Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Wazazi na walezi wanahimizwa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wao pamoja na kukuza ibada kwa Mtakatifu Yosefu Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Wazazi na walezi wanahimizwa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wao pamoja na kukuza ibada kwa Mtakatifu Yosefu 

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: 8 Desemba 2020 - 8 Desemba 2021!

Baba Mtakatifu Francisko asema: Yosefu Mtakatifu ni mtu asiyependa makuu, aliyetekeleza dhamana na wajibu wake katika Familia Takatifu kwa umakini mkubwa. Awe ni mfano bora wa kuigwa na mwombezi wa familia za Kikristo wakati wa raha na machungu, ili kamwe familia zisitindikiwe mafuta ya imani na furaha inayobubujika kwa kuungana na Mwenyezi Mungu. Ibada na Ulinzi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu. Anasema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Mei 2021 ameendelea kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, shuhuda wa maisha ya kila siku, anayeonesha uwepo wake mwanana. Yosefu Mtakatifu ni mtu asiyependa makuu, aliyetekeleza dhamana na wajibu wake katika Familia Takatifu kwa umakini mkubwa. Awe ni mfano bora wa kuigwa na mwombezi wa familia za Kikristo wakati wa raha na machungu, ili kamwe familia zisitindikiwe mafuta ya imani na furaha inayobubujika kwa kuungana na Mwenyezi Mungu.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Matumaini ni sawa na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Baba Mtakatifu anasema, Kwaresima ni muda muafaka wa kusali zaidi, kukuza na kudumisha ushiriki mkamilifu katika Sakramenti za Kanisa.

Ni wakati wa kufunga, kusali, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lengo ni kuwawezesha waamini kuzama zaidi katika upendo na huruma ya Mungu kama ilivyofunuliwa na Kristo Yesu na hatimaye, kumiminwa na Roho Mtakatifu katika nyoyo za waamini. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchangamkia kipindi hiki cha neema, toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anawatakia watu wote wa Mungu safari njema katika Kipindi hiki cha Kwaresima kwa mwaka 2021. Wawe tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka, huku wakiwa na mioyo iliyotakasika na kupyaishwa kwa neema za Roho Mtakatifu ambaye ni Mwalimu wa maisha ya kiroho, anayewasaidia waamini kufanana na Kristo Yesu kwa njia ya sala na ufuasi mkamilifu!

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu

 

 

03 March 2021, 15:49