Papa Francisko katika Sala yake kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa vita, ghasia na mashambulizi ya kigaidi amekazia umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kwani wote ni ndugu wamoja. Papa Francisko katika Sala yake kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa vita, ghasia na mashambulizi ya kigaidi amekazia umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kwani wote ni ndugu wamoja. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Sala Kwa Wahanga!

Papa amewaombea wale wote waliofariki dunia wakati wa vita, ghasia na vitendo vya kigaidi. Mwenyezi Mungu ni kiini cha maisha, kumbe ni dhambi kwa waamini kuuwana katika jina la Mungu. Mwenyezi Mungu ni asili ya amani, hivyo ni kosa kubwa kuanzisha vita na ghasia kwa kutumia Jina lake Takatifu. Mungu ni kisima cha upendo, hivyo ni dhambi kubwa kwa waamini kuchukiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Iraq anataka kuwahamasisha watu wa Mungu nchini humo kusimama kidete dhidi ya: rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma. Wawe tayari kupinga mifumo yote ya kibaguzi, ili kila mwananchi aweze kuwajibika barabara katika ujenzi wa nchi yake; kwa kuwa na haki na nyajibu sawa. Hija hii pamoja na mambo mengine inapania kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, umoja, ushirikiano na maridhiano ya kidugu. Baba Mtakatifu anapania kuwahamasisha Waislam na Wakristo kuimarisha udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu katika Sala kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa vita, ghasia na vitendo vya kigaidi, Jumapili tarehe 7 Machi 2021 amekazia umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wakitambua kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu wote ni ndugu wamoja! Baba Mtakatifu amewaombea wale wote waliofariki dunia wakati wa vita, ghasia na vitendo vya kigaidi nchini Iraq na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha maisha, kumbe ni dhambi kwa waamini kuuwana katika jina la Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ni asili ya amani, hivyo ni kosa kubwa kuanzisha vita na ghasia kwa kutumia Jina lake Takatifu. Mwenyezi Mungu ni kisima cha upendo, hivyo ni dhambi kubwa kwa waamini kuchukiana.

Baba Mtakatifu anaomba na kusali kwamba, Mwenyezi Mungu apende kuwapokea, kuwajalia uzima wa milele na amani, watu wote waliofariki dunia kwa sababu ya vita, ghasia na vitendo vya kigaidi. Amewaalika pia waamini wa dini mbalimbali kujiombea wao wenyewe katika tofauti zao za Mapokeo yao kiimani, wajitahidi kuishi katika amani na utulivu wakitambua kwamba, wote hao machoni pa Mwenyezi Mungu ni ndugu wamoja. Amemshukuru Mwenyezi Mungu anaendelea kuwashushia baraka viumbe vyake, licha ya bahari ya mateso na kifo; kishawishi cha ghasia, ukosefu wa haki, uchu wa mali na madaraka, lakini bado Mwenyezi Mungu anawasindikiza watoto wake kwa upendo wenye huruma. Licha upendo wenye huruma, lakini binadamu ameendelea kuitumia vibaya zaidi huruma hii kiasi hata cha kumezwa na malimwengu na hivyo kusahau fadhila ya amani na utulivu. Ni watu ambao wanajishughulisha kwa ajili ya mambo yao binafsi, kiasi hata cha kumgeuzia kisogo Mwenyezi Mungu na jirani; kwa kufunga lango la amani kwa ajili ya watu wengine.

Neno la Bwana lilimjia Nabii Yona na kusema kwa maana uovu wao umepanda juu mbele ya Mungu. Rej. Yon.1:2. Wakati wa Sala na Liturujia hawakuinua mikono juu mbinguni iliyotakata. Rej. 1 Tim 2:8. Na badala yake, kutoka ardhini, kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia imepanda juu.  Mwa. 4:10. Katika Kitabu cha Nabii Yona, wananchi wa Ninawi waliyasikiliza maneno ya Nabii, wakatubu na kumwongokea Mungu aliyewakirimia wokovu. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka watu wote waliofariki dunia kutokana na chuki za kibinadamu kwenye huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anaomba pia msamaha na neema ya toba na wongofu wa ndani. Katika mji wa Mosul kuna alama mbili za kudumu zinazo onesha ile kiu ya binadamu kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, yaani Msikiti mkuu wa A-Nouri na kinara chake cha Al-Hadba pamoja na Kanisa la Bikira Maria Mama wa Muda, ambalo mnara wake wa saa kwa zaidi ya miaka mia moja, umewakumbusha wanadamu kwamba, maisha ni kito cha thamani.

Waamini wanamwomba Mwenyezi awafundishe kutambua kwamba, amewakabidhi mpango wa upendo, amani na upatanisho na kuwataka kuutekeleza kwa wakati wanapokuwa bado wanaishi hapa duniani. Mwenyezi Mungu awasaidie kutambua kwamba, ni kwa njia ya kuweka hayo yote mara moja katika vitendo, mji wa Mosul na Iraq katika ujumla wake itaweza kuanza kujengwa na zile nyoyo zilizopondeka na kuvunjika kwa sababu ya mateso zitaweza kuponywa. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kutumia vyema muda wao kama mtu binafsi na katika makundi kwa ajili ya kuendeleza mpango wake wa upendo. Pale wanapoteleza na kukengeuka, awajalie neema ya kusikiliza tena sauti ya watu wa Mungu, tayari kutubu na kumwongokea Mungu kwa wakati na kamwe wasielemewe na mawazo ya uharibifu na kifo! Baba Mtakatifu amewaweka watu wote ambao muda wao wa kuishi hapa duniani ulikatishwa kutokana na mauaji yaliyofanywa na ndugu zao wenyewe. Wote hawa waweze kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kuguswa na nguvu ya huruma ya Mungu.

Requiem æternam dona eis, Domine, et lux perpetua luceat eis. Requiescant in pace. Amen. Baada ya sala hii, Baba Mtakatifu alimrusha juu njiwa mweupe, alama ya amani kwa watu wa Mungu nchini Iraq. Amesalimiana na viongozi mbalimbali wa kidini na kiserikali na baadaye akapanda ndege kuelekea Qaraqosh kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili kutembelea na kusalimiana na Wanajumuiya ya Qaraqosh pamoja na kusali nao Sala ya Malaika wa Bwana.

Papa Sala

 

07 March 2021, 16:53