Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq: Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu. Tafakari: Heri za Mlimani kama mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq: Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu. Tafakari: Heri za Mlimani kama mafundisho makuu ya Kristo Yesu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Heri za Mlimani!

Heri za Mlimani zinamwilishwa katika ushuhuda wa maisha ya umaskini wa kiroho; rehema, moyo safi na wapatanishi katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Huu ni ushuhuda na kielelezo cha hekima ya Kristo iliyomwilishwa katika maisha ya wafuasi wake ni chachu ya mageuzi ulimwenguni. Hiki ni kielelezo makini cha upendo kwa Kristo Yesu, kwa sababu upendo huvumilia yote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 33 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Jumamosi jioni, tarehe 6 Machi 2021, Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu lililotabarukiwa kunako mwaka 1956 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba. Kunako mwaka 2018 kwa utashi wa Kardinali Louis Raphaël Sako wa kwanza, Patriaki wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo. Baba Mtakatifu Francisko amekita mahubiri yake katika mambo makuu matatu: Hekima, Ushuhuda na Ahadi ya Mungu. Watu wengi wamevutwa na kuhamasika sana kutafuta hekima, wale wenye uwezo wa kiuchumi wanazo fursa nyingi zaidi na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wana nafasi “kiduchu” sana katika kupata hekima. Kwa macho ya walimwengu, wale wenye hekima kidogo si mali kitu! Lakini wale waliobahatika wanaonekana kupendelewa zaidi.

Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu ni ufunuo wa hekima ya Mungu inayojidhihirisha katika Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Kwa macho ya walimwengu: matajiri, watu wenye nguvu na maarufu duniani, hao wanaonekana kana kwamba, wamebarikiwa sana. Lakini, Mwenyezi Mungu anatoa upendeleo wa pekee kwa maskini wa roho na wanyenyekevu; watu wenye huruma maana hata wao watahurumiwa. Mwaliko unaotolewa na Kristo Yesu ni kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani. Juu ya Msalaba, upendo ulishuhudiwa kuwa na nguvu zaidi kuliko hata dhambi. Upendo umekuwa ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani wakati wa shida na madhulumu yao. Upendo ni chemchemi ya nguvu hata kwa watu wa Mungu nchini Iraq walioteseka kutokana na maamuzi mbele, kwa kudhulumiwa utu, kiasi cha kunyanyaswa na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Yote haya yamepita, lakini nguvu ya upendo imeendelea kusimama imara. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwilisha Heri za Mlimani kama dira na mwongozo wa maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anasema, Heri za Mlimani zinamwilishwa katika ushuhuda wa maisha ya umaskini wa kiroho; rehema, moyo safi na wapatanishi katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Huu ni ushuhuda na kielelezo cha hekima ya Kristo iliyomwilishwa katika maisha ya wafuasi wake, ili kuwa ni chachu ya mageuzi katika ulimwengu mamboleo. Hiki ni kielelezo makini cha upendo kwa Kristo Yesu, kwa sababu upendo huvumilia yote. Biblia inafafanua kwa kina kuhusu upendo unaofumbata uvumilivu wa Mungu katika maisha ya waja wake, kiasi cha kuwasamehe watu wake dhambi zao, walipokosa uaminifu, wakakengeuka na kutumbukia katika dhambi za zamani. Uvumilivu upyaisha upendo unaopaswa kuboreshwa kila wakati kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu, ili kutokukatishwa tamaa unapokumbana na ubaya. Wapendanao hawawezi kujifungia katika ubinafsi wao pale mambo yanapowaendea mrama! Upendo hujibu daima kwa wema.

Upendo wa Mungu umesimikwa katika huruma. Mtakatifu Paulo anafafanua kwa kusema kwamba: Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Rej. 1Kor. 13:4-7. Baba Mtakatifu anasema, tofauti na kinzani katika maisha ni mambo ya kawaida, lakini hakuna sababu ya kushikiana “majambia” ili kumaliza tofauti hizi, bali waamini wanapaswa kujitahidi kuwa ni mashuhuda wa uvumilivu wa upendo wa Mungu. Na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anatekeleza ahadi zake. Hekima ya Kristo Yesu inafumbatwa kwa namna ya pekee katika Heri za Mlimani zinazoboreshwa kwa ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu wale wanaozimwilisha: Watafarijika, watairithi nchi, watashibishwa, watapata rehema, watamwona Mungu na hatimaye, wataitwa wana wa Mungu kwa maana Ufalme wa Mungu ni wao.

Mwenyezi Mungu alitekeleza ahadi zake, kwa Ibrahimu Baba wa imani katika uzee wake akapata mtoto. Musa akawaongoza Waisraeli kutoka utumwani Misri. Bikira Maria, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akawa Mama Mungu na Kanisa. Mtakatifu Petro aliyemkana Kristo Yesu mara tatu, akaimarishwa, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Matukio yote haya yanaelezea huruma na upendo wa Mungu katika kutekeleza ahadi zake. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Heri za Mlimani ni kwa ajili ya walio maskini, wenye huzuni, wenye upole, wenye njaa na kiu ya haki; wenye rehema na moyo safi; wapatanishi na wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki. Wote hawa, Mwenyezi Mungu ameahidi kwamba, majina yao yataandikwa “kwenye sakafu ya moyo” lakini zaidi yataandikwa mbinguni. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru Mungu pamoja nao kwa sababu hekima kutoka kwa wahenga ambayo imeshuhudiwa kwa nyakati mbalimbali na ikapendeza machoni pa Mungu. Hawa ndio mashuhuda wanaojitahidi kumwilisha Heri za Mlimani ili kumsaidia Mwenyezi Mungu kutekeleza ahadi yake ya amani.

Misa Takatifu

 

06 March 2021, 17:36