Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu Katoliki Venezuela kwa kuliwezesha Kanisa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu Katoliki Venezuela kwa kuliwezesha Kanisa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Ujumbe wa Papa Kwa Maaskofu Katoliki Venezuela: Corona

Papa amegusia kuhusu: Utume wa Kanisa unaokita mizizi yake katika Amri ya Upendo na Huduma ya Upendo kwa Jirani. Amewashukuru na kuwapongeza Mapadre waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini humo. Anawatia moyo kwa ushuhuda wa upendo na mshikamano wa kidugu na nia yao njema ya kuendelea kutekeleza utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anatumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa linawahimiza watu wa Mungu kufuata taratibu na kanuni zinazotolewa na madaktari pamoja na wahudumu katika sekta ya afya kama njia ya kupambana na gonjwa hili ambalo linaendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbalimbali za dunia!

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela ambayo imeguswa na kutikiswa sana na umaskini pamoja na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 kati ya tarehe 19 na tarehe 20 Januari 2021 linafanya mkutano kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Mapadri wetu katika mapambano dhidi ya janga la gonjwa la COVID-19: Uzoefu na huduma yao ya Kikuhani katika kipindi hiki”. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia Jumatatu, tarehe 18 Januari 2021 mchana, kuna zaidi ya wagonjwa 120, 000 walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19, kati yao wagonjwa 113, 000 wamepona na waliofariki dunia ni 1, 106 ingawa wachunguzi wa masuala ya afya wanasema, pengine takwimu hizi haziakisi ukweli wa mambo nchini Venezuela.

Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linasema, lengo kuu la mkutano huu lilikuwa ni kuhamasisha majadiliano ya kidugu, kwa kutoa nafasi kwa Mapadre ili Kanisa liweze kusikiliza uzoefu na mang’amuzi yao katika kipindi hiki cha dharura dhidi ya gonjwa hatari la Corona, COVID-19. Hii imekuwa ni fursa kwa Maaskofu kuweza kusikiliza na hatimaye, kupokea ushauri uliotolewa na Mapadre ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia waathirika wa gonjwa la Corona, COVID-19. Ushauri na mapendekezo yanayotolewa yamepokelewa kwa moyo wa shukrani na Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela limesema, litayafanyia kazi kama sehemu ya mkakati na sera na shughuli za kichungaji katika sekta ya afya nchini Venezuela.

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe kwa njia ya video washiriki wa mkutano huu kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki na Mapadre nchini Venezuela. Amegusia kuhusu utume wa Kanisa unaokita mizizi yake katika Amri ya Upendo na Huduma ya Upendo kwa Jirani, mambo ambayo yanategemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Mapadre waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Anawatia moyo kwa ushuhuda wa upendo na mshikamano wa kidugu pamoja na nia yao njema ya kuendelea kutekeleza utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu hata katika kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu. Huu ni utume ambao Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake. Mwinjili Marko katika Maandiko Matakatifu anasimulia jinsi ambavyo Mitume walivyorudi kutoka katika shughuli zao za kichungaji, wakampatia Yesu habari za mambo yote waliyoyafanya na yale yote waliyofundisha. Yesu akawachukua na kuwapeleka faragha, ili wapate kupumzika kidogo. Rej. Mk. 6: 30-31.

Hivi ndivyo Kanisa linavyopaswa kutenda hata katika kipindi hiki kigumu chenye changamoto nyingi. Kanisa linapaswa kuonesha umoja na mshikamano wa dhati na watu wa Mungu katika ukweli na uwazi, daima wajitahidi kurejea tena kwa Kristo Yesu ili kujichotea nguvu za kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Ni muda wa kudumisha udugu wa Kisakramenti ili kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya yale mambo waliyotenda na kufundisha kwa kutambua kwamba, hii ni kazi ya Mwenyezi Mungu na wao kama Mapadre ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anasema, mkutano huu umefanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kutokana na madhara makubwa ambayo yamesababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Mapadre ni watu waliopokea utume wa kushuhudia na kuendeleza huruma na upendo wa kibaba kwa ajili ya watu waaminifu wa Mungu. Ikiwa kama Wakleri watakuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, Kanisa litaweza kukua na kuongezeka kwa kuzingatia mambo makuu mawili: Amri ya Upendo na Huduma ya Upendo kwa Jirani, mambo yanayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, wakati wa Karamu ya Mwisho, Siku ile iliyotangulia mateso na kifo chake Msalabani alipowaosha Mitume wake miguu! Katika historia, hili ni tendo ambalo lilifanywa na watumwa! Lakini, Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu, alijinyenyekesha ili kuonesha mfano na kuwataka wafuasi wake wawe ni mashuhuda na vyombo vya huduma ya upendo kati yao! Wadumishe udugu katika huduma bila kutafuta masilahi ya mtu binafsi na kwamba udugu wa kweli unafumbatwa katika huduma ya upendo. Kumbe, upendo na huduma ni sawa na chanda na pete ni mambo yanayosindikizana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Fracisko anakaza kusema, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake wawe ni “mabingwa katika mchakato wa kumwilisha Injili ya upendo kwa jirani zao”, wawe na uwezo wa kushuhudia upendo huu katika hali na matendo ya kawaida yanayotekelezwa kila kukicha. Wawaoneshe watu wa Mungu huruma na upendo; kwa kuwajali sanjari na kuwashirikisha faraja ya Mungu. Wawe ni watumishi hodari na wanyenyekevu, kwa kutambua kwamba, wameitwa na kutumwa na Kristo Yesu. “Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk. 20:26-28. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre kumjifunza Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni watumishi wanyenyekevu na waaminifu kwa watu wote wa Mungu, lakini zaidi kwa maskini na wahitaji zaidi. Kwa bahati mbaya hawa ndio wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kumbe, katika kipindi hiki cha janga kubwa la Virusi vya Corona, COVID-19, watu hawa wa Mungu wanapaswa kujisikia kwamba: wanathaminiwa, wanasindikizwa, wanahudumiwa na kupendwa. Baba Mtakatifu anawaalika Wakleri nchini Venezuela kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakitekeleza utume wa shughuli zao za kichungaji kwa furaha na umakini mkubwa. Waendelee kupyaisha sadaka ya maisha yao kwa Kristo na kwa ajili ya watakatifu wa Mungu. Anawashukuru kwa upendo na huduma makini wanayoendelea kuitoa kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Venezuela. Kipaumbele cha kwanza kimekuwa ni wagonjwa waliojitahidi kuwapelekea nguvu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu. Wamewasindikiza madaktari na wahudumu katika sekta ya afya, bila kuwasahau watu wa kujitolea wanaowasaidia waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Waendelee kuwa na jicho la pekee sana kwa kuwasaidia watu wasiokuwa na mahitaji msingi, ili waweze kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Papa Venezuela

 

 

 

 

 

 

19 January 2021, 15:26