Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni & Jubilei ya Miaka 25 tangu Kuanzishwa kwa Siku ya Watawa Duniani na Mtakatifu Yohane Paulo II: Watawa: Uvumilivu, Matumaini na Furaha katika huduma! Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni & Jubilei ya Miaka 25 tangu Kuanzishwa kwa Siku ya Watawa Duniani na Mtakatifu Yohane Paulo II: Watawa: Uvumilivu, Matumaini na Furaha katika huduma! 

Sikukuu Ya Kutolewa Bwana Hekaluni: Uvumilivu Na Matumaini

Uvumilivu wa Mzee Simeoni unaakisi uvumilivu, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa watawa kuangalia uvumilivu wao katika maisha ya mtu binafsi, maisha ya kijumuiya na ulimwengu katika ujumla wake. Watawa wanapotafakari uvumilivu wa Mungu, wajifunze kuwa na imani na matumaini kama alivyokuwa Mzee Simeoni na Nabii Ana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya kutolewa Bwana Hekaluni inaadhimishwa baada ya siku 40 tangu alipozaliwa Mtoto Yesu. Kadiri ya sheria ya Musa, Kristo Yesu anatolewa Hekaluni. Hili tukio muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho kwani hapa Mwenyezi Mungu anakwenda kukutana na watoto wake, sehemu ya utimilifu wa ahadi ya ukombozi, kwa ujio wa Kristo wa Bwana. Sikukuu hii kwa mwaka 2021 imenogeshwa kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoanzisha Siku ya Watawa Duniani. Baba Mtakatifu Francisko Jumanne jioni tarehe 2 Februari 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu sanjari na Jubilei ya Miaka 25 ya Siku ya Watawa Duniani katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19), Ibada hii imehudhuriwa na watawa wachache sana, ikilinganishwa na miaka mingine.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amejielekeza zaidi kufafanua uvumilivu wa Mzee Simeoni: mtu mwenye haki, mcha Mungu na aliyetarajia faraja ya Israeli. Uvumilivu wa Mzee Simeoni unaakisi uvumilivu, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa watawa kuangalia uvumilivu wao katika maisha ya mtu binafsi, maisha ya kijumuiya na ulimwengu katika ujumla wake. Watawa wanapotafakari uvumilivu wa Mungu, wajifunze kuwa na imani na matumaini kama alivyokuwa Mzee Simeoni na Nabii Ana ili kweli macho yao yaweze kuuona wokovu uliowekwa tayari machoni pa watu wote. Baba Mtakatifu anasema, Mzee Simeoni alikuwa na uvumilivu, akasubiri kwa muda mrefu, huku akisali, ili kuona Mwenyezi Mungu akitimiza ahadi zake. Kwa kawaida Mungu anatekeleza mpango wake katika hali ya kawaida na waamini katika hali ya unyenyekevu wanatekeleza pia mpango wa Mungu katika maisha yao.

Mzee Simeoni, katika hija ya maisha yake hata uzeeni, bado miali ya moto wa matumaini na uvumilivu iliendelea kuwaka na wala hakukata tamaa. Fadhila ya matumaini katika maisha ya Mzee Simeoni yalinafsishwa katika uvumilivu hadi pale macho yake yalipouona wokovu uliowekwa na Mungu tayari machoni pa watu wote. Uvumilivu na matumaini ya Mzee Simeoni yalikuwa yanabubujika kutoka katika sala na maisha ya watu wake, waliomtambua Mwenyezi Mungu kuwa ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli. Rej. Kut. 34:6. Mwenyezi Mungu aliwaonesha waja wake uvumilivu hata pale walipokengeuka na kutopea katika dhambi, daima alijitahidi kuwapatia nafasi ya kutubu na kumwongokea. Uvumilivu wa Mungu ni kioo cha uvumilivu wa Mzee Simeoni. Uvumilivu wa Mungu ni changamoto ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anavyojitahidi kujibu udhaifu wa binadamu, ili kumwezesha mwanadamu kupata muda wa kutubu na kumwongokea Mungu. Kristo Yesu kwa namna ya pekee kabisa, anashuhudia uvumilivu, upole, wema na huruma ya Mungu, kwa kuwapatia wadhambi fursa ya kutubu na kuongoka.

Hili ndilo lengo kuu la uvumilivu unaonafsishwa katika maisha ya waamini, kwani Mwenyezi Mungu anaendelea kuwavutia subira bila kuchoka hata kidogo. Hata pale wanapoteleza na kuanguka, bado Mwenyezi Mungu anaendelea kuwavutia subira. Uvumilivu wa Mwenyezi Mungu na ule wa Mzee Simeoni unapaswa kumwilishwa katika wito na maisha ya kuwekwa wakfu. Uvumilivu kamwe si alama ya udhaifu, bali ni nguvu ya ndani inayowawezesha watawa kubeba matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoibuliwa katika maisha ya mtu binafsi na yale ya kijumuiya. Uvumilivu unawasaidia watawa kupokeana jinsi walivyo, kwa kutoa kipaumbele cha mazuri ya wengine, kuweza kuonekana hata kama “si mali kitu.” Uvumilivu unawawezesha watawa kusonga mbele hata pale hatari za maisha zinapoonekana kuwaandama na kuwasonga. Baba Mtakatifu Francisko anasema, uvumilivu unapaswa kunafsishwa katika maisha ya mtu binafsi ambaye amepokea changamoto ya wito na kuijibu kwa moyo wa ukarimu, kiasi hata cha kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani.

Katika hija hii ya maisha, kuna faraja na wakati mwingine kuna hali ya kujikatia tamaa. Wakati mwingine, matunda ya kazi na utume wa watawa hayalingani na matokeo yake, ni watawa kupunguza moyo wa sala hali inayowapelekea kuonja “Ukame wa maisha ya kiroho”. Matumaini yanayotoweka kama “ndoto ya mchana” kwa watawa kushindwa kutekeleza ndoto yao. Baba Mtakatifu anatoa wito kwa watawa kujivumilia kwanza na kuendelea kuvuta subira kwa utekelezaji wa mapenzi ya Mungu, kwa sababu Yeye daima ni mwaminifu kwa ahadi zake. Hasira inayowaka ndani ya nyoyo za watawa ni sumu kali sana inayowapekenya kutoka katika undani wao! Jambo la msingi ni kuondokana na hasira moyoni. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uvumilivu una nafsishwa katika maisha ya Kijumuiya. Hasa pale inapokuwa ni katika mchakato wa kushirikiana mpango wa maisha, sera na mikakati ya kitume! Hili si jambo rahisi hata kidogo. Watawa wajifunze kusoma alama za nyakati. Kinzani na mipasuko ya kijamii ni jambo la kawaida katika maisha ya kijumuiya. Jambo la msingi ni kuyamaliza yote haya kwa amani na utulivu; katika upendo na ukweli. Watawa wajitahidi kufanya mang’amuzi ya maisha yao ya kiroho na kiutu. Watawa wataweza kuona ukweli wanapokuwa katika hali ya amani na utulivu.

Watawa wasaidiane na kutegemezana hata katika madhaifu na mapungufu yao. Watambue kwamba, wameitwa ili kuishi katika Jumuiya na kupendana jinsi walivyo! Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Uvumilivu na matumaini ya watawa yajioneshe kwa namna ya pekee katika ulimwengu. Mzee Simeoni na Nabii Ana walikuwa na matumaini, hata kama bado waliendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali za dunia. Bado waliendelea kuvuta subira, huku wakitumainia wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anachelea kusema kwamba, kuna baadhi ya watawa wamebobea katika “taaluma ya kulalamika daima”. Lakini, watambue kwamba, katika tabia kama hii, ulimwengu utashindwa kuwasikiliza! Wanalalama kuhusu hali ngumu ya maisha kutokana na kuyumba kwa uchumi! Wanalalamika kuhusu upungufu wa miito unaopelekea kufungwa kwa baadhi ya Jumuiya zao.

Mwenyezi Mungu anaendelea kutekeleza mapenzi yake katika nyoyo za waamini, hata pale wao wenyewe wanaposhindwa kuonesha uvumilivu. Ni watu wanaotaka matokeo chanya kwa haraka, kitu ambacho si kawaida hata kidogo. Kuna umati mkubwa wa watawa ambao wamepoteza fadhila ya matumaini kwa kukosa uvumilivu! Uvumilivu uwawezeshe watawa kujichunguza wenyewe, kuangalia jumuiya zao na ulimwengu katika ujumla wake, kwa kutumia “miwani ya huruma ya Mungu”. Wajiulize ikiwa kama wamekuwa tayari kupokea uvumilivu wa Roho Mtakatifu katika maisha yao kama mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Je, wamejitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili katika maisha ya udugu wa kibinadamu? Je, wanatekeleza dhamana na utume wao kwa uvumilivu, au wamegeuka kuwa mahakimu na watu wasiothamini tena utume wao?

Zote hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto katika maisha na utume wa kitawa. Kwa hakika wanahitaji ujasiri wenye uvumilivu ili kutembea na hatimaye kugundua njia mpya pamoja na kufuata ushauri wa Roho Mtakatifu, katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu; bila kutaka kujimwambafai au kujitafutia “ujiko”. Watawa wanapotafakari uvumilivu wa Mungu, wajifunze kuwa na imani na matumaini kama alivyokuwa Mzee Simeoni na Nabii Ana ili kweli macho yao yaweze kuuona wokovu uliowekwa tayari machoni pa watu wote.

Papa Watawa
03 February 2021, 15:48