Tafuta

Vatican News
Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Machi 2021: Sakramenti ya Upatanisho. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Machi 2021: Sakramenti ya Upatanisho.  (AFP or licensors)

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Machi 2021: Sakramenti ya Upatanisho

Sakramenti ya Upatanisho ni mahali ambapo mwamini anakimbilia kiti cha huruma ya Mungu ili apate kugangwa na kuiponya roho yake. Lengo ni kupata afya bora zaidi ya maisha ya kiroho. Huu ni mchakato unaomwondoa mwamini kutoka katika mahangaiko na kuzamishwa katika huruma ya Mungu. Kitovu cha maungamo ni upendo wa Mungu ambao mwamini anaupokea na kuuhitaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni Uso wa huruma ya Baba. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. Ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu ambao ni kiini cha Injili; huruma ambayo kimsingi inapaswa kupenya na kugota katika moyo na akili ya binadamu. Kanisa linapaswa kuwaendea wote pasi na ubaguzi kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni ushuhuda unaofumbata huruma ya Mungu, mwanga na njia inayowaelekeza watu kwa Baba wa milele! Huruma ya Mungu ni sehemu ya mpango wa maisha unaoleta furaha na amani ya ndani! Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayoadhimishwa kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Upatanisho! Msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono dhaifu, ili kumwezesha mwamini kuachilia mbali hasira, ghadhabu, ukatili na kisasi ili kuishi kwa furaha.

Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika zaidi ili watoto wake waweze kuwa na afya bora zaidi. Wakati umewadia kwa Mama Kanisa kuitikia kwa mara nyingine tena wito huu wa furaha na msamaha. Ni wakati wa kurejea kwenye msingi wa imani na kubeba madhaifu na mahangaiko ya jirani. Huruma ya Mungu ni msukumo unaowaamsha waamini kwa maisha mapya na hivyo kuwatia ujasiri wa kuangalia wakati ujao kwa matumaini. Msamaha wa dhambi zilizotendwa baada ya Ubatizo hutolewa kwa Sakramenti ya pekee iitwayo: Sakramenti ya uongofu, ungamo, kitubio na upatanisho. Sakramenti hii inaundwa na matendo makuu matatu: Kutubu, Kuungama na Kutimiza Malipizi. Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa: Mwana wa Mungu alijifanya mtu ili kutuokoa na aliamua kulihusisha Kanisa kama "chombo cha lazima" katika kazi hii ya wokovu, na ndani yake, wale aliowachagua, akawaita na kuwaweka wawe wahudumu wake. Ili kuelezea ukweli huu, daima Kanisa limefundisha kwamba mapadri, katika maadhimisho ya Sakramenti, hutenda “in persona Christi capitis”, yaani, katika nafsi ya Kristo aliye Kichwa: «Kristo huturuhusu sisi kutumia “Mimi”, twanena katika “Mimi” ya Kristo, Kristo “anatuvuta ndani mwake” na kuturuhusu kuungana. Hutuunganisha na 'Mimi' yake. [...] Ni muungano huu na 'Mimi' yake ambao huthibitishwa katika maneno ya wakfu. Pia katika “Nakuondolea dhambi” kwa sababu hakuna yeyote kati yetu anayeweza kusamehe dhambi - ni “Mimi” ya Kristo, ya Mungu, ambayo ndiyo pekee ina uwezo wa kuondolea dhambi».

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Machi 2021 kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anapenda kujielekeza zaidi katika Sakramenti ya Upatanisho. Hapa ni mahali ambapo mwamini anakimbilia kiti cha huruma ya Mungu ili kuungama, apate kugangwa na kuiponya roho yake. Ili hatimaye, aweze kupata afya bora zaidi ya maisha ya kiroho. Huu ni mchakato unaomwondoa mwamini kutoka katika mahangaiko na kuzamishwa katika huruma ya Mungu. Kitovu cha maungamo ya dhambi si dhambi zinazoungamwa, bali ni upendo wa Mungu ambao mwamini anaupokea na ambao anauhitaji daima. Kitovu cha maungamo ni Kristo Yesu mwenyewe ambaye anawasubiri, anayewasikiliza na kuwasamehe dhambi zao. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba: Kwenye moyo wa Mungu, binadamu anatangulia kuliko makosa yake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kusali ili waweze kupata uzoefu wa Sakramenti ya Upatanisho yenye kina kipya, ili kuonja msamaha na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Waamini wasali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kulikirimia Kanisa lake mapadre wenye huruma na wala sio mapadre wanaowatesa waamini.

Kwa upande wake, Padre Frédéric Fornos S.J., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakaza kusema, Baba Mtakatifu katika nia zake za Mwezi Machi 2021 anapenda kuliaminisha Kanisa Katoliki ujumbe uliosheheni matumaini. Anawaalika waamini kugundua tena ndani mwao nguvu ya upyaisho inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho, ili hatimaye, kuonja msamaha na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Mara kadhaa, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa “akikimbilia kiti cha huruma ya Mungu, ili kugangwa na kuponywa na huruma ya Mungu. Katika Sakramenti ya Upatanisho, Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hapa ni mahali ambapo, mwamini anakutana mubashara na huruma na upendo wa Mungu bila kujali dhambi, sheria, kanuni, taratibu, hukumu pamoja na udhaifu wa binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu alijalie Kanisa lake, Mapadre wema na wenye huruma na sio wale wanaowatesa na kuwanyanyasa waamini katika kiti cha huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza kwa mara nyingine tena Mapadre kujiandaa kwa makini ili kutoa huduma ya Sakramenti ya Upatanisho ambayo ndiyo utume halisi wa Kipadre. Anawashukuru na kuwaomba wawakaribishe waamini wote kama mashuhuda wa upendo wa Kibaba, licha ya uzito wa dhambi; wawe wenye juhudi katika kusaidia kutafakari juu ya maovu yaliyotendeka¸wawe wazi katika kusisitiza kanuni msingi za kimaadili; wawe tayari kuwasindikiza waamini katika safari ya toba, wakitembea nao hatua kwa hatua kwa uvumilivu; wawe na busara katika kupambanua kila tatizo la kila mmoja. Mapadre wawe wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Kama Yesu mbele ya mwanamke mzinzi alivyochagua kubaki kimya ili kumwokoa katika hukumu ya kifo, vivyo hivyo na Padre awe mnyenyekevu wa moyo, akijua kwamba kila mwamini anayetubu dhambi zake, anamkumbushia pia yeye mwenyewe alivyo: mwenye dhambi, lakini mhudumu wa huruma.

Mapadre waungamishaji wanajua vizuri ni watu wangapi wanaodhihirisha wongofu wao wakiwa mbele ya macho yao. Kwa hiyo, wajitahidi kutumia vitendo na maneno ambavyo vitaweza kumgusa mtima mwa moyowa mwamini anayetubu kusudi agundue jinsi alivyo karibu naye kwa upendo Mungu Baba mwenye kusamehe. Waungamishaji wasibatilishe nafasi hizi kwa vitendo ambavyo vinaweza kupinga hamu ya kupewa huruma. Badala yake, wasaidie kuangaza dhamira ya kila mmoja kwa mwanga wa upendo wa Mungu usio na mipaka (Taz. 1Yoh 3:20). Sakramenti ya Upatanisho inahitaji kupewa nafasi yake katika kiini cha maisha ya kikristo; ndiyo maana inadai wawepo makuhani wanaoweka maisha yao tayari kwa kuitumikia “huduma ya upatanisho” (2Kor 5:18), kwa namna ya kwamba, pamoja na kutomzuia yeyote, mwenye majuto ya dhati, asiujongee upendo wa Mungu Baba anayesubiri kurudi kwake, waamini wote wajaliwe nafasi na uwezo wa kuonja nguvu zenye kuokoa za msamaha. (Rej. Misericordia et misera no. 10 na 11).

Papa Nia Machi

 

02 March 2021, 16:41