Tafuta

Mkataba wa Ushirikiano "Rome Call For Artificial Intelligence": Umuhimu wa Kanuni maadili na utu wema katika matumizi ya akili bandia. Iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mkataba wa Ushirikiano "Rome Call For Artificial Intelligence": Umuhimu wa Kanuni maadili na utu wema katika matumizi ya akili bandia. Iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Papa Francisko Mkataba wa Akili Bandia: Kanuni Maadili na Utu!

Tarehe 28 Februari 2021 ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili uliowekwa saini kati ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Kampuni ya Microsoft, Kampuni ya IBM pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO! Maadili na Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya “akili bandia” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolijia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya “akili bandia” kutokana na mchango wake mkubwa! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema kwamba, tarehe 28 Februari 2021 ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili uliowekwa saini kati ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Kampuni ya Microsoft, Kampuni ya IBM pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organzation of the United Nations"; kifupi: FAO).

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, maendeleo ni kwa ajili ya wote! Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha katika kumbukizi la Mwaka mmoja tangu kuadhimishwa kwa tukio hili anasema, Taasisi yake inaendelea kuragibisha Hati hii ili iweze kufahamika na wengi, ili kuwawajibisha wadau katika matumizi bora zaidi ya akili bandia, mintarafu kanuni maadili na utu wema. Ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kwa ajili ya kupata mwelekeo mpya wa ushirikiano katika masuala ya huduma kwa binadamu, bila mtu kutengwa au kubaguliwa. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanahitaji kuongozwa na kuratibiwa na kanuni maadili na utu wema; kwa kuunganisha imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda; usawa na haki ili kujenga na kudumisha misingi ya amani ya kudumu na udugu wa kibinadamu.

Kwa upande wake, Bwana Brad Smith, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Microsoft, anasema, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hayana budi kuwa ni msaada wa maendeleo kwa wengi. Kimsingi maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kujikita katika kanuni maadili, ili kuboresha maisha ya watu na kuzuia athari zake. Bwana Dario Gil, Makamu wa Rais na Mkurugenzi wa Tafiti katika Kampuni ya IBM anakazia kuhusu: Utawala bora, tathmini za protokali, uaminifu, elimu na mafunzo kazini bila kusahau mapinduzi ya sayansi na teknolojia pamoja na kuwasaidia watu kujikita katika kanuni maadili. Naye Qu Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa anasema, Jumuiya ya Kimataifa kufikia mwaka 2050 itaweza kuzalisha chakula cha kutosha watu bilioni 10 ikiwa kama mfumo wa uzalishaji utakuwa ni shirikishi, shupavu na endelevu. Kanuni maadili na utu wema uwe ni msingi katika mchakato mzima wa uzalishaji, lishe bora, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na maisha bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya maisha, tarehe 28 Februari 2020, alikazia kanuni maadili na utu wema katika matumizi ya akili bandia. Hotuba hii ilikuwa ni mchango wa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Ishirini na Sita uliojikita katika matumizi ya “artificial intelligence” yaani “akili bandia” kwa ajili ya huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu katika hotuba yake aliwataka wadau mbali mbali katika ulimwengu wa kidigitali kupembua kwa kina na mapana mchango wa “akili bandia” katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu na hususan katika baiolojia. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano na wadau mbali mbali katika ulimwengu wa kidigitali; Umuhimu wa kulea ili kuwa na dhamiri iliyokomaa pamoja na kuratibu mwingiliano wa mchakato wa maendeleo unaozingatia na kuheshimu kanuni maadili na utu wema!

Baba Mtakatifu anasema, historia ya maendeleo ya mwanadamu imekwisha kupiga hatua kubwa tangu ugunduzi wa mashini pamoja na hifadhi ya habari kwa wakati huu. Haya ni matunda ya mwingiliano wa sayansi katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu kiasi cha kufikia hatua ya kutenganisha au kuunganisha mambo katika uhalisia wake au katika ulimwengu wa kufikirika. Ulimwengu wa kidigitali umemwezesha mwanadamu kupata mang’amuzi mapya kuhusu: nafasi, muda na kuhusu mwili wa mwanadamu. Katika masuala ya kiuchumi na kijamii, watumiaji wa teknolojia hii wamegeuzwa kuwa ni walaji wa kupindukia, kiasi kwamba, mafao ya watu wengi yamo mikononi mwa watu wachache. Ulimwengu wa kidigitali unaendelea kuratibu mahusiano ya watu kwa ajili ya masuala ya kibiashara au kisiasa bila hata ya watumiaji wenyewe kujitambua.

Baba Mtakatifu anakazia zaidi kwamba, kuna haja ya kuwa na utambuzi mpana zaidi ili watu waweze kutumia vyema uhuru wao, badala ya amana na utajiri huu kuhodhiwa na watu wachache ndani ya jamii. Matumizi ya “akili bandia” katika masuala ya Kibaiolojia yamepelekea mabadiliko makubwa katika uelewa na uratibu wa maisha ya viumbe hai na kwa namna ya pekee maisha ya binadamu. Kuna tofauti kubwa ya uzoefu wa maisha kwa njia ya hisia na hali halisi. Kanuni maadili na utu wema ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika maisha ya binadamu. Ili kuweza kukabiliana na changamoto hii kuna haja ya kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi katika nyanja mbali mbali za maisha ya binadamu, ili kuweza kutoa majibu muafaka. Uwepo wa wadau na wakuu mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa katika mkutano huo ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa kusikilizana, ili kuunganisha mang’amuzi na tafakari makini.

Waamini kwa njia ya Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kiimani wanaweza kusaidiwa kutambua njia bora zaidi ya kufuata na kwa kujikita katika uinjilishaji, wakaendelea kutemba kwa pamoja. Kwa njia hii, wataweza kukuza na kudumisha majadiliano na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia pia maendeleo ya maisha yake ya kiroho pamoja na kuishirikisha familia ya binadamu katika ujumla wake! Watu wafundishwe kuwa na matumizi bora na sahihi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa sababu yanaacha athari zake katika dhamiri na tunu msingi za maisha ya binadamu, daima mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Kamwe mwanadamu asigeuzwe kuwa ni kichokoo cha maendeleo ya sayansi. Kuna haja ya kuunda Taasisi za Kimataifa zitakazokazia pamoja na mambo mengine kanuni maadili na utu wema kwa walimu na watumiaji wa sayansi na maendeleo ya teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uwajibikaji huu unajumuisha mchakato mzima wa maendeleo ya teknolojia katika tafiti, mipango, uzalishaji, ugavi na matumizi yake; kwa kuzingatia kanuni maadili katika maendeleo, ili kuweza kuweka uwiano bora kati ya binadamu na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaweza kutoa mchango mkubwa katika azma hii kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; haki na mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni. Yote haya ni kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu bila ubaguzi wala mtu kutengwa! Kanuni maadili na utu wema liwe ni daraja linalowakutanisha wadau katika maendeleo ya teknolojia kwa njia ya majadiliano; kwa kuzingatia uelewa wa ulimwengu na haki msingi za binadamu; haki na wajibu, ili kukabiliana na changamoto changamani kwa siku za usoni. Kanuni maadili na utu wema ni jambo la kupewa msukumo wa pekee kabisa katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, maadili, elimu na sheria ni mambo muhimu sana ya kuzingatiwa katika maendeleo ya teknolojia. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka wadau mbali mbali wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kuendelea kufanya mang’amuzi na majadiliano na wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Papa Akili Bandia
28 February 2021, 15:37