Mama Kanisa kila mwaka tarehe 8 Februari anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita sanjari na Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari Dhidi ya Biashara ya Utumwa mamboleo Mama Kanisa kila mwaka tarehe 8 Februari anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita sanjari na Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari Dhidi ya Biashara ya Utumwa mamboleo 

Siku ya Kimataifa ya Sala Dhidi ya Biashara ya Binadamu 2021

Siku ya Sala na Tafakari Kimataifa juu ya Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo ilianzishwa mwaka 2015. Hii ni biashara ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kauli mbiu kwa Siku ya Saba ya Sala na Tafakari kwa mwaka 2021 ni “Uchumi bila biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita aliyezaliwa kunako mwaka 1868 huko Sudan Kongwe na kufariki dunia tarehe 8 Februari 1947. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 1 Oktoba, mwaka 2000. Mtakatifu Josephine Bakhita kutoka Sudan, aliokolewa kutoka utumwani, akabahatika kubatizwa, hivyo kuuvua utu wake wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya na hatimaye akawa ni mtawa wa Shirika la Wakanosa. Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Sala na Tafakari Kimataifa juu ya Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo. Hii ni biashara ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kauli mbiu inayonogesha siku ya saba ya sala na tafakari kwa mwaka 2021 ni “Uchumi bila biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.” Huu ni muda muafaka kwa ajili ya kusali na kuwaombea waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Ni muda wa kuwaunga mkono wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaokoa, kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa biashara hii, ili kuwapatia tena matumaini katika mahangaiko yao ya ndani, daima wakijiaminisha katika ulinzi na nguvu ya Mungu inayoponya na kuokoa. Uchumi unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sheria na kanuni za uchumi fungamani zihakikishe kwamba, haki na usawa vinatendeka sawa na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote Baba Mtakatifu Francisko anawakumbuka watu wote wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete ili kukomesha kabisa biashara hii haramu inayoendelea kuchefua utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameendelea kulivalia njuga suala hili na biashara haramu ya binadamu aliwahi kusema kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kuwa watu hawa wanapewa haki zao msingi, uhuru na utu wao kama binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa; kwa kuwaonesha ukarimu na kuwapatia hifadhi; ili hatimaye, waweze kurejeshwa tena katika maisha ya kijamii. Watu waoneshe ujasiri wa kuwafichua wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu na vyombo vya ulinzi, sheria na haki vitekeleze dhamana na wajibu wake pasi na makunjanzi. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanatumia umaskini na ujinga wa watu kuwanyanyasa kwa kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu na hatimaye, kuwageuza kuwa ni vyombo vya kutosheleza tamaa zao mbovu pamoja na kutafuta utajiri wa chapuchapu!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganisha nguvu zao ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwa kuwalinda na kuwasaidia kwa dhati waathirika. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo na awajalie matumaini ya kuweza kujipatia tena uhuru wale wote wanaoteseka kutokana na janga hili la aibu katika maisha yao! Hiki ni kilio cha sala ya watu wanaoteseka kutokana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Wakati huo huo, “Talita Kum” ambao ni mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa unaotekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 sehemu mbalimbali za dunia, tarehe 8 Februari 2021 umeandaa Siku ya Sala na Tafakari kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19) linaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato. Waathirika wakuu ni wanawake, wasichana na watoto! Mtandao huu ukipewa ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu; kwa kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo.

Bakhita 2021
06 February 2021, 16:17