Katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mama Kanisa pia anatumia fursa hii kutangaza Pasaka ya Bwana itakayoadhimishwa tarehe 4 Aprili 2021. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mama Kanisa pia anatumia fursa hii kutangaza Pasaka ya Bwana itakayoadhimishwa tarehe 4 Aprili 2021. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Tangazo la Pasaka ya Bwana 2021

Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, linatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, hasa Juma Kuu na hatimaye Pasaka

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. , - Vatican.

Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 4, Aprili 2021.

Kila Jumapili, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo ameshinda dhambi na mauti. Sherehe ya Pasaka ni chemchemi ya Sikukuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 17 Februari 2021 kwa kupakwa majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani.  Mama Kanisa ataadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 16 Mei 2021 na Pentekoste, Sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini Walei itaadhimishwa hapo tarehe 23 Mei 2021.

Jumapili ya kwanza ya Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa Kristo itaadhimishwa hapo tarehe 28 Novemba 2021. Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Sikukuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Sikukuu za Mitume na Watakatifu mbali mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu. Sifa na utukufu kwa Kristo aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake. Amina.

Tangazo la Pasaka

 

06 January 2021, 15:06