Sherehe ya Tokeo la Bwana: Mwaliko kwa waamini juinua macho yao juu, kufunga safari, ili kumwona na hatimaye, kumwabudu Mtoto Yesu, Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu. Sherehe ya Tokeo la Bwana: Mwaliko kwa waamini juinua macho yao juu, kufunga safari, ili kumwona na hatimaye, kumwabudu Mtoto Yesu, Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Safari ya Kumshujudia Mungu Mwana!

Mchakato wa kumtafuta na hatimaye kumsujudia Mwenyezi Mungu ni hija ya maisha ya kiroho inayochukua muda mrefu hadi kufikia ukomavu wa maisha ya ndani. Hili si jambo rahisi sana, Kristo Yesu, kama Nafsi ya Pili ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ni Mungu kweli na mtu kweli: Muhimu: Kuinua macho juu, kufunga safari na hatimaye kumwona Mtoto Yesu, Mfalme wa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana, kwa lugha ya Kigiriki ἐπιφάνεια, epifaneia, ni Sherehe ya ufunuo wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Ni Sikukuu pia ya Utoto Mtakatifu ambayo kwa mwaka 2021 inaongozwa na kauli mbiu “Tunogeshe udugu wa kibinadamu”. Mwinjili Mathayo anasimulia kwamba, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali: “Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia”. (Mt. 2:11). Mchakato wa kumtafuta na hatimaye kumsujudia Mwenyezi Mungu ni hija ya maisha ya kiroho inayochukua muda mrefu hadi kufikia ukomavu wa maisha ya ndani. Hili si jambo rahisi sana, Kristo Yesu, kama Nafsi ya Pili ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ni Mungu kweli na mtu kweli. Katika ubinadamu wake, alipaswa pia kuabudiwa. Lakini, hapa kuna hatari kubwa ya kukosea lengo, kwani ikiwa kama mwanadamu anashindwa kumwabudu Mwenyezi Mungu ataishia kumwabudu, Shetani, Ibilisi pamoja na kuabudu miungu wengine na matokeo yake ni kutumbukia katika ibada ya kuabudu miungu wa kuchonga.

Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo, anawaalika watoto wake kujizatiti na kutenga muda zaidi kwa ajili ya kumwabudu Mwenyezi Mungu. Sherehe ya Tokeo la Bwana, ni muda muafaka wa kwenda kwenye shule ya Mamajusi, ili kujichotea utajiri na amana inayofumbatwa katika maisha yao. Kama waamini wanaitwa kumwangukia na kumsujudia Mwenyezi Mungu kama mtu binafsi na jumuiya ya waamini katika ujumla wake. Ili kuweza kumwabudu Mwenyezi Mungu kuna haja kwa waamini kujifunza: “kuinua macho juu”, “kufunga safari” na “kuona”. Ni maneno msingi yanayowasaidia waamini kumsujudia Mwenyezi Mungu zaidi. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, Jumatano tarehe 6 Januari 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kufafanua mambo hayo matatu kwa kusema kwamba, Nabii Isaya katika Somo la kwanza anawaalika Waisraeli kuinua macho na kutazama juu.

Hawa ni watu waliokuwa wamerejea punde tu kutoka utumwani, kumbe, ni watu waliokuwa wamekata tamaa kutokana na matatizo na changamoto mbalimbali walizokuwa wamekabiliana nazo utumwani. Nabii Isaya anawaambia akisema “Inua macho yako, utazame pande zote” (Is. 60:4). Huu ni wito wa kuondokana na uchovu na “litania ya malalamiko ambayo haina tena kiitikio”, kuachana na mitazamo hasi ya maisha, kuondokana na ubinafsi; kwa kujitafuta na kujifungia katika wasiwasi, hofu na machungu ya ndani yanayozima fadhila ya matumaini na kwamba, shida na magumu ya maisha, kamwe yasiwe ni kiini cha maisha ya mwanadamu. Ukweli utabakia kama ulivyo, mwamini anapaswa kuwa na mwelekeo mpya wa kuyaangalia matatizo na changamoto anazokabiliana nazo, ili kuendelea kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Watambue kwamba, Mungu mwingi wa huruma na mapendo anayatambua matatizo yao, anawasikiliza kwa umakini mkubwa na kamwe hawezi kugeuza kisogo kwa machozi wanayomlilia.

Mtazamo huu, licha ya magumu na changamoto za maisha, bado unaendelea kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuwa ni chemchemi ya moyo wa shukrani. Kinyume chake, mwamini anaweza kujikuta akiwa mtumwa wa matatizo na changamoto zake za maisha na hivyo kushindwa kumwinulia Mwenyezi Mungu macho yenye matumaini. Hofu na mashaka vinauzonga moyo na kuharibu mwelekeo wa maisha na matokeo yake, ni kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha; kukumbwa na chuki na hasira na hatimaye kutumbukia kwenye ugonjwa wa sonona. Katika muktadha huu, ni vigumu sana kumsujudia Mwenyezi Mungu. Mwamini akianza kuhisi na kugundua hali kama hii, anapaswa kuvunjilia mbali mzuguko huu mara moja na kuachana na hitimisho linalokatisha tamaa, kwani ukweli wa mambo ni mkubwa zaidi kuliko mawazo yao!

Mwenyezi Mungu kwa namna ya pekee kabisa anawaalika waamini kuinua macho yao mbinguni na kumwangalia, kwa kujiamimisha kwake, kwa sababu anawalinda na kuwatunza watoto wake wote. Huu ni mwaliko wa kuiishi neema ya Mungu, kwani Mwenyezi Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa, Je, kweli atashindwa kuwatendea mema waja wake? (Rej. Lk. 12:28). Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwasahau wala kuwaacha watoto wake wanaomkimbilia, wakiomba huruma na upendo wake wa daima kwani: Neno wa Mungu amefanyika mwili naye ataendelea kubaki pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, waamini wanapoinua macho yao mbinguni si kwamba, matatizo yao yote yanatoweka “kama umande wa asubuhi”, bali anawapatia nguvu ya kuweza kupambana na hali zao. Kumbe, kuinua macho mbinguni maana yake ni kumsujudu Mwenyezi Mungu, ambaye ni chemchemi ya furaha mpya. Ikumbukwe kwamba, furaha ya dunia hii, imekita mizizi yake katika vitu, mafanikio na mambo kama hayo.

Kwa mfuasi wa Kristo Yesu, msingi wa furaha ya kweli unabubujika kutoka kwenye uaminifu wa Mungu, anayetekeleza ahadi zake kwa wakati muafaka, tofauti kabisa na hali na mazingira yanayowazunguka. Furaha ya kweli ni chanzo cha ushuhuda wa shukrani unaomsukuma mwamini kumsujudia Mungu na kwamba, imani daima haiwezi kumwacha mwamini “kuogelea” peke yake! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema, kabla ya Mamajusi kwenda kumsujudia Mtoto Yesu, iliwabidi kufunga safari, huku wakikabiliana na changamoto za njiani. Mwinjili Mathayo anasema Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walifika Yerusalemu wakisema, “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia” (Mt. 2: 1-2). Safari ni mchakato unaoleta mabadiliko, wongofu wa ndani na tayari kuanza “kuandika ukurasa mpya wa maisha”. Hii inatokana na ukweli katika safari mtu hujifunza mambo mapya, uwezo na uelewa wake unakuwa ni mpana zaidi kutokana na kuona na kukutana na watu mbalimbali. Utashi wa msafiri unaimarika zaidi kutokana na kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha pamoja na hatari ili kuweza kufikia lengo la safari yake. Mwamini anaweza kumsujudia Mungu baada ya kufunga safari inayomwezesha kufikia ukomavu wa ndani!

Kumsujudu Mwenyezi Mungu ni safari inayofanyika hatua kwa hatua, kutokana na uzoefu, mang’amuzi na umri wa mtu husika. Mtume Paulo anakazia uhakika wa ufufuko mbele ya hofu ya mauti kwa kusema, kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku ili kuweza kumsujudia Mwenyezi Mungu. (Rej. 2Kor. 4:16). Katika hali na mazingira kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa mwamini “kuteleza na kuanguka; matatizo, hali ya kuchanganyikiwa, makosa yaliyopita, yote haya yanaweza kuwa ni fursa ya kujifunza kumsujudia Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Yeye anamlipa mtu kwa kuangalia hamu yake ya maisha na uzima wa milele! Kimsingi, Mungu anaangalia undani wa mtu! Changamoto na magumu ya maisha ni nyenzo msingi katika kutakasa moyo na hivyo kumwezesha mwamini kuwa mnyenyekevu, tayari kujiaminisha mbele ya Mungu katika shida na magumu yanayomsonga!

Waamini kwa kuongozwa na dhamiri nyofu watambue, wakiri na kuungama udhaifu na dhambi zao, ili kukua na hatimaye, kukomaa katika maisha ya kiroho, tayari kukutana na Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, ili kumsujudia.  Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni mwaliko kwa waamini kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaunda na kuwafunda wakati wa safari ya maisha yao ya ndani, lakini jambo la msingi ni kutokukata tamaa, bali kwa njia ya unyenyekevu, waweze hatua kwa hatua kumwendea Kristo Yesu. Ikumbukwe kwamba, maisha ni safari ya kumwendea Mwenyezi Mungu anayewapenda upeo, kwa kumwangalia Kristo Yesu, waamini wataweza kujipatia nguvu ya kuendelea na safari kwa furaha iliyopyaishwa. Baba Mtakatifu anasema Mamajusi walikuwa na furaha kubwa walipomwona Mtoto Yesu, Maria na Yosefu. Wakaanguka na kumsujudia. “Nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu: dhahabu na uvumba na manemane.” (Mt. 2: 11-12). Ibada ya kusujudu ilikuwa imetengwa maalum kwa ajili ya wafalme na watu wenye heshima zao.

Mamajusi walimwabudu Mtoto Yesu kwa kumtambua kwamba, ndiye aliyekuwa ni Mfalme wa Wayahudi. Walimwona Mtoto mchanga na maskini akiwa na Mama yake Bikira Maria. Lakini hata katika unyenyekevu huu, Mamajusi waliweza “kumwona” Mungu aliyejifunua kwa njia ya Mtoto Yesu. Wakamsujudia na kumpatia zawadi kutoka katika undani wa nyoyo zao. Ili kuweza kumsujudia Mwenyezi Mungu kuna haja kwanza kwa waamini “kumwona” kwa macho ya imani. Mfalme Herode alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Hili ni kundi la watu lililomezwa na malimwengu na hivyo kuwa ni mateka wa mambo yanayoonekana machoni pa watu, ili waweze kuvutika zaidi. Kwa bahati mbaya wanaangalia lakini hawaoni kitu! Wakati mwingine wanaona, lakini hawaamini. Hawawezi kuona vyema kwa sababu ni mateka wa mambo ya nje. Kwa upande mwingine, Mamajusi wanashuhudia mambo msingi yanayogusa undani wa mtu, kiasi cha kuthubutu kumsujudia Mwenyezi Mungu. Huu ni wito wa kumsujudia Mungu anayejifunua katika mambo ya kawaida, miongoni mwa watu wanyenyekevu na maskini. Hili ni jicho linaloangalia mambo msingi katika maisha.

Mtume Paulo anawahimiza Wakristo kwa kusema “tusiviangalie vinavyooneka, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu, bali visivyoonekana ni vya milele”. (2Kor. 4:18). Mwishoni mwa mahubiri yake, Sherehe ya Ufunuo wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia neema ya kuwa mashuhuda wake watakaomsujudu kwa njia ya maisha mintarafu upendo, unaowakumbatia watu wote! Ibada ya kuabudu na kumsujudu Mungu ipewe kipaumbele cha pekee kwa sababu Mungu mwenyezi ndiye anayestahili kuabudiwa na kusujudiwa na wote!

Papa Epifania 2021

 

06 January 2021, 16:12