Mpango Mkakati wa Saa 24 Kwa Ajili ya Mwaka kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Akusamehe maovu yako yote" Zab. 103:3 Mpango Mkakati wa Saa 24 Kwa Ajili ya Mwaka kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Akusamehe maovu yako yote" Zab. 103:3 

Mpango Mkakati wa Saa 24 Kwa Ajili ya Bwana 2021: Toba Kamili

Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima: Tarehe 12-13 Machi 2021. Kauli mbiu: “Akusamehe maovu yako yote” Zab. 103:3. Kila Jimbo linapaswa kujiandaa kikamilifu ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye kutimiza malipizi yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja: Upendo, huruma na msamaha wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya: imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na kwa mwaka huu ni tarehe 12-13 Machi 2021. Mpango huu unanogeshwa na kauli mbiu “Akusamehe maovu yako yote” Zab. 103:3. Kila Jimbo linapaswa kujiandaa kikamilifu ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye kutimiza malipizi. Lengo ni kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kadiri ya mazingira na hali halisi ya wakati huu wa mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Iwe ni fursa kwa waamini pia kusali na kuabudu Ekaristi Takatifu. Mpango huu unahitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu, Jumamosi jioni. Mababa wa Kanisa wanasema, toba inapotokana na upendo wa Mungu, anayependwa kuliko vitu vyote, huitwa “kamili” yaani “toba ya mapendo”.

Toba ya aina hii huondoa makosa madogo; pia hupata msamaha wa dhambi za mauti endapo inakwenda pamoja na kusudi thabiti la kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho mapema iwezekanavyo! Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, anapenda kuwakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe, si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa upole na umakini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina, kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana”, ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Baba wa milele. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. Ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu ambao ni kiini cha Injili; huruma ambayo kimsingi inapaswa kupenya na kugota katika moyo na akili ya binadamu. Kanisa linapaswa kuwaendea wote pasi na ubaguzi kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni ushuhuda unaofumbata huruma ya Mungu, mwanga na njia inayowaelekeza watu kwa Baba wa milele! Huruma ya Mungu ni sehemu ya mpango wa maisha unaoleta furaha na amani ya ndani! Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayoadhimishwa kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Upatanisho! Msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono dhaifu, ili kumwezesha mwamini kuachilia mbali hasira, ghadhabu, ukatili na kisasi ili kuishi kwa furaha.

Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika zaidi ili watoto wake waweze kuwa na afya bora zaidi. Wakati umewadia kwa Mama Kanisa kuitikia kwa mara nyingine tena wito huu wa furaha na msamaha. Ni wakati wa kurejea kwenye msingi wa imani na kubeba madhaifu na mahangaiko ya jirani. Huruma ya Mungu ni msukumo unaowaamsha waamini kwa maisha mapya na hivyo kuwatia ujasiri wa kuangalia wakati ujao kwa matumaini. Msamaha wa dhambi zilizotendwa baada ya Ubatizo hutolewa kwa Sakramenti ya pekee iitwayo: Sakramenti ya uongofu, ungamo, kitubio na upatanisho. Sakramenti hii inaundwa na matendo makuu matatu: Kutubu, Kuungama na Kutimiza Malipizi. Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa: Mwana wa Mungu alijifanya mtu ili kutuokoa na aliamua kulihusisha Kanisa kama "chombo cha lazima" katika kazi hii ya wokovu, na ndani yake, wale aliowachagua, akawaita na kuwaweka wawe wahudumu wake.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujizatiti kikamilifu katika hija ya Kipindi cha Kwaresima, yaani Siku 40 katika Jangwa la maisha ya kiroho kwa: toba na wongofu wa ndani; kufunga, kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu. Yote haya yanapaswa kunafsishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Anasema matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao ya kiroho. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Kristo Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, aliwafunuliwa wafuasi wake kiini cha maisha na utume wake, alipowashirikisha kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kama utekelezaji wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na hivyo kuwaalika wanafunzi wake kushiriki kikamilifu katika utume wake wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayowakumbusha waamini kuhusu Kristo Yesu: “tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba.” Flp. 2:8. Pale inapowezekana, Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kushiriki Ibada hii kwa uchaji, kama njia ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Waamini watambue kwamba, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa njia hii, waamini nao wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Hii ni huruma inayopaswa pia kushuhudiwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho inayogusa undani wa mtu, kwani hili ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani. Ni huruma inayosamehe na kuokoa. Mapadre waungamishi wanao wajibu wa kuwa ni watumishi waaminifu wa: upendo, huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu, kwa kuwapokea waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma katika mfano wa Mwana mpotevu!

Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kumrudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni Sakramenti inayomfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma ya Mungu, ili kupata amani na utulivu wa ndani! Katika Kesha la Pasaka, Mama Kanisa atawasha Mshumaa wa Pasaka kwa moto mpya ambao pole pole utalifukuza giza na kuwaangaza waamini watakaokuwa kwenye maadhimisho ya Liturujia. Mwanga wa Kristo Mfufuka katika utukufu unaofukuzia mbali giza la moyo na roho, ili wote waweze kuishi katika mang’amuzi ya wanafunzi wa Emmau: kwa kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa kwa Ekaristi Takatifu itakayoiwezesha mioyo yao kuweza kuwaka tena moto wa imani, matumaini na mapendo!

Mpango Mkakati 24hrs
11 March 2021, 16:23