Ujumbe wa Baba Mtakatifu Franciko kwa Rais Joe Biden wa Marekani: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu kwa kutafuta na kuambata: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Franciko kwa Rais Joe Biden wa Marekani: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu kwa kutafuta na kuambata: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Rais Joe Biden wa Marekani

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sera, maamuzi na mikakati ya Rais Joe Biden italindwa na kuongozwa na: haki ya kweli, uhuru; kwa kuheshimu na kuthamini utu na haki msingi za binadamu; maskini, watu wasiokuwa na sauti na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wakipewa kipaumbele cha kwanza. Umoja na upatanisho wa kitaifa ni muhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Joseph Robinette Biden Jr., ambaye anajulikana na wengi kama Rais Joe Biden mwenye umri wa miaka 78, baada ya kula kiapo, tarehe 20 Januari 2021 amesimikwa na kuwa ni Rais wa 46 nchini Marekani na anakuwa ni mwamini wa pili kutoka Kanisa Katoliki kuwa Rais wa Marekani. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumtakia heri na baraka anapoanza kuwatumikia watu wa Mungu nchini Marekani na kwamba, anapenda kumhakikishia sala zake katika maisha na utume wake kama Rais wa Marekani. Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa watu wa Mungu nchini Marekani kuendelea kujikita katika masuala ya kisiasa, kwa kuzingatia kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho ambazo zimeipamba nchi yao tangu kuanzishwa kwake. Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kuna haja kwa Marekani kujiunga na familia kubwa ya binadamu ili kushirikiana na kushikamana na nchi nyingine ili kutoa majibu muafaka kwa changamoto hii.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sera, maamuzi na mikakati yake italindwa na kuongozwa na: haki ya kweli, uhuru; kwa kuheshimu na kuthamini utu na haki msingi za binadamu; maskini, watu wasiokuwa na sauti pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wakipewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu anamwombea kwa Mwenyezi Mungu, aliye chemchemi ya: busara, hekima na ukweli, kuongoza juhudi zake zitakazosaidia mchakato wa maridhiano, upatanisho na amani ndani na nje ya Marekani, ili hatimaye, kutafuta na kuambata ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amehitimisha ujumbe wake kwa Rais Joe Biden akimtakia heri na baraka kwa ajili ya familia na watu wa Mungu nchini Amerika katika ujumla wao.

Kwa upande wake, Rais Joe Biden katika hotuba yake ya kwanza kama Rais wa Marekani amegusia kuhusu ushindi wa demokrasia nchini Marekani; umuhimu wa kuganga na kuponya madonda ya utengano nchini Marekani, kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa Umoja wa Kitaifa. Marekani inaandika ukurasa mpya wa demokrasia kwa kujikita katika Katiba ya nchi na utawala wa sheria, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bado kuna haja ya kuganga na kuponya madonda ya utengano nchini Marekani, ili kulinda na kudumisha haki jamii. Kumekuwepo na watu wenye itikadi kali za kisiasa, mifumo mbalimbali ya ubaguzi pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyoendeshwa ndani ya nchi. Marekani inahitaji kuendelea kujikita katika demokrasia na umoja wa Kitaifa.

Na kwa njia hii, Marekani itaweza kujizatiti na kupambana fika na chuki na uhasama, misimamo mikali, magonjwa, ukosefu wa fursa za kazi, ukosefu wa utawala wa sheria pamoja na kuwasaidia wale wote waliokata tamaa ya maisha. Umoja wa Kitaifa ujenge na kudumisha haki jamii na usawa ili kuondokana na mifumo yote ya ubaguzi wa rangi, kwa kuheshimu haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Haya ni mapambano endelevu katika maisha ya watu wa Mungu nchini Marekani. Ni wakati wa kumwilisha imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda. Umoja ukoleze mchako wa kuheshimiana ili kudumisha amani na kukataa kinzani, migogoro na vita. Rais Joe Biden anasema ni Rais wa Wamarekani wote bila ubaguzi, kumbe wanapaswa kupendana. Mambo msingi yanayowatambulisha Wamarekani: Fursa mbalimbali, uhuru, utu, heshima na ukweli. Leo wananchi wengi wa Marekani wanahofu kuhusu hatima za familia na kazi zao. Unyenyekevu, maridhiano sanjari na ulinzi wa Injili ya uhai ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya Marekani kwa sasa na kwa siku za usoni, ikiwa kama wananchi wote wataendelea kushikamana katika umoja. Rais Joe Biden amesema kwamba, Marekani imepepetwa sana katika miaka ya hivi karibuni, lakini imesimama tena ili kuendelea kujizatiti kama mdau wa amani, maendeleo na usalama.

Marekani imewakumbuka na kuwaombea wagonjwa wa Corona, COVID-19 waliofariki dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wagonjwa 400, 000 waliofariki dunia. Gonjwa hili limesababisha ukosefu wa usawa. Ni wakati wa kupambana na changamoto hizi ili kuboresha ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake kwa kutekeleza majukumu yake barabara. Rais Joe Biden amesema atajizatiti kulinda: Katiba ya nchi, demokrasia, Wamarekani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Anataka kujielekeza zaidi katika ujenzi wa fadhila ya upendo, ili kuganga na kuponya; tayari kuendeleza demokrasia, matumaini, ukweli na haki.   Rais Joe Biden mwanzoni kabisa wa madaraka yake kama Rais tayari amekwisha saini mambo kumi na tano yanayopaswa kutekelezwa kwa haraka sana. Haya ni pamoja na mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuwataka wananchi wote wa Marekani wanaofanya kazi na kutembelea ofisi za Serikali kuu kuhakikisha kwamba wanavaa barakoa. Marekani imerejea tena katika utekelezaji wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliotiwa mkwaju mjini Paris, nchini Ufaransa ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Marekani imejiunga tena na Shirika la Afya Duniani, WHO. Hali inayoirejesha tena Marekani katika shughuli za Kimataifa, ili kusaidia mchakato wa mabooresho ya afya na usalama zaidi.

Papa: Rais Joe Biden
21 January 2021, 16:05