya, hakuna dhambi yenye neno la mwisho. Mungu anashinda, lakini tawi la ushindi linapitia mti wa msalaba. Kwa maana hiyo matawi na msalaba viko pamoja.

Papa Francisko amehimiza kuomba neema ya kuwa na mshangao. Maisha ya kikristo bila mshangao ni mabaya sana. Inawezekanaje kushuhudia furaha ya kuwa umekutana na Yesu ikiwa huachi ushangazwe kila siku na upendo wa kushangaza ambao unatusamehe na unatufanya kuanza kwa upya? Ikiwa imani inapoteza mshangao,inakuwa kiziwi. Haiwezi kusikia zaidi mshangao wa neema,haiwezi kusikia zaidi radha ya Mkate wa maisha na ya Neno, haiwezi kutambua uzuri zaidi wa ndugu na zawadi ya uumbaji. Katika Juma Kuu takatifu, Papa Fracisko ameomba kuinua mtazamo juu ya msalaba ili kupokea neema ya Mshangao. Mtakatfu Francis wa Assisi kwa kutazama Msalaba, alikuwa akishangaa ni kwa nini ndugu wengine walikuwa hawalii. Je sisi tunaweza kweli kujiachia kuguswa na upendo wa Mungu? Kwa nini hatujuhi tena kushangaa mbele yake? Papa anauliza maswali. Kwa kujibu amesema, "Labda ni kwa sababu imani yetu imeharibiwa na ukawaida. Labda ni kwa sababu tunabaki tumejifungia ndani ya majuto na tunaacha kugandishwa na kutotosheka kwetu. Labda ni kwa sababu tumepoteza imani kwa yote na tunajiaminisha hadi kukosea.  Lakini nyuma ya hizi ‘labda’ kuna suala la kwamba hatujajifungulia zawadi ya Roho ambaye ni Yule anayetupatia neema ya mshangao", Papa amethibitisha.

Papa Francisko akiendelea amekazi akuwa tuanzie katika mshangao, tutazame msalaba na kusema kwamba “Bwana ni jinsi gani unanipenda! Ni kwa jinsi gani nilivyo wa thamani kwako! Tujiachie tushangazwe na Yesu ili kurudi kwa mara nyingine kuishi, kwa sababu ukuu wa maisha haupo kwa sababu ya kuwa navyo  na kujithibitisha, bali ni katika kujigundua kuwa tunapendwa. Huo ndiyo ukuu wa maisha wa kujigundua kuwa tunapendwa, Papa amesisitia na kwamba na ukuu wa maisha ndiyo kweli uzuri wa upendo. Na katika uzuri wa kupenda. Katika Msalaba tunamwona Mungu mnyenyekevu, Mwenyezi aliyeharibiwa na kubaguliwa. Na kwa neema ya mshangao tunajua kuwa kumpokea aliyebaguliwa, kumkaribia aliye nyenyekezwa katika maisha, tunapenda Yesu, kwa sababu yeye yuko hapo katika walio wa mwisho na waliokakataliwa. Leo hii mara baada ya kifo cha Yesu, Injili inaonesha sura iliyo nzuri zaidi ya mshangao. Ni katika tukio la Askari ambaye kwa kumwona anatoa roho yake kwa namna hiyo alisema “Hakika huyo alikuwa ni Mwana wa Mungu” ( Mk 15,39). Je ni kwa jinsi gani alikuwa amemwona Yesu anakufa? Alimwona anakufa akipenda. Alikuwa anateseka sana lakini aliendelea kupenda. Na tazama huo ndiyo mshangao mbele ya Mungu ambaye anatambua kujaza upendo hata akiwa anakufa.

Katika upendo huo wa bure, askari wa kirumi, mpagani, alimpata Mungu. Kweli alikuwa ni Mwana wa Mungu! Sentensi yake inagandisha Mateso. Wengi kabla yake katika Injili walikuwa wanastaajabia Yesu kwa miujiza yake na mambo makuu, walikuwa wamemtambua Mwana wa Mungu, lakini Yesu alikuwa amewambia wanyamaze, kwa sababu kulikuwa na hatairi ya kusimamia juu ya kustaajabu kidunia, katika wazo la Mungu wa kuabudu na kuogopa kwa jinsi ya nguvu na ya kutisha. Lakini sasa siyo tena hivyo chini ya msalaba, na siyo tena kumfikiria hivyo, kwa maana Mungu amejionesha na anatawala tu kwa nguvu isiyo na silaha, upendo usio na kizuizi cha hatari. Leo hii Mungu anatushangaza tena katika akili zetu na katika mioyo yetu. Tuacha mshangao huo utuzingire na tutazame Msalaba na kusema hata sisi “Wewe kweli ni mwana wa Mungu. Wewe ni Mungu wangu!

MAHUBIRI YA PAPA DOMINIKA YA MATAWI
28 March 2021, 14:07

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >