Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2021: Angalieni Tunapanda Kwenda Yerusalemu: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo. Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2021: Angalieni Tunapanda Kwenda Yerusalemu: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwaresima 2021: Fadhila za Kimungu!

Ujumbe wa Kwaresima 2021: Kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani: kukubali ukweli na kuushuhudia. Matumaini ni chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele. Upend na huruma kielelezo cha juu kabisa cha imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Kristo Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, aliwafunuliwa wafuasi wake kiini cha maisha na utume wake, alipowashirikisha kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kama utekelezaji wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na hivyo kuwaalika wanafunzi wake kushiriki kikamilifu katika utume wake wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayowakumbusha waamini kuhusu Kristo Yesu: “tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba.” Flp. 2:8.

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaopyaisha imani kwa kuchota maji hai kutoka katika matumaini, yanayomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani, anayewawezesha wote kujisikia kuwa ni ndugu wamoja! Katika mkesha wa Pasaka, Wakristo watarudia tena ahadi zao za Ubatizo na hivyo kuzaliwa na kuwa watu wapya chini ya uongozi tendaji wa Roho Mtakatifu. Hija ya Kipindi cha Kwaresima inaangazwa na mwanga wa Ufufuko ambao huchochea mawazo, mitazamo na maamuzi ya wafuasi wa Kristo Yesu. Kufunga, kusali na matendo ya huruma ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Njia ya ufukara, kwa kufunga na upendo kwa maskini pamoja na sala ni mambo yanayowawezesha waamini kuishi kiaminifu imani yao, matumaini na upendo wa kweli.

Katika sehemu ya kwanza, Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Huu ni mwaliko wa kukubali na kunafsisha ukweli kadiri ulivyofunuliwa na Kristo Yesu maana yake ni kwamba: kufungua mioyo yao kwa Neno la Mungu ambalo Mama Kanisa anakirithisha kizazi kimoja hadi kingine. Huu ni ujumbe kwa watu wote unaowawezesha waamini kufungua nyoyo zao kwa makuu ya Mungu anayewapenda upeo, hata kabla ya wao wenyewe kuanza kumpenda. Kristo Yesu ndiye ukweli huu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo aliutwaa ubinadamu na mapungufu yake, akawa njia ambayo iko wazi kwa wote. Hii ndiyo njia inayoelekea kwenye utimilifu wa maisha.

Kufunga na kujinyima ni fursa ya kutambua karama ya Mungu inayowawezesha watu wote kujisikia kuwa ni wamoja, watoto wa Baba mmoja, walioumbwa kwa sura na mfano wake na wote wanapata utimilifu ndani mwake.  Kufunga ni kielelezo cha upendo wa mashikamano na maskini na hivyo kujikusanyia upendo walioupokea, ili kuwashirikisha wengine. Kufunga kunawasaidia waamini kumpenda Mungu na jirani na hivyo kujitambulisha pamoja nao! Kwaresima ni kipindi cha kuamini na kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika maisha ya waja wake, ili hatimaye, aweze kuweka makazi yake kati yao. Huu ni wakati wa kuondokana na mambo yote yale yanayowadidimza chini. Mambo haya ni ulaji wa kupindukia, usakaji wa habari za kweli au hata habari za kughushi. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu anayewaendea waja wake “amejaa neema na kweli” Jn. 1: 14, yaani Mwana wa Mungu na Mkombozi wa binadamu.

Katika Sehemu ya Pili, Baba Mtakatifu Francisko anasema matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Kristo Yesu alipokutana na Mwanamke Msamaria kwenye kisima cha Yakobo, alitumia fursa hii kufafanua maana ya maji yaliyo hai, yaani Roho Mtakatifu atakayewapatia waja wake wakati maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, ili kuwawezesha kuwa na matumaini bila kuwakatisha tamaa, kwani baada ya siku tatu angeweza kufufuka kwa wafu, kama kielelezo cha huruma na upendo wa Baba yake wa mbinguni. Imani katika Kristo Yesu, haikomi kutokana na vurugu na ukosefu wa haki au dhambi zinazotesa upendo, bali ni kupokea kutoka katika Moyo wa Baba yake msamha wa dhambi. Katika nyakati hizi ambazo janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea “kutamalaki” inakuwa vigumu sana kuzungumzia fadhila ya matumaini.

Kimsingi, Kwaresima ni kipindi cha matumaini, waamini wanamrudia tena Mungu wao kwa toba na wongofu na wongofu wa ndani. Huyu ndiye Mungu anaendelea kuitegemeza kazi ya uumbaji licha ya upotevu wa viumbe hai, kushuka kwa ubora wa maisha ya mwanadamu pamoja na kudhoofika kwa jamii. Changamoto mbele ya waamini ni upatanisho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sakramenti ya Upatanisho ni chanzo msingi katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili baada ya kupata msamaha wa dhambi, waamini waweze pia kuwa ni vyombo vya msamaha wa Mungu na faraja kwa jirani zao wanaopitia katika mateso na majonzi makuu. Kwa njia ya msamaha wa dhambi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, katika mawazo na matendo yao, waamini wanaweza kuonja mang’amuzi ya Udugu wa Kipasaka.

Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kuendelea kufariji, kutia nguvu na shime ya kuweza kusonga mbele. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa jirani zao, kwa kuwathamini zaidi, kwa kuwapatia tabasamu “la kukata na shoka” pamoja na kusikiliza kwa makini badala ya “kuwageuzia watu kisogo”. Kwa kufunga na kusali, waamini wanakirimiwa matumaini yanayowashwa na moto wa ndani unaoangaza changamoto na chaguzi wanazokutana nazo katika maisha. Kumbe, sala ni muhimu sana ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, katika undani wa maisha ya mwamini. Kwaresima ni kipindi cha matumaini yanayofumbatwa katika upya wa maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Katika sehemu ya tatu anakazia upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anakazia upendo unaofurahia kuona mafanikio ya wengine. Huu ndio upendo wa kijamii unaopania kujenga ulimwengu mpya unaokita mizizi yake katika mfumo wa maendeleo fungamani ya binadamu. Upendo ni zawadi inayotoa maana katika maisha ya waamini, kwa kugusa na mahitaji msingi ya jirani, ndugu na jamaa. Matendo ya huruma ni kielelezo msingi cha upendo unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine. Mang’amuzi ya Kipindi cha Kwaresima yasimikwe katika upendo, kwa kuwahudumia wagonjwa na wale wote wanaoteseka, waliosahaulika na wenye taharuki kuhusu janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Upendo wa waamini uwasaidie watu wote hawa kutambua kuwa wao ni watoto wa Mungu na kwamba, anawapenda upeo!  

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Ujumbe wa Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo” kwa kuwakumbusha waamini kwamba, Kwaresima ni hija ya toba na wongofu wa ndani. Ni kipindi cha sala pamoja na kugawana mapaji mbalimbali ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake. Huu ni msaada mkubwa kwa mtu binafsi na jumuiya za waamini katika ujumla wake. Hii ni sehemu ya mchakato unaopania kupyaisha imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliye hai, matumaini kutoka kwa Roho Mtakatifu na mapendo yanayotoka katika Moyo wenye huruma wa Mungu Baba.

Papa Kwaresima 2021

 

16 February 2021, 15:50