Tafuta

Vatican News
Ilikuwa ni tarehe 22 Februari 1931 Kristo Yesu alipomtokea Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska na kumuagiza jinsi ya kuadhimisha: Ibada ya Huruma ya Mungu: Kisima cha Utakatifu, Neema na Baraka tele! Ilikuwa ni tarehe 22 Februari 1931 Kristo Yesu alipomtokea Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska na kumuagiza jinsi ya kuadhimisha: Ibada ya Huruma ya Mungu: Kisima cha Utakatifu, Neema na Baraka tele! 

Ibada ya Huruma ya Mungu: Kisima cha Utakatifu, Neema na Baraka!

Kazi ya Kristo ya Ukombozi hudhihirika katika Sakramenti Takatifu, na Liturujia ya Dominika ya Pili ya Pasaka inayozungumzia Sakramenti hizo. Ubatizo, Kitubio na Ekaristi Takatifu. Hivi ni visima vya huruma na upendo wa Mungu visivyokauka. Kanisa huviongoza vizazi vyote vya dunia nzima kuelekea katika visima hivi vya: utakatifu, neema, baraka na matumaini. Sr. Faustina Kowalska!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.  

Kwa mara ya kwanza Kristo Yesu alipozungumza kwamba anatamani Sikukuu ya Huruma ya Mungu iadhimishwe katika Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka, ilikuwa ni tarehe 22 Februari 1931 katika Kanisa la Plock, nchini Poland. Na hapo aliagiza picha ya Yesu mwenye Huruma ichorwe. Katika miaka iliyofuata baada ya hapo, alirudia agizo hili zaidi ya mara 14, akieleza nafasi ya Sikukuu hii katika Kalenda ya Kiliturujia, sababu za kuanzishwa kwake, namna ya kuiandaa na kuiadhimisha. Wazo la Huruma ya Mungu ndilo hutawala katika mwaka mzima wa Liturujia ya Kanisa. Sababu ya kuchagua Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka, ambayo ni kilele cha siku nane tangu Mama Kanisa aadhimishe Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wake, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Uhusiano huu pia husisitizwa kwa Novena ya Huruma ya Mungu, ambayo huitangulia Sikukuu; novena hii huanza Ijumaa Kuu, siku ambayo Kristo Yesu aliteseka na kufa Msalabani. Tunasoma katika kitabu cha kumbukumbu cha Sr. Maria Faustina Kowalska kwamba Yesu alisema: ‘Nawajulisha watu kilindi cha Huruma yangu kupitia kwa Neno aliyefanyika mwili’ (88).

Kazi ya Kristo ya Ukombozi hudhihirika katika Sakramenti Takatifu, na Liturujia ya Dominika ya Pili ya Pasaka inayozungumzia Sakramenti hizo. Ubatizo, Kitubio na Ekaristi Takatifu. Hivi ni visima vya huruma na upendo wa Mungu visivyokauka. Kanisa huviongoza vizazi vyote vya dunia nzima kuelekea katika visima hivi vya: utakatifu, neema, baraka na matumaini. Ibada ya Huruma ya Mungu imepata msukumo na kuhamasishwa katika Kanisa Katoliki katika Karne ya 20 kutokana na ufunuo binafsi aliopewa Sr. Maria Faustina Kowalska kwa mara ya kwanza tarehe 22 Februari 1935, yaani miaka 90 iliyopita. Lakini pia ndani ya Kanisa, Ibada ya Huruma ya Mungu ina historia pana yenye kukita mizizi na kuimarika miongoni mwa familia ya Mungu. Mwito kwa Ibada ya Huruma ya Mungu umepata kutolewa na kusisitizwa kwa nyakati tofauti ndani ya Kanisa kupitia kwa Mababa Watakatifu wafuatao: Mtakatifu Yohane XXIII, Mtakatifu Yohane Paulo II na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi hawa wa Kanisa wametoa mchango mkubwa katika kukuza na kueneza Ibada ya Huruma ya Mungu kila mmoja kadiri ya nafasi na nyakati yake.

Lakini kwa namna ya pekee kabisa kwa njia ya Sr. Maria Faustina Kowalska kwake tumepata kuifahamu ibada ya Huruma ya Mungu kwa njia mbalimbali. Kwa njia ya Picha ya Yesu wa Huruma inayomwonesha Yesu akibariki na miale miwili ikitoka katika ubavu wake uliochomwa kwa mkuki na chini imeandikwa Yesu Nakutumainia, ikimwalika mwanadamu kuitumainia daima Huruma kuu ya Mungu katika maisha yake. Njia ya Rosari ya Huruma ya Mungu inayomwalika mwanadamu kutakafakari Mateso makali ya Yesu aliyoyapata kwa ajili ya kumkomboa Mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumwalika kumtolea Baba wa milele kwa ajili ya dunia nzima. Njia ya Saa ya Huruma, yaani kujizamisha katika Huruma ya Mungu saa ya huruma kuu, saa 9 alasiri ambapo Kristo Yesu alidhihirisha upeo wa Huruma yake na kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Njia ya Sherehe ya Huruma ya Mungu inayoadhimishwa Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka ambapo Kristo alitaka picha yake Ibarikiwe kwa ibada na waamini wapokee Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi wapate maondoleo ya dhambi na adhabu zake.

Ni katika maadhimisho ya Miaka 90 tangu Kristo Yesu alipomtokea Sr. Maria Faustina Kowalska, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu Piotr Libera wa Jimbo Katoliki la Plock, amekazia tena umuhimu wa huruma ya Mungu kama chemchemi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wakimbilie na kuambata huruma ya Mungu inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha na wito wao. Waamini wawe na ujasiri wa kurejea tena katika chemchemi ya huruma ya Mungu inayokita mizizi yake katika Sakramenti za Kanisa. Kwa njia hii, waamini wataweza tena kuhisi uwepo wake wa karibu na upendo, kiasi hata cha wao pia kugeuka na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu, wavumilivu, watu wenye uwezo wa kusamehe na kusahau, kupenda na kupendwa! Katika Kisima cha Huruma ya Mungu, mwanadamu ataweza kuonja amani na furaha ya kweli, changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Mtakatifu Yohane XXIII: Katika hotuba yake ya ufunguzi tarehe 11 Oktoba 1962, alitoa mwongozo wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuwa ni ufunguo wa huruma na mtazamo mpya wa maisha ya Kikristo (Aggiornamento”. Kanisa lilikuwa limepania kufundisha kwa ufasaha amana na utajiri wa Mafundisho ya Kikristo sanjari na kujielekeza kwa upole na huruma badala ya kulaani. Mtakatifu Yohane XXIII alifahamika na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuwa ni Baba wa Huruma na Kweli, mambo yanayoambatana na kukamilishana. Mnamo Julai Mosi, 1962, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitoa Waraka wa kichungaji uitwao “Paenitentiam agere” yaani “Msamaha wa dhambi”. Waraka huu ulipembua kwa kina na mapana juu ya zawadi ya huruma ya Mungu na umuhimu wa kila mwamini kutambua hitaji la zawadi hiyo katika maisha yake na hivyo kukimbilia Kiti cha huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho! Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ungeweza kupata mafanikio makubwa na matunda yake kuenea sehemu mbalimbali za dunia ikiwa kama mbegu hii ingeangukia katika nyoyo iliyo andaliwa, iliyo tayari, amini na kweli. Kumbe, bado kuna umuhimu wa watu wa Mungu kuendelea kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kukimbilia na hatimaye, kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II naye ana mchango mkubwa katika Ibada ya Huruma ya Mungu ndani ya Kanisa Katoliki. Kati ya majukumu makubwa aliyokuwa nayo ni kutekeleza kwa ufasaha, weledi na ufanisi Maazimio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ambao yeye mwenyewe alishiriki kama Askofu. Alipitia tena kuona na kuchunguza Shajara ya Mtakatifu Faustina na kunako mwaka 1981 alitamka wazi kwamba, katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alipenda kutoa huruma ya Mungu kuwa ni kati ya vipaumbele vyake. Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo mwaka 1997 alikaza zaidi kusema, ujumbe wa huruma ya Mungu umekuwa daima dira na mwongozo, uzoefu na mang’amuzi na hivyo kuwa ni muundo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alisisitiza sana kwamba; “Hakuna kitu ambacho mtu awaye yote uhitaji zaidi kuliko huruma ya Mungu...” Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji: “Dives in misericordia”: It is "God, who is rich in mercy" yaani: “Mwenyezi Mungu tajiri wa huruma” anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska alizaliwa tarehe 25 Agosti 1905. Mwaka 1925 akajaribu kuanza maisha ya kitawa ndani ya Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa huruma. Tarehe 3 Aprili 1927 akatokewa na muujiza, Mwaka 1931 akaanza utume wake katika tasaufi ya huruma ya Mungu. Mwaka 1993 akaweka nadhiri za daima. Mwaka 1938 akafariki dunia. Mwaka 1993 akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri!  Tarehe 30 Aprili 2000 Mwenye Heri Sr. Maria Faustina Kowalska akatangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika ya Pili ya Pasaka sanjari na Maadhimisho ya Sikukuu ya Huruma ya Mungu itakayokuwa inaadhimishwa kila mwaka Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka. Tarehe 17 Agosti 2002 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alifanya hija ya pili ya kitume katika Kituo cha Hija cha Kraków-Łagiewniki. Ibada ya kutabaruku Kanisa kuu la Huruma ya Mungu na Sala ya majitoleo kamili ya kutakatifuza ulimwengu mzima kwa Huruma ya Mungu. Mwaka 2005 Chapisho la kwanza la Nyaraka za Sr. Faustina zikaanza kutolewa hadharani.

Tarehe 27 Mei 2006 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alisali mbele ya Picha ya Yesu wa Huruma na mbele ya Masalia Matakatifu Sr. Faustina katika Kituo cha Hija cha Kraków-Łagiewniki. Tarehe 30 Julai 2016 Baba Mtakatifu Francisko alifanya ya Kitume nchini Poland sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 26-31 Julai 2016 katika Kituo cha Hija cha Kraków-Łagiewniki na sala yake binafsi mbele ya Picha ya Yesu wa Huruma na mbele ya Masalia ya Mtakatifu Faustina. Mchango wa Papa Francisko: Ujumbe wa huruma ya Mungu umeendelezwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amejiaminisha sana katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Hii ni kutokana na historia ya wito na maisha yake ya Kikuhani. Kauli mbiu yake ya Kiaskofu ni: “Miserando Atque Eligendo” yaani Mwenyezi Mungu katika huruma yake alimwita na leo hii yuko hivi alivyo ni kwa neema na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2020 alisema kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, amejitahidi kuwafunulia watu, huruma na upendo wa Mungu, kama Kristo Yesu alivyomfunulia Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma.

Tangu sasa, Mtakatifu Sr. Maria Faustina Bikira, atakuwa anaadhimishwa katika Kumbukumbu ya Hiyari na Kanisa zima, kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba! Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa katika tamko lililotolewa tarehe 18 Mei 2020 linasema, kuanzia sasa waamini wataweza kuadhimisha Kumbukumbu ya Hiyari kwa Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, Bikira, baada ya jina lake kuingizwa kwenye Kalenda ya Kirumi. Huu ni wakati wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa sababu rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha! Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” anatafakari kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu wote na kwamba, kazi hii inatoa mwangi wake kwenye maisha ya kiroho yanayosimuliwa na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, Bikira, ambaye kwa njia ya zawadi kubwa kutoka mbinguni, alibahatika kukutana na Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu Baba na akawa shuhuda na chombo cha kutangaza na kueneza Ibada ya Huruma ya Mungu. Mtakatifu Faustina alizaliwa Głogowiec, karibu na mji wa Łódź, nchini Poland kunako mwaka 1905 na kufariki dunia huko Cracovia kunako mwaka 1938.

Mtakatifu Faustina alibahatika kuishi katika Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma kwa muda mfupi. Alionesha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wito na zawadi mbali mbali za maisha ya kiroho, akajitahidi kuishi kwa uaminifu mkubwa kwa zawadi zote hizi. Katika Shajara ya moyo wake, Madhabahu ambayo aliyatumia kukutana na Kristo Yesu, mwenyewe anasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomwezesha kwa ajili ya faida ya watu wengi zaidi. Kwa kumsikiliza Kristo Yesu ambaye ni Upendo na Huruma aliweza kutambua kwamba, hakuna dhambi yoyote ya binadamu ambayo ingeweza kushinda huruma ya Kristo inayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu. Na tangu wakati huo, akawa ni muasisi wa Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo leo hii imeenea sehemu mbali mbali za dunia. Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu, wakati wa Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa makini kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa; tafakari ambayo inapaswa sasa kuendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa. Kimsingi hili ndilo lililokuwa lengo kuu la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uliohitimishwa kwa Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 20 Novemba 2016.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Misericordia et misera” “Huruma na haki” uliandikwa kama sehemu ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma na Mungu inayopaswa kuendelezwa katika maisha ya waamini kama kielelezo cha huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka. Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa lakini kwa namna ya pekee kabisa Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba, Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Hapa Mapadre wahubiri wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanaandaa mahubiri yao vyema na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayojikita katika: ukarimu, ushuhuda wa maisha, msukumo wa kichungaji, uwazi na utayari wa kutoa huduma ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Mapadre sasa wanaweza kuwaondolea watu dhambi ya utoaji mimba. Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: Uso wa huruma “Misericordia vultus” na “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” ni nyaraka zinazoweza kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini ukuu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto anasema Baba Mtakatifu ni kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kwa njia hii, Kanisa litaendelea kuwa kweli ni shuhuda wa huruma ya Mungu na utambulisho wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi kwa waamini kurejea katika mambo msingi ya imani, maisha ya kiroho, sala, tafakari na hija.

Ijumaa ya huruma ya Mungu, imekuwa ni siku ya pekee ya kuweza kuonja shida, magumu na changamoto ya watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kielelezo cha Kanisa linalosikiliza kilio cha watu na kuwajibu kwa wakati muafaka! Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” amewathibitisha Wamissionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuwaondolea waamini vikwazo na vizingiti vilivyokuwa vinawazuia kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya wongofu wa ndani, toba, msamaha na upatanisho. Mapadre kwa nguvu ya Sakramenti waliyoipokea sasa wameongezewa madaraka ya kuweza hata kusamehe dhambi ya utoaji mimba ambayo hapo awali ilikuwa imeachwa rasmi kwa Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lengo ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki.

Waraka wa kitume “Misericordia et misera” ni mwaliko wa kumwilisha huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii kwa njia ya umoja na mshikamano wa upendo. Kuanzia sasa, Kanisa linapenda kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini ndiyo maana kila mwaka Jumapili ya XXXIII ya Mwaka wa Kanisa itaadhimishwa Siku ya Maskini Duniani ili kutoa nafasi kwa Kanisa kutafakari kuhusu maskini ambao kimsingi ni amana, hazina na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Lengo kuu ni kujenga misingi ya haki jamii kwani hakuna haki na amani ya kweli, ikiwa kama bado kuna makundi makubwa ya Maskini wanaoteseka kwa njaa, magonjwa, utupu na upweke katika maisha. Huruma ni kielelezo makini cha imani na ushuhuda wa Kikristo. Huu ni mwaliko wa kutafakari dhana ya umaskini duniani kwa kutumia miwani ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga utamaduni wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu, kwa kuwathamini, kuwajali na kuwasaidia kadiri ya uwezo na fursa zilizopo.

Huruma ya Mungu

 

24 February 2021, 15:25