Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa wakiwa wametakaswa na kupyaishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa wakiwa wametakaswa na kupyaishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. 

Papa Francisko: Jiandaeni kwa Sala na Toba Kuadhimisha Pasaka!

Waamini wajiandae kuadhimisha Fumbo la Pasaka, huku nyoyo zao zikiwa zimetakasika na kupyaishwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Maadhimisho ya Juma kuu, iwe ni fursa ya kuwakumbuka, kuwaombea na kuwahudumia: wagonjwa, maskini na wote wanaoteseka. Fumbo la Pasaka ni ufunuo wa upendo wa Mungu unaosamehe kwa kujifunua katika huruma na maisha mapya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake kuhusu maadhimisho ya Juma kuu kwa Mwaka 2021, Jumatano tarehe 31 Machi 2021 amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Na kwa njia hii, wataweza kuonja wema na huruma ya Mungu, ikiwa kama watania mamoja na kuendelea kukaa ndani ya Kristo Yesu. Anawataka wagonjwa, wazee na wanandoa wapya wawe vyombo na mashuhuda wa huruma, wema na matumaini. Waamini wajiandae kuadhimisha Fumbo la Pasaka, huku nyoyo zao zikiwa zimetakasika na kupyaishwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini waendelee kuwa ni watu wa furaha na matumaini na kamwe wasiwaruhusu wajanja wachache kuwapoka matumaini yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wawe tayari kushiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Maadhimisho ya Juma kuu, iwe ni fursa ya kuwakumbuka, kuwaombea na kuwahudumia: wagonjwa, maskini na wote wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia. Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni ufunuo wa upendo wa Mungu unaosamehe kwa kujifunua katika huruma na maisha mapya.

Furaha ya mapambazuko ya Sherehe ya Pasaka iwe ni chemchemi ya: imani, matumaini na amani ya kukutana na Kristo Mfufuka! Hata katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Bikira Maria, Mama wa mateso, awe ni mfano bora wa kuigwa. Waamini wasithubutu kukimbilia Misalaba ya maisha yao, bali wawe na ujasiri wa kuunganisha mateso yao na yale ya Kristo Yesu anayewakirimia nguvu ya upendo wake unaofariji na kama kielelezo cha utukufu wake. Msalaba wa Kristo Yesu uwe ni mwanga unaowaangazia waamini kuelekea kwenye bandari salama. Pasaka ya Mwaka 2021 kwa wale wote wanaoteseka na kupepetwa katika maisha, iwe ni alama wazi ya matumaini, furaha ya kweli na amani ya ndani!

Maandalizi ya Pasaka

 

31 March 2021, 14:09