Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Iraq amekazia zaidi msamaha na upatanisho katika ukweli na haki ni tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Iraq amekazia zaidi msamaha na upatanisho katika ukweli na haki ni tunu msingi za maisha ya Kikristo. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Iraq: Msamaha na Upatanisho!

Msamaha ni muhimu sana ili kuendelea kujikita katika upendo na maisha ya Kikristo. Wakristo wasamehe bila ya kukata tamaa, watambue kwamba, msamaha ni changamoto endelevu, lakini kwa neema Mwenyezi Mungu anaweza kuwakirimia amani. Watu wanapaswa kusimama kidete ili kupinga vitendo vyote vya kigaidi pamoja na matumizi ya dini kwa mafao ya watu binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili lilianza kujengwa kunako mwaka 1932 na hatimaye, kutabarukiwa kunako mwaka 1948, baada ya kazi ngumu, sadaka na majitoleo ya watu wa Mungu kutoka katika Uwanda wa Ninawi. Sehemu hii ina historia ndefu katika maisha ya waamini wa dini mbalimbali, lakini kwa Wakristo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ni kielelezo cha imani na mateso mbali mbali. Hata leo hii watu wanaoishi katika eneo hili wamejaribiwa sana; wakasalitiwa hata na ndugu zao wenyewe; nyumba za ibada zikaharibiwa na kunajisiwa! Yote haya yalijitokeza kunako mwezi Agosti 2014, Kanisa hili likanajisiwa, likavunjwa na kuchomwa moto na na wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State, IS”. Huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kutoka huko Mashariki ya Kati, lakini kutokana na imani watu wameanza kurejea tena katika makazi yao ya awali, tayari kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo. Hiki kimekuwa ni kipindi cha ushuhuda wa imani kutoka kwa mashuhuda waliothubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani hakuna jambo lolote lile linaloweza kuwatenga waamini na upendo wa Kristo!

Mwezi Oktoba 2016 baada ya mji huu kukombolewa, Kanisa limekarabatiwa kutabarukiwa upya na hivyo kuanza kutumika tena kama nyumba ya Ibada na Sala. Kuanzia mwaka 2020 ukarabati mkubwa unaendelea kufanywa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hii ni hija inayofumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, uhamasishaji wa ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu akiwa nchini Iraq ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mungu msamaha na kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Ni hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Anaendelea kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini.

Ni katika muktadha huu, Jumapili tarehe 7 Machi 2021, Baba Mtakatifu ametembelea na kusali katika Jumuiya ya Qaraqosh. Amesikiliza shuhuda za waamini na viongozi wa Kanisa. Ameshuhudia uzuri na magofu ya nguvu ya uharibifu, chuki pamoja na vita pamoja na mchakato wa ujenzi wa Iraq mpya. Vitendo vya kigaidi na utamaduni wa kifo, kamwe havina sauti ya mwisho katika maisha ya mwanadamu, kwani hadi sasa macho ya imani na ushindi wa maisha dhidi ya kifo vinajidhihirisha hadharani. Jambo la msingi ni kwa waamini kudumu katika imani, matumaini pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayeendelea kuwategemeza kwa njia ya neema na baraka zake. Kuna amana na utajiri mkubwa ambao ni urithi kutoka klwa wahenga wao wanaopaswa kuuendeleza, kwani hii ndiyo nguvu yao. Huu ni wakati wa kuchakarika ili kuanza ujenzi wa Iraq mpya, kwa kuendelea kutegemea pia neema na baraka za Mungu anayeongoza hatima ya maisha ya kila mwanadamu. Watu wa Mungu nchini Iraq watambue kwamba, Kanisa liko pamoja nao kwa sala na sadaka inayomwilishwa katika ushuhuda wa huduma ya upendo. Wakati wa shida na mahangaiko yao, watu wengi walifungua mikono na nyoyo zao ili kuwasaidia kwa hali na mali.

Baba Mtakatifu amewaambia kwamba, huu ni wakati muafaka wa kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijumuiya na kijamii; kwa kuwawezesha vijana na wazee kutembea kwa pamoja kwa sababu wazee wana ndoto na vijana wana utabiri. Makundi haya mawili yanapounganika, vijana wanakuwa wepesi kumwilisha ndoto za wazee katika uhalisia wa maisha yao. Wazee wanakuwa ni vyombo vya kurithisha amana na utajiri waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu yaani: ardhi, utamaduni, mapokeo pamoja na imani. Daima waamini watambue na kuthamini asili na uwepo wao; mambo msingi yanayowafungamanisha pamoja na kuendeleza mizizi ya utambulisho wao. Katika safari ya imani, kuna wakati ambapo imani inaweza kujaribiwa kiasi cha mwamini kudhani kwamba, hakuna Mungu na kama yupo haoni wala kuguswa na mahangaiko ya waja wake. Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati wa vita na mashambulizi ya kigaidi nchini Iraq. Ndivyo ilivyo hata wakati huu wa janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambalo limesababisha mgogoro mkubwa wa kiafya na ukosefu wa uhakika wa usalama. Majanga yote haya yawakumbushe waamini kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao!

Kamwe wasichoke kuota ndoto wala kutindikiwa na matumaini kwa sababu mbinguni kuna umati mkubwa wa watakatifu wa Mungu wanaowasindikiza kwa sala. Lakini pia watambue kwamba, kuna watakatifu ambao ni majirani na wanaishi kati pamoja nao! Iraq ina umati mkubwa sana wa watakatifu mbinguni, hawa wawe ni wandani na wenza wa safari kwa ajili ya leo iliyo bora na kesho iliyo bora zaidi. Msamaha na upatanisho katika ukweli na haki ni tunu msingi za maisha ya Kikristo. Msamaha ni kipimo cha kanuni maadili mintarafu Injili ya Kristo Yesu, tofauti kabisa na tabia ya kulipizana kisasi kwa sera za “jino kwa jino; jicho kwa jicho”, kiasi hata cha kufikia wakati watu kuanza kunoa mapanga! Hii ni hatari kubwa sana kwa ulimwengu mamboleo, kwani kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kupatana ni mchakato wa utakatifu wa maisha. Msamaha ni muhimu sana ili kuendelea kujikita katika upendo na maisha ya Kikristo. Wakristo waoneshe jeuri ya kusamehe bila ya kukata tamaa, kwa kutambua kwamba, msamaha ni changamoto endelevu, lakini kwa neema na baraka, Mwenyezi Mungu anaweza kuwakirimia watu wake amani. Watu wanapaswa kusimama kidete ili kupinga vitendo vyote vya kigaidi pamoja na matumizi ya dini kwa mafao ya watu binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini wawe na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, wakati wa raha na shida; wakati wakiwa na afya njema au wagonjwa. Shukrani kwa Mwenyezi Mungu inapata chimbuko lake kwa kutambua karama na ahadi zake. Kumbukumbu ya mambo ya kale inaweka sawa mambo ya nyakati hizi na hivyo kuwaongoza waamini kwa yale yajayo. Shukrani kwa Mwenyezi Mungu ni kitendo cha neema na fursa ya kuweza kuomba tena: amani, msamaha na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya Iraq. Waamini waendelee kusali bila kuchoka kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa Injili ya uhai uweze kutamalaki; upatanisho na upendo wa kidugu viweze kuwaambata watu wote wa Mungu. Watu waheshimiane na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi, ili kujenga umoja na ushirikiano kati ya watu wenye mapenzi mema. Huu ni udugu wa kibinadamu unaotambua tunu msingi za ubinadamu zinazowawezesha kushirikiana, kujenga, kujadiliana, kusamehe na kukuwa kwa pamoja.

Baba Mtakatifu anapenda kuwaaminisha watu wa Mungu nchini Iraq chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa upendo. Kwa bahati mbaya sana, taswira ya Bikira Maria nchini Iraq imekashifiwa na kunajisiwa, lakini hata hivyo, Bikira Maria anaendelea kuwaangalia kwa huruma na mapendo, kwa faraja na hatimaye, kuwatia shime kuendelea kusadaka maisha, licha ya mabaya wanayowatendea. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wanawake wataheshimiwa, watalindwa na kupewa fursa ya kujiendeleza zaidi. Baadaye wote wamesali Sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu Francisko ameweka sahihi pia kwenye Kitabu cha Watu Mashuhuri kwa kuandika hivi: “Katika Kanisa hili lililoharibiwa na hatimaye kufanyiwa ukarabati, alama ya matumaini kwa watu wa Mungu Qaraqosh na Iraq katika ujumla wake, nina mwomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa Bikira Maria aweze kuwakirimia zawadi ya amani”.

Papa Qaraqosh
07 March 2021, 17:33