Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga utamaduni wa Sala kwa kutumia Maandiko Matakatifu kama njia ya kuzungumza na kujadiliana na Mwenyezi Mungu katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga utamaduni wa Sala kwa kutumia Maandiko Matakatifu kama njia ya kuzungumza na kujadiliana na Mwenyezi Mungu katika maisha. 

Papa Francisko: Sala Kwa Kutumia Neno la Mungu: Lectio Divina!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa njia ya Sala, Neno la Mungu linamwilishwa tena katika maisha ya waamini. Kwa njia hii, wanakuwa ni “Tabernakulo”, mahali ambapo Neno la Mungu linahitaji kupokewa kwa ukarimu na kuhifadhiwa kwa mapendo, ili hatimaye, liweze kuutembelea ulimwengu. "Lectio Divina": Kusoma, Kuwaza, Kusali na Kutafakari Neno la Mungu! Muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” anasema kwamba, kwa hiyo Biblia, iliyo Maandiko Matakatifu, inasema ya Yesu Kristo na kumtangaza kuwa yeye ndiye aliyepaswa kupitia mateso ili kuingia kwenye utukufu (taz. a. 26). Maandiko yote yanasema habari zake, si tu sehemu fulani za Maandiko. Haiwezekani kuelewa maana ya kifo chake na ufufuko wake mbali na Maandiko Matakatifu. Ndiyo sababu ungamo la imani la kale linasisitiza kwamba Yesu Kristo “alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa” (1Kor 15:3-5). Kwa vile Maandiko Matakatifu yanasema habari za Yesu Kristo, yanatuwezesha kuamini kwamba kifo na ufufuko wake si mambo yanayohusu visasili, bali ni matukio ya kihistoria ambayo yaunda kiini cha imani ya wanafunzi wake. Kuna uhusiano wa pekee baina ya Maandiko Matakatifu na imani ya waamini. Kwa vile imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo (taz. Rum 10:17), mwito muhimu tunaopata ni kwamba sisi waamini tupokee upesi Neno la Bwana, kwa kulisikiliza katika tendo la kiliturujia, katika sala na katika tafakari binafsi. Rej. “Aperuit illis”, namba 7.

Ni katika muktadha huu wa umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa sajari na maisha ya waamini wote katika ujumla wao, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Januari 2021 wakati wa Katekesi yake kutoka kwenye Maktaba binafsi alipembua kuhusu umuhimu wa Sala kwa Kutumia Maandiko Matakatifu. Katekesi hii, imeongozwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Zaburi ya 119 kuhusu sifa za sheria ya Mungu: Heri walio kamili njia zao waendao katika sheria ya Bwana. Nitayatafakari mausia yako, nami nitaziangalia njia zako. Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria zako. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, nami nitazitafakari amri zako. Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia zangu. Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga. Baba Mtakatifu anasema, Biblia Takatifu imeandikwa ili iweze kupokelewa na mwamini anayesali ili hatimaye liweze kuotesha mizizi yake katika moyo wa mtu anaye Sali. Roho Mtakatifu ni “maji hai” ambayo ndani ya moyo unaosali yanabubujikia uzima wa milele. Roho Mtakatifu ndiye anayewafundisha waamini kuyapokea Maji haya katika chemchemi yake: Kristo.

Katika maisha ya Kikristo kuna chemchemi nyingi ambamo Kristo Yesu anawangojea, ili aweze kuwanywesha Roho Mtakatifu. Kamwe waamini wasisome Neno la Mungu kama Kitabu cha hadithi tu! Mababa wa Kanisa wanawahimiza Wakristo wote kujifunza kusoma na kuyatafakari Maandiko Matakatifu. Wanakaza kwa kusema, sala lazima iambatane na somo la Maandiko Matakatifu ili ianzishe majadiliano kati ya Mungu na mwanadamu. Kwani Mungu anasema na watoto wake wanaposali na kuwasikiliza wanaposoma maneno ya Mungu. Kila kifungu cha Neno la Mungu kimeandikwa pia kwa ajili yako karne kadhaa zilizopita. Waamini wanaweza kuonja mang’amuzi haya, hata kama Neno la Mungu limesomwa na kurudiwa rudiwa mara nyingi, lakini siku moja linaweza kuwa ni mwanga angavu katika hali na mazingira ambayo mwamini anajikuta akiwamo! Ili kupata mang’amuzi haya kuna haja kwa mwamini kuwa na Neno la Mungu na kuwepo mahali hapo. Kila kukicha Mwenyezi Mungu anapandikiza mbegu ya Neno lake katika maisha ya waamini wake.

Lakini, haijulikani ikiwa kama Mwenyezi Mungu katika “pilika pilika” za kupanda mbegu hizi kama anavyosimulia Mwinjili Marko atakumbana na hali gani? Je, mbegu zitaangukia kando ya njia? Penye mwamba? Penye miiba au penye udongo ulio mzuri? Rej. Mk. 4:3-9. Kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya “pilika pilika” za Mwenyezi Mungu yanategemea juhudi za mtu binafsi, maisha ya sala, moyo ulio wazi, tayari kuyapokea Maandiko Matakatifu, ili kweli Neno la Mungu liendelee kuwa hai katika maisha ya mwamini! Mwenyezi Mungu anawatembelea waja wake kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Kumbe, ni wajibu wao kumsikiliza kwa makini, vinginevyo watakuwa kama Mtakatifu Augustino aliyekuwa anaogopa mapito ya Mungu katika maisha yake, kwani hakuwa tayari kumsikiliza! Kwa njia ya Sala, Neno la Mungu linamwilishwa tena katika maisha ya waamini. Kwa njia hii, wanakuwa ni “Tabernakulo”, mahali ambapo Neno la Mungu linahitaji kupokewa kwa ukarimu na kuhifadhiwa kwa mapendo, ili hatimaye, liweze kuutembelea ulimwengu.

Kumbe, waamini wanapaswa kuliendea Neno la Mungu kwa moyo mweupe pe, bila ya kuwa na makando kando mengine au kwa mwamini kutaka kulitumia kwa ajili ya mafao yake binafsi. Si jambo sahihi kwa mwamini kutumia Maandiko Matakatifu ili kuhalalisha mtazamo wake wa kifalsafa au kimaadili, bali ni kielelezo cha matumaini ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu. Hii ni kutokana na imani kwamba ukweli uliofunuliwa na Mwenyezi Mungu ambao umo katika Maandiko Matakatifu, umekabidhiwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Kumbe, ni wajibu wa mwamini kulipokea na kulielewa Neno la Mungu ili mkutano huu uweze kukamilika. Haipendezi kuona waamini wakilisoma na kukariri Neno la Mungu kama Kasuku tu! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Maandiko Matakatifu yanazama na kuotesha mizizi yake katika akili na moyo wa mwamini, ili kukutana na Mwenyezi Mungu Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanaposoma Neno la Mungu watambue pia kwamba, Neno la Mungu linawasoma hata wao pia!

Ni neema kwa mwamini kuweza kujitambua katika baadhi ya vifungu vya Maandiko Matakatifu au katika mazingira fulani ya Maandiko Matakatifu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Neno la Mungu limeandikwa kwa ajili ya watu wote. Neno la Mungu ni nguvu ya Roho Mtakatifu linapopokelewa kwa moyo mnyofu, ili kuleta mabadiliko katika maisha ya mwamini. Mapokeo ya Kikristo yamesheheni amana na utajiri mkubwa wa mang’amuzi na tafakari mintarafu Neno la Mungu. Kwa namna ya pekee, hili linajidhihirisha katika “Lectio Divina”. Maana yake halisi ni “Masomo ya kimungu” yaani njia ya kutafakari Neno la Mungu katika hatua nne: Mosi, Kusoma, “Lectio”, Neno la Mungu kwa umakini na utii mkubwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufahamu mambo msingi yanayofumbatwa katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu.Hatua inayofuata ni kuzama katika tafakari kwa msaada wa Neno la Mungu, kiasi kwamba, vile vifungu vya Maandiko Matakatifu vinakuwa ni sehemu ya sala. Hii ndiyo hatua ya Pili yaani: Kuwaza, “Meditatio”. Sehemu ya tatu ni Kusali “Orati”, hatimaye ni Kutafakari “Contemplatio”.

Hapa mawazo na maneno yanamwilishwa katika upendo na hivyo kutoa nafasi kwa mwamini kumwangalia Mwenyezi Mungu katika hali ya ukimya, kama vile “vijana wawili wanapopendana na kushibana kwa dhati kabisa” anasema Baba Mtakatifu Francisko. Vifungu vya Maandiko Matakatifu vinabakia jinsi vilivyo, lakini vinakuwa ni kioo cha kuweza kujiangalia, kujipima na kutafakari. Huu ni mtindo wa sala unaopata chimbuko lake katika maisha ya Wamonaki, lakini kwa sasa umeenea sana na kuwa ni sehemu ya Utume wa Biblia unaotekelezwa kwenye Parokia, sehemu mbalimbali za dunia. Kwa njia ya Sala, Neno la Mungu linapata maskani katika maisha ya waamini na kwa upande wao, waamini nao wanapata nafasi katika Neno la Mungu. Neno la Mungu linawajalia waamini kuwa na mawazo mazuri, linategemeza matendo mema na kuwapatia waamini nguvu, amani na utulivu wa ndani, hata pale ambapo, watu wanateleza na hatimaye, kutumbukia katika kinzani na migogoro ya maisha. Katika giza nene la maisha pamoja na “maporomoko ya matatizo na changamoto” Neno la Mungu linakuwa ni kiini cha imani na mapendo yanayomhifadhi mwamini dhidi ya mashambulizi ya “makombora ya maangamizi” kutoka kwa Shetani, Ibilisi.  Hivi ndivyo Neno la Mungu linavyomwilishwa miongoni mwa waamini wanaolipokea katika Sala.

Katika baadhi ya vifungu vya Maandiko Matakatifu, kuna sehemu zinazomwonesha mwamini akiwa amejifananisha kabisa na Neno la Mungu, kiasi hata kama Biblia zote ulimwenguni zingeweza kuchomwa moto, bado watu wangeweza kusoma Neno la Mungu kutokana na amana, utajiri na ushuhuda wa maisha ya watakatifu wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, maisha ya Wakristo ni sehemu ya mchakato wa utii kwa sababu wanasikiliza Neno la Mungu pamoja na ubunifu kwa sababu kutoka katika undani wa mtu, Roho Mtakatifu anamsukuma kutenda hivyo ili kulisongesha Neno la Mungu mbele zaidi. Kristo Yesu: “Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.” Mt. 13:52. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kuhusu Sala na Maandiko Matakatifu kwa kusema, Neno la Mungu ni amana na utajiri usiokuwa na kikomo. Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake, ili waweze kujichotea utajiri huu kwa njia ya Sala!

Papa: Lectio Divina

 

27 January 2021, 15:52