Tafuta

Kardinali Jorge Mario Bergoglio, yaani Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Februari 2021 amefanya kumbukizi la Miaka 20 tangu alipoteuliwa na kusimikwa kama Kardinali, na mwaka 2013 akawa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Jorge Mario Bergoglio, yaani Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Februari 2021 amefanya kumbukizi la Miaka 20 tangu alipoteuliwa na kusimikwa kama Kardinali, na mwaka 2013 akawa Khalifa wa Mtakatifu Petro. 

Kumbukizi la Miaka 20 Tangu Jorge Mario Bergoglio Awe Kardinali

Papa Francisko ameadhimisha kumbukumbu ya Miaka 20 tangu alipoteuliwa na kusimikwa kuwa Kardinali hapo tarehe 21 Februari 2001. Siku hiyo, Mt. Yohane Paulo II aliwatangaza na kuwasimika Makardinali 44, kati yao alikuwepo pia Kardinali Jorge Bergoglio, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, ambaye hapo tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu yanayobubujika katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa ni yeye ni nani mbele ya watu na mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uamifu, mahala pa kutakaswa na kuonja wema, upendo na huruma ya Mungu. Waisraeli wakiwa jangwani Mungu aliwaonesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza na kuwapatia chakula na maji!

Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha kumbukumbu ya Miaka 20 tangu alipoteuliwa na kusimikwa kuwa Kardinali hapo tarehe 21 Februari 2001, huku akiwa jangwani kwa sala, mafungo na tafakari ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2021. Siku hiyo, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwatangaza na kuwasimika Makardinali 44, kati yao alikuwepo pia Kardinali Jorge Mario Bergoglio, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, nchini Argentina, ambaye hapo tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali hawa wakaanza kuandika kurasa mpya za Kanisa Katoliki katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili ili kujibu maswali msingi katika maisha ya mwanadamu kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza kila kukicha, kumbe, Kanisa halina budi kuendelea kuwa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote. Rej. GS. N. 4.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kukazia mambo makuu yafuatayo: Maskini, Amani, Mazingira na Udugu wa Kibinadamu. Anatamani kuona Kanisa ambalo linaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Franciko wa Assisi. Kati ya madonda makuu yanayoendelea kumtesa Baba Mtakatifu Francisko ni: umaskini wa watu duniani. Mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaoongozwa na kanuni auni usaidie kupambana na umaskini duniani. Katika maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi udugu wa kibinadamu ni uhalisia unaotambua maisha kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni mwendelezo wa tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyouchambua katika Waraka wa Kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Hii ni tafakari inayozama katika utu na heshima ya binadamu kwa kutambua kwamba, Mtakatifu Francisko wa Assisi alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na hasa wagonjwa wa ukoma, ushuhuda angavu wa Injili. Ndugu katika umoja wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kupokelewa, kuheshimiwa, kuthaminiwa, lakini zaidi kupendwa jinsi walivyo katika udhaifu na utofauti wao, kazi ya Roho Mtakatifu. Udugu unapomwilishwa katika uhalisia wa maisha unakuwa ni chachu ya mageuzi ya dhati kabisa, kwa kutambua wote ni watoto wa Baba mmoja, yaani Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo na wala hakuna sababu ya kuangaliana kwa “macho ya kengeza”. Mahusiano na mafungamano ya kimataifa yanaweza pia kuangaliwa kwa njia ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayozingatia haki msingi za binadamu pamoja na diplomasia ya kimataifa. Amani inafungamana na wajenzi wa amani duniani; haki msingi za binadamu zinatekelezwa kwa kuangalia mahitaji msingi ya watu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, mfano bora wa kuigwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yake katika msingi wa utu na udugu wa kibinadamu.

Kardinali Jorge

 

22 February 2021, 13:51