Papa Francisko, Ijumaa tarehe 19 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi na wachezaji wa Timu ya Soka ya Sampdoria kutoka Genova, Kaskazini mwa Italia Papa Francisko, Ijumaa tarehe 19 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi na wachezaji wa Timu ya Soka ya Sampdoria kutoka Genova, Kaskazini mwa Italia 

Papa Francisko: Michezo ni: Maisha, Ukomavu na Utakatifu

Wanamichezo wajitahidi kutekeleza mambo makuu mawili: wote kwa pamoja, kucheza kama timu moja, kwa umoja, ushirikiano na mshikamano. Ushindi mzuri ni ule unaochangiwa na wachezaji wote kwa pamoja. Ubinafsi katika michezo ni hatari sana. Wachezaji wajifunze kushirikiana vyema ili kuondokana na uchoyo, ubinafsi na hata pengine kutaka “kujimwambafai," Hii ni hatari sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatambua na kuthamini kwamba, michezo ni nyenzo muhimu sana katika kusimamia haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Michezo ni muhimu katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu wa kibinadamu pamoja na haki, mambo msingi sana katika kudumisha: umoja na mshikamno wa kidugu. Baba Mtakatifu Francisko katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu pamoja na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo.

Katika kukuza na kudumisha mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 19 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi pamoja na wanachezaji wa Timu ya Soka ya Sampdoria, iliyoanzishwa kunako tarehe 12 Agosti 1946 huko Genova, Kaskazini mwa Italia. Timu ya Soka ya Sampdoria ilikuwa imewasili mjini Roma tayari kwa mpambano wa kutoana jasho la Timu ya Soka la Lazio, Jumamosi, tarehe 20 Februari 2021. Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake, amewakumbusha wanamichezo kwamba, michezo ni maisha, ukomavu na utakatifu. Wanamichezo wajitahidi katika maisha yao kutekeleza mambo makuu mawili: wote kwa pamoja, kucheza kama timu moja, kwa umoja, ushirikiano na mshikamano. Ushindi mzuri ni ule unaochangiwa na wachezaji wote kwa pamoja. Ubinafsi katika michezo ni hatari sana. Wachezaji wajifunze kushirikiana vyema ili kuondokana na uchoyo, ubinafsi na hata pengine kutaka “kujimwambafai” hali ambayo haina mvuto wala mashiko.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, jambo la pili ni kuhakikisha kwamba, wanamichezo wanasaidia kuhamasisha michezo kama sehemu ya maisha na wito wao. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanapenda michezo na soka kwa namna ya pekee. Huu ndio ushauri kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na viongozi pamoja na wanachezaji wa Timu ya Soka ya Sampdoria. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mam Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha!

Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, kimekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Papa Michezo
20 February 2021, 15:20