Watu wa Mungu nchini Iraq wanaendelea kukamilisha maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021. Majadiliano, Amani, Ustawi na Mafao ya wengi. Watu wa Mungu nchini Iraq wanaendelea kukamilisha maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021. Majadiliano, Amani, Ustawi na Mafao ya wengi. 

Hija ya Kitume ya Papa Nchini Iraq: Sala Ya Watu wa Mungu Iraq

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Iraq imezamwishwa mikononi mwa Kristo mwenyewe kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, ili maneno na matendo ya Papa wakati wa hija yake yawaguse na kuwaangaza wote watakaokutana naye na kumsikiliza. Maneno na matendo yake yawe ni zawadi ya ujasiri, faraja na daraja la kuwakutanisha watu wa Mungu hata katika tofauti zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hija za kitume ni muhimu sana katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nyenzo ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Serikali mbalimbali duniani. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inapenda kuheshimu Mikataba na Itifaki mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kitume nchini Iraq, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8.

Kardinali Louis Raphaël Sako wa kwanza, Patriaki wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo, anasema, Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq imewekwa na kuzamishwa mikononi mwa Kristo mwenyewe kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, ili maneno na matendo ya Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume, yawaguse na kuwaangaza wale wote watakaokutana na kumsikiliza. Maneno na matendo yake yawe ni zawadi ya ujasiri, faraja na daraja la kuwakutanisha watu wa Mungu katika tofauti zao msingi za kikabila, kitamaduni na kidini; ili wote kwa pamoja waweze kuzama katika mchakato wa upatanisho na ushirikiano wa kidugu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Waamini wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo nchini Iraq wanamwomba Mwenyezi Mungu awajalie faraja, mwanga na nguvu, ili kamwe wasichoke kuwa ni vyombo na wajenzi wa udugu wa kibinadamu na amani ya kweli. Waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awangalie watu wake huko Mashariki ya Kati na kuwaondolea chuki, uhasama na vita. Watu wa Mungu nchini Iraq wanaendelea na sala kwa ajili ya kufanikisha Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, inayonogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8.

Papa Iraq

 

 

 

 

 

 

01 March 2021, 15:13