Baba Mtakatifu Francisko amawapongeza wanachama wa FIDESCO yaani: Imani na Ushirikiano kwa kuadhimisha kumbukizi la miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Francisko amawapongeza wanachama wa FIDESCO yaani: Imani na Ushirikiano kwa kuadhimisha kumbukizi la miaka 40 tangu kuanzishwa kwake.  

Papa Francisko: FIDESCO Miaka 40 ya Injili ya Huduma kwa Jirani

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi na wanachama wa FIDESCO, kuishi utume wao, huku wakikita mahusiano na mafungamano yao ya dhati na Kristo Yesu, kwa kushuhudia ari ya kuishi Injili katika udugu na haki. Kwa hakika, wanahitaji muda wa faragha wanapokumbana na nyakati ngumu na upweke; wanapokatishwa tamaa na kupoteza dira na mwelekeo. Injili ya huduma

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

FIDESCO ni Shirika la Kanisa Katoliki la Watu wa Kujitolea Kimataifa lililoanzishwa kunako mwaka 1981 na Jumuiya ya Emmanuel kutoka nchini Ufaransa, baada ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki kutoka Barani Afrika waliokutana mjini Vatican. Lengo lilikuwa ni kuendeleza ushirikiano wa Kimataifa kati ya nchi za Kaskazini na Kusini mwa Ulimwengu katika masuala ya elimu, afya, kilimo, ustawi na maendeleo ya jamii katika ujumla wake. Ushirikiano huu kwa ajili ya mafao ya wengi bila kuangalia: dini, kabila, utamaduni au mahali anapotoka mtu. FIDESCO kirefu chake ni “Fidei-Co yaani “Imani na Ushirikiano”. Kwa sasa Shirika hili limeenea sehemu mbalimbali za dunia na kwa upande wa Bara la Afrika lina ofisi zake nchini DRC na Rwanda. FIDESCO inaadhimisha kumbukizi la miaka 40 tangu kuanzishwa kwake kwa ajili ya huduma kwa Kanisa sanjari na kuendeleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Ni Shirika ambalo linakita mizizi yake katika matendo kama ushuhuda wa imani tendaji, kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; kiini cha maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Viongozi na wanachama wa Shirika hili, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kupyaisha maisha yao ya kiroho, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani hususan katika kipindi hiki cha Kwaresima. Ni imani katika matendo, inayowahakikishia jirani zao zao ile ari, mwamko na furaha ya Injili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 20 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na wanachama wa FIDESCO, kama sehemu ya kumbukizi la miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni changamoto ya kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika huduma za kijamii, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya Uinjilishaji na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ni mwelekeo wa kuukubali uinjilishaji wa awali, unaowaalika waamini kupokea upendo wa Mungu na kujibu kwa kumpenda Mungu kwa upendo ule ule ambao ni zawadi yake kwa binadamu. Na hii ni chemchemi ambayo huibua katika maisha na matendo ya waamini jibu ambalo ni la kimsingi na kiasili yaani: kutamani, kutafuta na kulinda yaliyo mema kwa mafao ya wengine. Rej. EG, 178.

Kumbe, FIDESCO inapania kutoa huduma kwa jirani na wenye uhitaji zaidi, kwa kutambua kwamba, hata wao ni watoto wapenzi wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wake, wenye utu na heshima zao. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa sasa Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Kristo Yesu mteseka, anaendelea kujifunua, kujitambulisha na kujifungamanisha na maskini, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wagonjwa na wenye njaa bila kuwasahau wale wote wanaobeba Fumbo la Msalaba pamoja na Kristo Yesu. FIDESCO wanayo bahati ya kuweza kuliishi Fumbo hili pamoja na kuendelea kujichotea nguvu kutoka katika chemchemi hii ya imani. Hii inatokana na imani kwamba, Kristo Yesu alimwaga Damu yake azizi kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika wasiwasi wowote kuhusu upendo usio na mipaka unaoikweza hadhi ya binadamu wote.

Kila mtu anastahili kupewa heshima hii kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi na wanachama wa FIDESCO, kuishi utume wao, huku wakikita mahusiano na mafungamano yao ya dhati na Kristo Yesu, kwa kushuhudia ari ya kuishi Injili katika udugu na haki. Kwa hakika, wanahitaji muda wa faragha wanapokumbana na nyakati ngumu na upweke; wanapokatishwa tamaa na kupoteza dira na mwelekeo. Mama Kanisa analishuruku FIDESCO kwa kazi kubwa iliyotenda katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Huu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu, aliyekuja kuwakomboa wanadamu wote. Huu ni mshikamano unaomwambata mtu mzima sanjari na mahitaji yake ya kutaka kuingizwa katika jamii, kwa kusaidia mchakato wao wa kukua kiakili, kitamaduni na kiroho, kila mtu akipewa hadhi yake kama binadamu.

FIDESCO hawana budi kuendelea kujichimbia katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, waamini wenyewe wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Ni muda muafaka wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini duniani, kwa kujenga Ufalme wa Mungu na kudumisha udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika haki, amani, utu na heshima ya binadamu. Kanisa linaendelea kujibidiisha katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe, kila mtu katika nafsi yake kuendelea kujipyaisha kiimani na kiutu kwa kutambua kwamba, wao ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu, wanaotumiwa na Mwenyezi Mungu kama mashuhuda na vyombo vyake vya huruma kwa jirani zao. “Basi iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” Lk. 6:36. Mwelekeo huu unapenyeza pia katika maisha ya kiroho kama jibu la zawadi ya Mungu. Kanisa linatambua na kumshukuru Mungu kwa FIDESCO kutoa fursa kwa vijana wa kizazi kipya ya kukua katika imani na utu wema.

Fidesco

 

 

21 March 2021, 15:36