Mikunde ni chakula bora na uwezo mkubwa wa kuimarisha usalama wa chakula ulimwenguni. Mikunde ni chakula bora na uwezo mkubwa wa kuimarisha usalama wa chakula ulimwenguni.  

Papa Francisko:mikunde inaweza kuimarisha usalama wa chakula

Katika ujumbe kwa FAO wakati wa fursa ya maadhimisho ya Siku ya Mikunde Kimataifa iliyofanyika kwa njia ya mtandao mwaka huu,Papa Francisko anakumbusha kuwa mikunde inaweza kuimarisha usalama wa chakula ulimwenguni.Dengu,maharage,mbaazi na njugu ni chakula bora,muhimu kwa lishe bora,vyakula rahisi na vyenye virutubisho ambavyo vinashinda vizuizi vya kijiografia,mali ya kijamii na tamaduni.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mwaliko wa kuwa hodari na katika jamii ya mikunde na kuungana kwa ajili ya kumaliza mara moja na kwa wote njaa, ndiyo ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, kwa lugha ya kispanyola uliosainiwa na Katibu wa Vatican wa  Mahusiano na Mataifa, Askofu Mkuu Paul Gallagher, katika tukio la kuadhimisha Siku ya mikunde  Duniani, tarehe  10 Februari 2021  kupitia mtandaoni iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO. Katika ujumbe huo aliotumwa kwa mkurugenzi Mkuu wa FAO, viongozi wa Mamlaka na wawakilishi wote wa kidiplomasia, Papa anashukuru fursa ya kushiriki tukio hili la kufanya kumbu kumbu ya mwaka wa Kwanza wa Siku hiyo ya Kimataifa ya mikunde. Kuanzishwa kwa siku hii ni kutaka kutoa umuhimu hata nafasi msingi ya wanawake vijijini katika uzalishaji na mgawanyo wa vyakula kwa njia ya mifumo ya mashirika ambayo kiukweli yanapata sababu na nguvu ya upendo kwa ajili ya jirani na katika kazi za pamoja

Papa Francisko anasema mikunde ni chakula bora na uwezo mkubwa wa kuimarisha usalama wa chakula ulimwenguni. Hawana kiburi, wala kutafakari anasa, wakati mikunde hiyo ni sehemu muhimu ya lishe bora. Hivi ni vyakula rahisi na vyenye lishe ambavyo vinashinda vizuizi vya kijiografia, mali ya kijamii na tamaduni. Kwa mfano dengu, maharage, mbaazi na njugu zinaweza kupatikana kwenye meza za familia nyingi, kwa sababu zina uwezo wa kukidhi mahitaji tofauti ya protini katika lishe yetu ya kila siku. Kwa maana hiyo amependa kuwakumbusha kwamba neno kunde linatokana na neno la Kilatino legumen na inahusu matunda au maganda ambayo huvunwa sio kwa kukata, bali kwa kung'oa mimea kwa mikono. Kazi hii kawaida husababisha mikono kuwa mibaya, kwa sababu ya kushika udongo na hali ngumu ya hewa, kwa masaa yasiyofaa, ambayo wafanyakazi wa vijijini, hasa wanawake, wamekuwa wakifanya na bado wanaendelea kufanya.

Kwa bahati mbaya takwimu zinaonesha bado kuna watu wengi, ambao kati yao hatuwezi kusahau watoto, ambao hawawezi kupata rasilimali msingi zaidi na kukosa chakula bora, na cha kutosha. Njaa haiishi kuendelea kusababisha janga lake mbaya, la vifo katika kanda nyingi za dunia, hali ambayo imezidishwa na shida ya kiafya tunayopitia. Katika nyakati hizi, jukumu la kulima ardhi bila kuharibu ni ya haraka, ili tuweze kushiriki matunda yake tukifikiria sio sisi tu, bali pia juu ya vizazi vitakavyokuja baada yetu. Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza kwa maneno halisi, wanawake wa vijijini na wanawake asilia wana mengi ya kutufundisha jinsi ya juhudi na kujitoa kunaturuhusu kujenga, pamoja na kila mmoja na sio hiyo tu bali  shukrani kwa kila mmoja, mitandao ambayo inahakikisha upatikanaji wa chakula, usambazaji sawa wa bidhaa na uwezekano kwamba kila mwanadamu anatimiza matakwa yake.

Kufuata afya inapaswa kuwa haki ya ulimwengu wote. Kwa njia hiyo jukumu la Mataifa ni msingi ili  iwezekane na kuhamasisha sera za elimu kwa umma ambazo zinakuza ujumuishaji wa vyakula vyenye virutubisho kulingana na ukweli wowote, na ambapo kunde lazima ziwe sehemu ya lishe pamoja na vyakula vingine ambavyo hukamilisha. Papa anahimiza kuendelea pamoja na matumaini. “Tuige matendo mema na mazuri ya wale wanawake wa vijijini ambao hawaachii dhamira yao ya kulisha watoto wao wenyewe na watoto wa familia nyingine. Tuthamini kujitoa kwa kuhisi kuwa sehemu ya nyumba yetu ya pamoja ambapo lazima kuwe na nafasi kwa kila mtu, bila kumtupa mtu yeyote. Tulishe kila mtu na kwa njia nzuri, ili kila mtu apate fursa sawa na tunaweza kujenga ulimwengu unaojumuisha na wenye haki.

Mwandishi wa Argentina Jorge Luis Borges aliwahi kusema kuwa “kila mtu lazima afikirie kwamba [...] kila kitu kinachomtokea, hata fedheha, matukio na shida, kila kitu amepewa kama udongo wa mfinyanzi, kama nyenzo ya sanaa; lazima azitumie kwa ajili ya faida yake […] Vitu hivi tumepewa ili tuweze kuvigeuza, vile vilivyo katika hali mbaya kutokana na maisha yetu kuwa vitu vya milele au vinavyotamaniwa kuwa hivyo (kutoka kitabu cha Obras Completas III. 1975-1985. Buenos Aires, Emecé, 1997, uk. 285). Kwa njia hiyo Papa anawaalika kuendeleza sanaa zetu, kuwa hodari na hodari kama mazao ya nafaka, na kuungana pamoja kumaliza njaa mara moja na kwa wote.  

13 February 2021, 16:00