Baba Mtakatifu Francisko anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia kuipongeza Serikali ya Colombia kwa kuweka saini mkataba unaotoa kibali cha muda cha hifadhi kwa wakimbizi kutoka Venezuela. Baba Mtakatifu Francisko anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia kuipongeza Serikali ya Colombia kwa kuweka saini mkataba unaotoa kibali cha muda cha hifadhi kwa wakimbizi kutoka Venezuela. 

Mshikamano wa Papa Francisko na Maaskofu wa Colombia: Wakimbizi!

Papa Francisko amejiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Colombia, kuipongeza Serikali ya Columbia kwa kutoa “Kibali cha Muda cha Hifadhi kwa Wakimbizi na Wahamiaji kutoka Venezuela" kama kielelezo cha utekelezaji kwa vitendo “Tamko la Cartagena la Mwaka 1984”. Wakimbizi milioni 1.7 kutoka nchini Venezia watapata hifadhi nchini Colombia! Udugu wa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii inamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu, mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso dhidi ya utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 14 Februari 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alijiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Colombia, kuipongeza Serikali ya Columbia kwa kutoa “Kibali cha Muda cha Hifadhi kwa Wakimbizi na Wahamiaji kutoka Venezuela” “Temporary Protection to Venezuelans, TPS”.

Hili ni tukio la kihistoria lililotiwa saini tarehe 8 Februari 2021 kama kielelezo cha utekelezaji kwa vitendo “Tamko la Cartagena la Mwaka 1984”. Serikali ya Colombia inapania kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji milioni 1.7 kutoka nchini Venezuela ambayo kwa sasa inakabiliwa na majanga makubwa katika maisha na utume wake. Mkataba huu pamoja na mambo mengine utawawezesha wakimbizi na wahamiaji kupata fursa za ajira, huduma ya elimu na afya. Hili ni jibu makini ambalo limesikiliza na hatimaye, kutoa jibu makini kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela. Itifaki hii inazingatia pia sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Hiki ni kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, unaopania kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa Katoliki nchini Colombia litaendelea kujielekeza zaidi katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya Kanisa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaendelea kuwapongeza wale wote wanaojitosa kushirikiana na wengine katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Na kwa namna ya pekee, anapenda kuungana na Maaskofu Katoliki nchini Columbia kuipongeza Serikali ya Colombia ambayo imesaini Kibali cha Muda Cha Hifadhi kwa Wakimbizi na Wahamiaji kutoka nchini Venezuela. Na kwa njia hii wataweza: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya wananchi wa Colombia. Hiki ni kielelezo cha ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu ikikumbukwa kwamba, Colombia ni kati ya nchi maskini duniani. Inakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto nyingi za maisha. Mchakato wa maendeleo fungamani bado unasuasua; nchi inayokabiliwa na umaskini wa kutupwa na kwa zaidi ya miaka 70 imekuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Pamoja na changamoto zote hizi, Colombia imeamua kutoa hifadhi ya muda kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka nchini Venezuela. Kwa hakika, Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Venezuela kutoka katika undani wa maisha yake.

Takwimu zilizotolewa na Bwana Filippo Grandi, Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, zinaonesha kwamba, Colombia inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji takribani milioni 4.6, sawa na asilimia 37% ya wakimbizi na wahamiaji wote wanaoishi Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean. Kumbe, Mkataba huu, utawawezesha wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Colombia. Mkataba huu utawasaidia wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela kupata chanjo dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambalo kwa sasa ni tishio kwa usalama, ustawi na maendeleo ya wengi.

Masuala ya wakimbizi na wahamiaji kimataifa yamekuwa yakiongozwa kisheria duniani ikiwa pamoja na utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi wa mwaka 1951, Itifaki ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 1967, Tamko la Cartagena la Mwaka 1984 pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018”. Huu ni Mkataba unaopania kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Papa Colombia
15 February 2021, 15:44