Mkutano wa Papa na Maaskofu wa Ufilipino wakati wa hija yao jijini Roma 06. 07. 2019. Mkutano wa Papa na Maaskofu wa Ufilipino wakati wa hija yao jijini Roma 06. 07. 2019. 

Ufilipino:Papa ashauri Kanisa la Ufilipino kurudi katika upendo wa kiinjili!

Katika ujumbe wa Papa Francisko aliotuma kwa Baraza la maakofu nchini Ufilipino(Cbcp) anawahimiza kuendeleza juhudi za kushuhudia kwa dhati upendo wa kiinjili hasa wakati huu katikati ya janga la virusi vya corona.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican.

Janga linaloendelea la virusi vya corona au Covid -19 kwa hakika haliruhusu kufanya mkutano wa uwepo wa pamoja kama ilivyokuwa zamani katika mkutano mingi ya kitaifa na kimataifa na kwa maana hiyo mingi inafanyika kwa njia ya mtandao. Na hiyo ndiyo pia imewatokea  Baraza la Maaskofu wa Ufilipino ambao wamefungua mkutano wa 121 wa mwaka, tarehe 26 Januari 2021. Katika fursa ya ufunguzi huo Papa Francisko amewatumia ujumbe wake akiwahimiza waendeleze jitihada za kweli za kushuhudia hata katikati ya janga la virusi vya corona.  Ujumbe wake umesomwa na Balozi wa kitume nchini humo, Askofu Mkuu Charles Brown.

Katika ujumbe wake, Papa anaonesha matumaini na matarajio yatakayo kuwapo katika mkutano huo na kwamba kinahitajika kielelezo cha ubunifu zaidi wa kichungaji, kwa namna ya kwamba Kanisa katoliki nchini Ufilipino liweze kujulikana kama nyumba yenye milango wazi, ambayo inatoa matumaini na nguvu kwa wanaoteseka na kwa wote ambao wanatafuta maisha ya kibinadamu zaidi na  hadhi.  Papa anawabariki kwa baraka wajumbe wote wa Baraza la Maaskofu na kuelezea msaada wake katika utume wao.

Ratiba ya mkutano wao, ni wa siku mbili yaani tarehe  26 na 27 Januari, kwa njia ya mtandao na ambao unaongozwa na Rais wa Baraza hilo (Cbcp), Askofu Mkuu, Romulo Valles wa jimbo Kuu katoliki la  Davao. Zaidi ya mada ya janga la virusi vya corona, ambavyo nchini humo vimesababaisha zaidi ya maambukizi 515 elfu na zaidi ya vifo elfu kumi, ipo ajenda hata ya tathimini ya jumla ya majanga mengine ya vimbunga, kama vile  Hayan naVamco, vilivyo ikumba  Nchi ya Asia mwaka 2020. Maaskofu watajadili pia kuhusu maadhimisho ya miaka 500 tangu kuingia ukristo nchini Ufilipino.  Mwanzoni walitarajia kuadhimisha mwaka 2021 lakini wakaahirishwa hadi mwezi Aprili 2022 kwa sababu ya dharura ya kiafya.

26 January 2021, 15:20