Tarehe 15 Februari 2015 Wakristo 21 wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox la Alexandria Misri waliuwawa kikatili na wapiganaji wa Dola ya Kiislam. Wakuu wa Makanisa wamewakumbuka mashuhuda hawa wa imani. Tarehe 15 Februari 2015 Wakristo 21 wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox la Alexandria Misri waliuwawa kikatili na wapiganaji wa Dola ya Kiislam. Wakuu wa Makanisa wamewakumbuka mashuhuda hawa wa imani.  

Mashuhuda wa Imani Kanisa la Kikoptik Misri 15 Feb. 2015

Wakristo wa Kanisa la Kikoptik kutoka Misri waliuwawa kikatili na wapiganaji wa Dola ya Kiislam tarehe 14 Februari 2015 kwa vile tu walikuwa ni Wakristo. Wakristo hao walipokea: Ubatizo wa Maji, Roho Mtakatifu na Damu. Ni watakatifu wa Wakristo wote. Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa maisha unaofumbatwa katika uekumene wa damu na hatimaye, uekumene wa utakatifu wa maisha. Haya ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume. Uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu kati yao.

Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Ni katika muktadha huu wa Uekumene wa damu, viongozi mbalimbali wa Makanisa ya Kikristo, wamefanya kumbukumbu ya mauaji ya kikatili yaliyotokea nchini Libya hapo tarehe 15 Februari 2015 kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Wakristo wa Kanisa la Kikoptik kutoka Misri waliuwawa kikatili na wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State, IS”, kwa vile tu walikuwa ni Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video katika kumbukizi hili anasema Wakristo hao walipokea: Ubatizo wa Maji, Roho Mtakatifu na Damu. Ni watakatifu wa Wakristo wote. Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo. Rej. Ufu. 7:14.

Ni watu waaminifu wa Mungu; waliojitosa kwenda kufanya kazi ughaibuni ili kutafuta riziki kwa familia zao, watu wa familia, waliokuwa na utu na heshima yao kama wafanyakazi, “waliochakarika usiku na mchana” kuhakikisha kwamba, wanakula matunda ya jasho lao” lakini wakauwawa kikatili na hivyo kutolea maisha yao kwa Kristo Yesu, wakati wanauwawa kikatili na wapiganaji wa Dola ya Kiislam, waliungama jina takatifu la Kristo Yesu. Hawa ni watu walioyamimina maisha yao kwenye ufukwe wa Libya na hivyo kubarikiwa kwa damu yao. Hawa ni watu wanyoofu wasiokuwa na makuu, wamekuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kiasi hata cha kuyamimina maisha yao, kielelezo cha ushupavu wa imani. Baba Mtakatifu Francisko anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya mashuhuda hawa wa imani.

Anamshukuru Roho Mtakatifu kwa nguvu alizowakirimia katika uhalisia wa maisha yao kiasi hata cha kuweza kumuungana Kristo Yesu kwa kumwaga damu yao. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru waamini wote wa Wakristo wa Kanisa la Kikoptik kutoka Misri waliochangia kwa njia mbalimbali katika malezi na makuzi ya imani na leo hii, wanakumbukwa. Anawashukuru wanawake wote waliowanyonyesha watu hawa ishirini na moja maziwa ya imani ya kudumu ambayo haikuweza kuondolewa kwa mateso na kifo. Baba Mtakatifu ametuma salam maalum kwa Patriaki Tawadros wa Pili wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox la Alexandria, Misri, ambaye katika maisha na utume wake, amekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa katika imani na mapendo, hata wakati wa nyakati tete katika maisha na utume wa Kanisa. Ushuhuda wa wafiadini na waungama imani unawatia shime waamini kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Baba Mtakatifu amemshukuru Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani, aliyehamasisha kumbukizi hii kwa mwaka 2021. Baba Mtakatifu anaungana na watu wote wa Mungu katika unyofu na umakini katika maisha yao, licha ya dhambi na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini bado wanaweza kujitokeza hadharani kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Bwana! Baba Mtakatifu amewashukuru wafiadini hawa ishirini na moja kutoka katika imani na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, kwa ushuhuda wao wenye mvuto na mashiko. Anamshukuru Kristo Yesu kwa kuwa karibu zaidi na waja wake bila hata ya kuwasahau. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa kuwaalika Wakristo kuwakumbuka na kuwaombea, kwa sababu hata wao huko mbinguni wanawaombea.

Mashuhuda wa imani

 

 

 

16 February 2021, 15:16