Tafuta

Siku ya Wapendanao Duniani tarehe 14 Februari 2021: Salam na Matashi Mema kutoka kwa Papa Francisko sanjari na kampeni ya uragibishaji dhidi ya nyanyaso, vipigo kwa kuhimiza upendo wa dhati Siku ya Wapendanao Duniani tarehe 14 Februari 2021: Salam na Matashi Mema kutoka kwa Papa Francisko sanjari na kampeni ya uragibishaji dhidi ya nyanyaso, vipigo kwa kuhimiza upendo wa dhati 

Siku ya Wapendanao Duniani: Utu, Heshima na Umuhimu wa Ndoa!

Siku ya wapendanao ni changamoto kwa vijana kuondokana na “uchumba sugu” kwa kujikita katika maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kuthamini utu, heshima na haki zao msingi na kamwe wasiruhusu miili yao kuchezewa kama “mpira wa kona”. WCC., imeamua kuragibisha kampeni ya upendo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, dhidi ya ukatili, nyanyaso na mauaji ya wanawake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linamkumbuka na kumuenzi Mtakatifu Valentino aliyejisadaka bila ya kujiachia kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya, akiwafunda na kuwaelekeza katika maadili na utu wema. Aliwataka vijana kuachana na tabia ya “uchumba sugu” na badala yake akawaelekeza wafunge ndoa takatifu na kuishi maisha adili yanayompendeza Mungu na jirani. Vijana wengi walihamasika kufunga ndoa takatifu, jambo lililomtia kichefuchefu Mfalme Aureliona kuamuru akatwe kichwa kunako mwaka 273, ili kutoa nafasi kwa vijana wengi kujiunga na Jeshi. Mtakatifu Valentino alijitosa kuwatetea vijana kuwa na wenzi wao wa ndoa, ili hata wao waweze kujenga familia, Kanisa dogo la nyumbani! Ni katika muktadha wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 14 Februari 2021 kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kuhusu Siku ya Wapendanao Duniani. Amewatakia wanandoa watarajiwa heri na baraka pamoja na kuwahakikishia wote wanaopendana sala na maombezi yake! Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anakaza kusema, mwanadamu ameumbwa ili kupenda na kupendwa. Katika Ndoa Takatifu, huu ni umoja ambao ni chimbuko la maisha na utimilifu wa maisha!

Mtakatifu Valentine kabla ya kifo chake, binti wa Kamanda mkuu wa Gereza alimokuwa amefungwa alikwenda kumtembelea na kumkuta amelala, akamwachia ujumbe kwa maandishi mekundu uliosema: “Mwenyezi Mungu akusaidie” naye akamjibu “Valentina wangu ninakuombea”. Siku ya wapendanao ni changamoto kwa vijana kuondokana na “uchumba sugu” kwa kujikita katika maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kuthamini utu, heshima na haki zao msingi na kamwe wasiruhusu miili yao kuchezewa kama “mpira wa kona”. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Siku ya Wapendanao Duniani, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., limeamua kuragibisha kampeni ya upendo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, dhidi ya ukatili, nyanyaso na mauaji ya wanawake. Baraza la Makanisa Ulimwengu linasema, umefika wakati wa kuachana na nyanyaso, vipigo na mauaji ya wanawake yanayoendelea kujitokeza katika medani mbalimbali za maisha.

Kumekuwepo na vitendo vya kikatili vikiwemo vipigo, ubakaji, matusi na vingine vingi ambavyo wanakutana navyo wanawake kwenye mahusiano yao ndani ya jamii au katika maisha ya ndoa na hivyo kupelekea maumivu makali kwao na mara nyingine vifo kama inavyoshuhudiwa kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ukatili huu wa kisaikolojia na kimwili, wakati mwingine unatendeka katika maeneo ya kazi, maeneo ya Ibada na katika jamii kwa ujumla. Siku ya wapendanao duniani, ilete furaha na upendo wa kweli, kwani upendo wa kweli unaganga na kuponya na kamwe si sababu ya upanga mkali unaopenya katika moyo wa yule anayependwa na hivyo kusababisha majeraha makali! Hii ni siku ya kuadhimisha upendo, ili kuwakinga wanawake dhidi ya nyanyaso. Ukatili dhidi ya wanawake ni donda ndugu katika ulimwengu mamboleo. Imefikia hata wakati kwa wanawake kutumiwa kama silaha za vita. Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vimeongezeka maradufu wakati huu wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kimsingi upendo unasimikwa katika utu wema, ni kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; unaheshimu na kuwathamini wengine jinsi walivyoumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Sikukuu ya Wapendanao iwakumbushe walimwengu kwamba, upendo una ganga na kuponya na hizi zinapaswa kuwa ni hisia za kweli. Kwa mtu asiyefahamu kupenda, kupendwa kwake kunageuka kuwa ni janga katika maisha. Upendo wa kweli ni amana na utajiri mkubwa katika maisha ya mwanadamu! Inapendekezwa: Kuongeza ufanisi katika kutambua ukatili wa kijinsia unaofanywa na wenza katika maisha ya ndoa na familia. Kutoa taarifa pale unapoona unafanyiwa ukatili mapema iwezekanavyo na kuomba msaada kwa kupaza sauti, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, haki, amani na utulivu kuweza tena kutawala. Elimu itolewe kwa jamii kuhusu Haki Msingi za Binadamu, haki za wanawake na ukatili wa kijinsia. Huu ni mwaliko wa kuachana kabisa na mila potofu na imani zinazoathiri usawa wa kijinsia na kuwafanya wanawake kuonekana dhaifu. Umefika wakati wa kuongeza madawati ya jinsia na kuongeza pia muda wa kuhudumia.

Kuna haja ya kuimarisha vyombo vya haki ili kuweza kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake! Pengine umefika wakati wa kuwa na sheria maalumu kuhusu ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani. Wanawake wanapaswa kuacha tabia ya kuvumilia ukatili wanaofanyiwa na wenza wao. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema, kuna wanaume pia wanaofanyiwa ukatili wa majumbani, lakini wameamua kunyamaza na “kufa na tai shingoni” kwani ni fedheha sana kusimulia kipigo kutoka kwa mwanamke!

Siku ya Wapendanao

 

14 February 2021, 15:04