Papa Francisko: Fumbo la Maisha ya Sala na Ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu: Kristo Yesu lango la matumaini ya sala katika maisha ya binadamu! Papa Francisko: Fumbo la Maisha ya Sala na Ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu: Kristo Yesu lango la matumaini ya sala katika maisha ya binadamu! 

Papa Francisko: Maisha ya Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu

Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; Sala zinatofautiana sana; mapungufu na umaskini katika sala; Upendo na huruma ya Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni Mlango wa Sala ya waamini. Papa anasema, kwa njia ya Kristo Yesu sala ya waamini inafungua malango ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na hivyo kuwakirimia waja wake mafuriko ya neema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui jinsi ipasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”. Rum. 8: 14-15. 26-27. Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Machi 2021 akiwa kwenye Maktaba yake binafsi, ametafakari kuhusu: Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; Sala zinatofautiana sana; mapungufu na umaskini katika sala; Upendo na huruma ya Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni Mlango wa Sala ya waamini.

Baba Mtakatifu anasema kwa njia ya Kristo Yesu sala ya waamini inafungua malango ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na hivyo kuwakirimia waja wake mafuriko ya neema. Mwinjili Yohane mwishoni wa dibaji yake anasema: “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.” Yn. 1:18. Kwa hakika waamini walikuwa hawafahamu namna nzuri ya kusali; maneno gani wangeweza kutumia, hisia na pengine, lugha gani ambayo wangepaswa kuitumia ili sala zao ziweze kueleweka mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii ni hali ambayo ilijionesha hata miongoni mwa Mitume wa Yesu, kiasi cha kumwomba ili aweze kuwafundisha namna bora zaidi ya kusali. Ombi hili la Mitume wa Yesu ni kielelezo cha “litania ya malalamiko ya binadamu, marudio ya sala zake na mapungufu yake kiasi cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu kwa kusema “Bwana, utufundishe sisi kusali”. Lk. 11: 1. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba sala zote hazilingani na wala si zote zenye muafaka. Maandiko Matakatifu yanasimulia ushuhuda wa sala mbaya zinazotolewa na waamini, kiasi hata cha kushindwa kupokelewa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Pengine mara nyingi sana Mwenyezi hafurahii sala zinazotolewa na waja wake, lakini wao wanaendelea tu bila hata wao wenyewe kujitambua. Mwenyezi Mungu anaangalia mikono ya mtu anayesali! Ili kweli mikono iweze kuwa safi, si lazima mtu “anawe na maji tiririka” ili kuitakatisha kama wanavyokazia wataalam wa tiba ya magonjwa ya binadamu. Jambo la msingi kwa mwamini wakati wa sala ni kujiondoa katika matendo yasiyofaa wala kumpendeza Mungu. Kwa kutambua udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu Mtakatifu Francisko wa Assisi alizoea kusema kwamba, hakuna mtu anayestahili kulitamka jina la Mwenyezi Mungu. Umaskini wa sala ya mwanadamu umeshuhudiwa kwa namna ya pekee kabisa na maneno ya Akida wa Kapernaumu aliyemwendea Kristo Yesu na kumtaka aseme neno moja tu na mtumishi wake atapona. Akida huyu alijitambua kuwa mbele ya Kristo Yesu, si mali kitu! Hakuwa wala Myahudi na mbaya zaidi alikuwa ni askari aliyekuwa anachukiwa na watu waliomzunguka, kwani alionekana kama “mvamizi”. Lakini usalama na afya ya mtumishi wake, inamsukuma kiasi cha kumfanya athubutu kusema “Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona”. Mt. 8:8.

Haya ni maneno ambayo waamini wanayarudia wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kujadiliana na Mwenyezi Mungu ni neema ya pekee, kwani kimsingi mwanadamu hasitahili hata kidogo wala hana haki, daima anachechemea katika maneno na mawazo yake! Lakini jambo la kushangaza ni lile la kutambua kwamba, Kristo Yesu ni lango linalofunguka tayari kusikiliza na kujibu sala za waja wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, binadamu anapendwa na Mwenyezi Mungu. Wanafalsafa wengi wanasema, kimsingi binadamu ni wakorofi, ni watu wenye makelele kibao, kumbe, wanapaswa kupuuzwa. Mwanafalsafa Aristotle alikwenda mbali na kusema, Mwenyezi Mungu anaweza kujifikiria peke yake. Kumbe, mwanadamu anapaswa kujiongeza ili matendo yake yaweze kumpendeza Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, binadamu alipaswa kutoa sadaka na kufanya ibada mara kwa mara ili kumshukuru Mwenyezi Mungu bubu na kiziwi.

Kristo Yesu amewafunulia waja wake umuhimu wa kuzungumzana na Mwenyezi Mungu katika maisha, kwa sababu Mungu anaonesha ukaribu wake kwa wale wote wanaomtafuta kwa moyo mnyofu. Ni kwa njia ya ufunuo wa Kristo Yesu, mwanadamu ametambua kwamba, kuna Mwenyezi Mungu anayempenda na kumthamini mwanadamu, kiasi kwamba, mwanadamu huyu amepata ujasiri wa kumwamini. Hiki ndicho kielelezo cha “Kashfa ya Baba mwenye huruma” au yule mchungaji mwema, au mfano wa shilingi iliyopotea. Rej. Lk. 15. Mifano yote hii isingeliweza kufahamika barabara, ikiwa kama mwanadamu asingebahatika kukutana na Kristo Yesu. Ni Mungu wa namna gani ambaye anathubutu kuuwawa kwa ajili ya binadamu? Je, ni Mungu wa wapi anapenda upeo bila masharti ya kutaka kupendwa tena? Ni Mungu gani ambaye anathubutu kumgawia mtoto wake sehemu ya urithi wake na baadaye anautapanya kwa maisha ya uasherati? Rej. Lk. 15, 12-13.

Huu ndio ushuhuda uliotangazwa na kunafsishwa na Kristo Yesu kwamba, hakuna Baba mwenye huruma kama Mungu wetu “Tam Pater nemo”. Si rahisi sana kwa mwanadamu kufahamu undani wa Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani: Mungu Baba Mwenyezi, Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya ulimwengu mzima. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa kuonesha ukaribu, huruma, upendo na msamaha wake usiokuwa na kifani. Lilikuwa ni jambo la kufikirika tu kwamba upendo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu ungeweza kushuka na kuzama katika undani wa mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanafafanua jambo hili kwa kusema, “Hakuna njia nyingine ya sala ya Kikristo zaidi ya Kristo. Sala yetu, iwe ya jumuiya au ya mtu binafsi, ya mdomo au ndani haiwezi kumfikia Baba isipokuwa tunasali “katika jina” la Yesu. Ubinadamu Mtakatifu wa Yesu ni njia ambayo kwayo Roho Mtakatifu hutufundisha kumwomba Mungu Baba yetu”. KKK 2664. Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ndiyo neema ya imani ya Kikristo. Isingewezekana kuwa na wito mkubwa zaidi, bali kwa njia ya Fumbo la Umwilisho wa Kristo Yesu, ameweza kuwashirikisha maisha ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Katekesi Sala
03 March 2021, 16:11