Baba Mtakatifu Francisko amewataka watawa sehemu mbalimbali za dunia kuachana kabisa na tabia ya kupiga majungu na umbea kwani ni hatari sana kwa maisha ya kijumuiya. Baba Mtakatifu Francisko amewataka watawa sehemu mbalimbali za dunia kuachana kabisa na tabia ya kupiga majungu na umbea kwani ni hatari sana kwa maisha ya kijumuiya. 

Papa Francisko: Watawa Epukeni Majungu na Umbea Ni Hatari Sana!

Baba Mtakatifu Francisko anawashauri watawa kuhakikisha kwamba, wanaondokana na majungu na umbea kwani huu si mtaji bali ni anguko la jumuiya nyingi za kitawa. Majungu ni chanzo cha wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Majungu ni chanzo cha watawa kutumbukia katika vilema na mizizi ya dhambi. Watawa wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili katika huduma kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu katika maadhimisho ya Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoanzisha Siku ya Watawa Duniani, Jumanne, jioni tarehe 2 Februari 2021, amewataka watawa kuwa na uvumilivu katika mapambano dhidi ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19). Gonjwa hili linaendelea kusababisha maafa makubwa katika maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia, jambo la msingi kwa watawa ni kuendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya upendo kwa Mungu na huduma makini kwa jirani. Watawa watambue kwamba, maisha ya jumuiya si lelemama kwani yataka moyo ili kuweza kuyasongesha mbele kwa imani, matumaini na mapendo! Ili kulinda na kudumisha maisha na wito wa kitawa, Baba Mtakatifu anawashauri watawa kuhakikisha kwamba, wanaondokana na majungu, kwani huu si mtaji bali ni anguko la jumuiya nyingi za kitawa.

Majungu ni chanzo cha wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Majungu ni chanzo cha watawa kutumbukia katika vilema na mizizi ya dhambi. Mababa wa Kanisa wanafafanua mizizi ya dhambi kama ifuatavyo: Majivuno, choyo, zinaa na uasherati, wivu, hasira, ulevi na ulafi pamoja na uvivu. Rejea (Thes 3:10; 1 Pet 5:5, Lk 14:11; 1 Kor 5:1-11; Mk 7:22.) Dawa ya majungu ni kung’ata ulimi anasema Baba Mtakatifu Francisko. Ulimi utavimba na mtu anakuwa na kazi ya kushughulikia kinywa chake badala ya kuzunguka na kuanza kupiga majungu! Watawa jitahidini kuachana na majungu kwani yanabomoa maisha ya Jumuiya. Baba Mtakatifu anasema, kuna matatizo, changamoto na fursa nyingi katika maisha ya kijumuiya. Jambo la msingi kwa watawa ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili, kwa kuendeleza ucheshi katika maisha na utume wao.

Huu ni ushauri wa kibinadamu unaokumbatia uvumilivu katika maisha. Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena, amewashukuru na kuwapongeza watawa kwa: ushuhuda na mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbalimbali za dunia. Anawatia shime, kutokukata tamaa wanapokumbana na matatizo na changamoto za maisha; na hata wanapotindikiwa miito ya kitawa. Wasonge mbele kwani Mwenyezi Mungu ni mkuu na mwingi wa huruma na mapendo, daima anawatakia mema katika maisha.

Papa: Majungu
03 February 2021, 15:15