Papa Francisko anatarajia kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 kufanya hija ya kitume nchini Iraq. Hizi ni juhudi za kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kwa njia ya majadiliano na huduma makini. Papa Francisko anatarajia kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 kufanya hija ya kitume nchini Iraq. Hizi ni juhudi za kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kwa njia ya majadiliano na huduma makini. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Majadiliano ya Kidini

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu nchini Iraq itakuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza na Ayatollah Ali Sistani ambaye ni kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq. Wachunguzi wa mambo wanasema, ni fursa ya kumwilisha kwa vitendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kitume nchini Iraq, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija za kitume ni muhimu sana katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nyenzo ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Serikali mbalimbali duniani. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inapenda kuheshimu Mikataba na Itifaki mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii itakuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza mubashara na Ayatollah Ali Sistani ambaye ni kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq. Wachunguzi wa mambo wanasema, ni fursa ya kumwilisha kwa vitendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”.

Malengo ya Waraka wa Kitume, "Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbalimbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Haya ni baadhi ya mambo msingi ambayo Askofu mkuu Lingua, Balozi wa Vatican nchini Croatia, katika mahaojiano maalum na Vatican News ameyagusia kabla ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa faragha tarehe 18 Februari 2021. Amegusia kuhusu hali ya watu wa Mungu nchini Croatia iliyoko Mashariki mwa Bara la Ulaya. Mwenyeheri Kardinali Alojzije Stepinac, alipendwa sana na watu wake na hivyo akawa mfano bora wa kuigwa katika kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Croatia. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, aliwahi kusema kwamba, Kardinali Stepinac ni mtu aliyaelekeza macho yake kwa Kristo Mteseka; akatambua magumu yaliyokuwa mbele yake, lakini akasimama kidete kulinda na kuwatetea Wayahudi na Waorthodox waliokuwa wanadhulumiwa nchini humo na utawala wa Kikomunisti. Alikuwa ni wakili mwema na sauti ya waamini na mapadre wake walioteswa na hatimaye kuuwawa kikatili. Ni kiongozi aliyesimama kidete kutetea na kudumisha ukweli; mwanga unaomwezesha mwanadamu kuishi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mashuhuda wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utakatifu katika Kanisa, unaojionesha kwa namna ya pekee, kwa kuimarishwa na Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Mwenyeheri Kardinali Stepinac alijibu wito huu kwa njia ya maisha yake ya kipadre na kiaskofu, kiasi hata cha kujitoa sadaka, ili kuungana na Yesu Kristo. Kifo chake ni kielelezo cha hali ya juu cha madhulumu ya Kikomunisti dhidi ya Kanisa, kwa kufanya madhulumu kwa viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa. Lakini, Watu wa Mungu nchini Croatia walikuwa tayari kuyamimina maisha yao badala ya kumsaliti Kristo, Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2016, Baba Mtakatifu Francisko aliunda Tume maalum inayowaunganisha wajumbe kutoka Vatican, Kanisa Katoliki la Serbia na Kanisa la Kiorthodox la Serbia ili kupembua kwa kina na mapana masuala ya kihistoria juu ya maisha na utume wa Mwenyeheri Kardinali Alojzije Stepinac, kabla, wakati na baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Tume hii imeundwa baada ya mikutano ya ushauri kutoka Vatican, Kanisa la Kiorthodox la Serbia pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Serbia, ili kupata ufafanuzi wa masuala mbali mbali ya kihistoria kabla ya kuendelea na mchakato wa kumtangaza Kardinali Stepinac kuwa Mtakatifu. Tume hii imepewa dhamana ya kufanya kazi ya kisayansi huku ikizingatia mbinu za kisayansi katika masuala ya kihistoria kwa kuchunguza na kupembua nyaraka mbali mbali zinazopatikana kwa wakati huu kwa kuzingatia mazingira ya wakati ule. Taarifa inakaza kusema, uchunguzi huu wa kisayansi hautaweza kuingilia mchakato wa kumtangaza kardinali Alojzije Stepinac kuwa Mtakatifu, kwani hii ni dhamana maalum ya Vatican na wala haina uhusiano na masuala ya kihistoria. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, Croatia imekumbwa na matetemeko makubwa mawili ya ardhi yaliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Bado wananchi wa Croatia wanateseka sana kutona na madhara ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na athari za kuanguka kwa theluji.

Kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora, lakini kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha. Wananchi hawa wanapaswa kusaidiwa ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Licha ya majanga na maafa haya makubwa, lakini bado watu wa Mungu nchini Croatia wana Ibada kubwa kwa Bikira Maria na upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa katika ujumla wake. Kwa ufupi ni kwamba, Askofu mkuu Lingua alizaliwa tarehe 23 Machi 1960 huko Fossano, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 10 Novemba 1984 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na hatimaye kuwekwa wakfu tarehe 9 Oktoba 2010 na Kardinali Tarcisio Bertone aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican wakati ule. Kimsingi Askofu mkuu Lingua alianza huduma ya kidiplomasia mjini Vatican kunako mwaka 1992.

Tangu wakati huo ametekeleza utume wake sehemu mbali mbali za dunia kama vile: Pwani ya Pembe, Marekani, Serbia na Italia. Amewahi kufanya kazi katika Sekretarieti ya Vatican kwenye idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican na alijikita zaidi kwa masuala yaliyokuwa yanazihusu nchi za Amerika ya Kusini na Caribbeani. Kunako mwaka 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Askofu mkuu Giorgio Lingua kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Croatia. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Lingua alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Cuba. Amewahi pia kuwa Balozi wa Vatican nchini Iraq na Yordan ambako ameshuhudia mateso na mahangaiko ya Wakristo kutokana na nyanyaso na dhuluma za kidini na kiimani, lakini wakati wote amejitahidi kuwa ni rejea ya matumaini kwa wale waliokata tamaa. 

Mahojiano Croatia
19 February 2021, 15:27