Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, yamekwenda sanjari na maadhimisho ya Siku ya Utotot Mtakatifu: Kauli mbiu kwa Mwaka 2021: "Tunogeshe Udugu wa Kibinadamu. Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, yamekwenda sanjari na maadhimisho ya Siku ya Utotot Mtakatifu: Kauli mbiu kwa Mwaka 2021: "Tunogeshe Udugu wa Kibinadamu. 

Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Mashuhuda wa Injili ya Upendo

Papa anawapongeza watoto wote na kuwataka waendelee kuwa ni mashuhuda aminifu na wenye furaha wa Kristo, daima wakijitahidi kunogesha udugu wa kibinadamu miongoni mwa watoto wenzao! Amewashukuru wada wanaoendelea kujikita kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa Mataifa, kwa njia ya mshikamano wa udugu wa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana ni siku ambayo Mama Kanisa pia anaadhimisha Sikukuu ya Utoto Mtakatifu, siku ya wamisionari watoto duniani, wanaojisikia kuwa ni ndugu wamoja, watoto wa familia ya Mungu, wanaotanguzana, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili hasa miongoni mwa watoto wadogo! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumatano tarehe 6 Januari 2021 kutoka kwenye Maktaba ya Kitume iliyoko mjini Vatican, amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Shirika la Utoto Mtakatifu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo kwa watoto wenzao wanaoogelea katika shida na magumu ya maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza watoto wote na kuwataka waendelee kuwa ni mashuhuda aminifu na wenye furaha wa Kristo, daima wakijitahidi kunogesha udugu wa kibinadamu miongoni mwa watoto wenzao!

Baba Mtakatifu amewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kujipambanua katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa Mataifa, kwa njia ya mshikamano wa udugu wa upendo! Maadhimisho ya Mwaka 2021 yanaongozwa na kauli mbiu “Tunogeshe udugu wa kibinadamu”, lengo kuu ni kuwajengea watoto wadogo ari na moyo wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia anasema, Sr. Roberta Tremarelli, Katibu mkuu wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu. Hii ni Siku iliyoanzishwa na Papa Pio wa XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka kuwaona waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa makuzi na malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee katika maisha na utume wake. Watoto wanapaswa kujifunza na kujenga: utamaduni wa upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja. Haya ni mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni, ili kujenga na kudumisha umoja na upendo wa udugu wa kibinadamu.

Siku ya wamisionari watoto duniani, ni muda muafaka wa kuendelea kujikita katika sala na tafakari inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama ushuhuda wa imani tendaji. Hawa ni watoto wanaoinjilisha, familia, shule na pamoja na “vijiwe vya michezo ya watoto wadogo”. Kwa mwaka 2021, maadhimisho haya yamefanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii, kwa nchi ambazo zina uwezo kutokana na hofu ya maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vy Corona, COVID-19. Hata hivyo watoto wanaendelea kuhamasishwa ili kuhakikisha kwamba, wanajitahidi hata katika hali na mazingira haya kumwilisha karama ya Shirika la Utoto Mtakatifu katika maisha yao, kama kielelezo cha ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watoto waanze kwanza kuinjilisha familia na jirani zao na katika Jumuiya ndogondogo za Kikristo na hatimaye, kuweza kupanua wigo kwa wahitaji wengine zaidi.

Ukarimu uanzie kwanza nyumbani! Huu ni ushuhuda unaopaswa kupata chimbuko lake kutoka kwa kwa wazazi na walezi, wanaorithisha tunu msingi za maisha ya: imani, utu na tamaduni kwa watoto wao. Kwa upande wa pili, watoto nao wanageuka kuwa ni wamisionari kwa watoto wenye shida na mahangaiko mbalimbali. Sadaka na majitoleo ya watoto wadogo yatakusanywa na kupelekwa kwa watoto wenye shida na mahangaiko mbalimbali duniani, kama kielelezo cha kunogesha udugu wa kibinadamu! Shirika la Utoto Mtakatifu lilianzishwa kunako mwaka 1843 na Askofu Toussaint de Forbin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy. Maadhimisho ya Siku ya Utoto Mtakatifu ni changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimissionari ili, hatimaye, waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka 2021 inasema, “tunogeshe udugu wa kibinadamu”.

Papa: Utoto Mtakatifu
06 January 2021, 15:22