Papa Francisko:Vijana igeni mfano wa Gabrieli ili kupata utimilifu katika Kristo
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko ametuma ujumbe wake kwa Askofu Lorenzo Leuzzi wa Jimbo katoliki la Teramo-Atri, Italia ambao Jumamosi tarehe 27 Februari 2021 wamefungua mwaka wa Jubilei ya miaka 100 tangu kutangazwa mtakatifu kijana Gabrieli wa Mateso. Katika ujumbe huo Papa anaandika: “katika fursa ya ufunguzi wa mwaka wa Jubilei tangu kutangazwa kwa Mtakatifu Gabrieli wa Mateso imepita miaka 100 tangu mtangulizi wangu Benedikto XV alipotangaza Mtakatifu Gabrieli wa Mateso, aliyefariki katika kisiwa cha Gran Sasso mnamo tarehe 27 Februari 1862 akiwa na umri wa miaka 24”. Papa Fracisko anaendelea kusema kuwa “tukio hili lilionesha kuwa ushuhuda wake wa kikristo ulikuwa namna hii maalum na wa kipekee hadi kufikia kuwa mfano wa kuigwa kwa ajili ya Kanisa hasa kwa ajili ya kizazi kipya.”
Papa katika kukumbuka na maana ya maadhimisho hayo anapenda “kuungana kiroho na Jimbo hilo, Mapadre wa shirika la Mateso, Jumuiya ya Kikristo ya Abruzo na Molise na kwa wale wote ambao wanashiriki mpango wa maandalizi ya ufunguzi wa mwaka wa Mtakatifu katika Madhabahu ya Mtakatifu huyo na msimamizi wa vijana. Ni matumaini yake kwamba mpango huo wa maandalizi kwa ajili ya miaka miamoja unaweza kuwa muafaka wa kuwaleta katika ibada kuu wale wote ambao wanamwona Mtakatifu huyo mpendwa kama mfano wa ushuhuda wa Injili na kwa maombezi yake kwa Mungu. Gabrieli alikuwa ni kijana wa wakati wake, aliyejaa maisha na shauku, kwa kuongoza na shauku ya utimilifu ambao ulikuwa ukimsukuma zaidi ya hali halisi ya ulimwengu na mambo yake huku akijificha ndani ya Kristo, Papa anandika. Hata leo, anawaalika vijana kutambua ndani mwao hamu ya maisha na utimilifu, ambao hauwezi kutenganishwa na utafutaji wa Mungu, kutokana na kukutana na Neno lake ambalo linatia nguvu ya uwepo wao, kuanzia katika huduma na kuilekeza kwa ndugu, hasa walio wa dhaifu zaidi, amesisitiza Papa.
Maisha yake mafupi lakini ya kina yaliacha nyayo ambayo inadumu maisha yake yote kwa dhati. Papa Francisko amesema kwa mfano huo uweze kuigwa na kuwa kwa vijana watawa wa Mateso, nguvu ya amani, uthabiti katika matumaini na shauku katika upendo, kwa kuongozwa na safari ya watawa, na waamini walei katika umakini wa upendo kuelekea kwa Mungu na kuelekea jirani. Hasa katika kipindi hiki cha dharura ya kiafya na matokeo ya udhaifu wa kiuchumi na kijamii Papa amesema ni lazima kwamba wafuasi wa Bwana wageuke kuwa mfano zaidi na chombo cha muungano na udugu kwa kuupanua kwa wengine ule upendo wa Kiristo na kuwaangazia kwa matendo ya dhati ya ukaribu, upole na jitihada. Kwa kihitimsha, Papa Francisko ansema, kwa wote ambao wanashiriki katika mipango mbalimbali ya kuhamasisha kuishi sala na upendo katika mwaka huu wa maana ya Jubilei, anawatakia waweze kujigundua kwa Bwana, wakiweza kutambua uso wa kila kaka na dada ambao wanahitaji faraja na matumaini. Kwa hisia hizo wakati akiomba wamwombee naye kwa moyo wote amewapa baraka yake ya kitume.
Rehema kamili kwa wale wanaosherehekea Jubilei ya Mtakatifu Gabrieli
Idara ya Toba ya Kitume imetoa rehema kamili hadi 27 Februari 2022, mara moja kwa siku kwa ajili ya mtu binafsi, au kwa ajili ya kuombea roho za marehemu, kwa mahujaji wanaotembelea madhabahu ya Mtakatifu Gabrieli wa Mateso na kushiriki katika sherehe ya Jubilei au kutumia muda vizuri mbele sanduku la Mtakatifu Gabrieli, na kuhitimisha kwa sala ya Baba yetu na kanuni ya Imani, na kwa maombi yaliyoelekezwa kwa Bikira Maria na kwa Mtakatifu Gabrieli ikiwa ni pamoja na (kuungama, kupokea ekaristi, na maombi kwa wa nia za Papa). Wazee, wagonjwa na wale ambao kwa sababu kubwa hawawezi kutoka nyumbani, wataweza kupokea rehema kamili baada ya kuamua kujitenga na dhambi zote na kwa nia ya kutimiza masharti matatu ya kawaida haraka iwezekanavyo, wakiwa mbele ya picha fulani ya mtakatifu na kuungana kiroho kwa yule anayeadhimisha Jubilei huku wakimtolea Bwana sala na mateso yao.