Tafuta

Baba Mtakatifu katika mahojiano maalum na Kituo cha Televishen cha Mediaset, TG, Canale 5 anazungumzia kuhusu: Ghasia za Marekani, Chanjo ya COVID-19, Imani na Udugu wa Kibinadamu. Baba Mtakatifu katika mahojiano maalum na Kituo cha Televishen cha Mediaset, TG, Canale 5 anazungumzia kuhusu: Ghasia za Marekani, Chanjo ya COVID-19, Imani na Udugu wa Kibinadamu. 

Papa Francisko: Muhimu: Ujirani mwema: Chanjo, Umoja na Udugu!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Kituo cha Televishen cha Mediaset, TG, Canale 5 anazungumzia kuhusu: Ghasia na vurugu zilizojitokeza nchini Marekani, Umuhimu wa chanjo dhidi ya Virusi vya Corona kama wajibu wa kimaadili; Utamaduni wa kifo na madhara yake na hatimaye, imani, zawadi kubwa kutoka kwa Mungu inayotangazwa na kushuhudiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kitendo cha wafuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani anayemaliza muda wake wa uongozi hapo tarehe 20 Januari 2021 cha kuvamia makao makuu ya Bunge la Marekani hapo tarehe 6 Januari 2021, kiliwaacha wapenda demokrasia, amani na utawala wa sheria wakiwa wamepigwa bumbuwazi na kushangazwa sana. Maandamano haya yalichochewa na kauli mbiu “Save America Rally”, ambapo Rais Trump aliwataka wafuasi wake kuunga mkono jitihada za wabunge waliokuwa wanapinga kuidhinishwa kwa Bwana Joe Biden kuwa Rais wa 46 wa Marekani. Rais Trump amekataa kukubali kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika hapo tarehe 3 Novemba 2020 na hivyo kumpatia ushindi Rais mteule Joe Biden na Kamala Harris kuwa Makamu wa Rais wa Marekani. Hata hivyo Rais mteule Joe Biden na Mgombea mwenza Kamala Harris, wameidhinishwa na Baraza la Wawakilishi pamoja na Baraza la Seneti ya Marekani na hivyo wataapishwa na kuanza kushika madaraka rasmi hapo tarehe 20 Januari 2021.

Tukio la wafuasi wa Rais Trump kuvamia makao makuu ya Bunge la Marekani lililaaniwa na viongozi wa kidini na kiserikali kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakisema kwamba, hii ilikuwa ni fedheha kubwa kwa demokrasia na utawala wa sheria na kwamba, shutuma za wizi wa kura zinazotolewa na Rais Trump hazina ushahidi wowote ule na ni hatari kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu nchini Marekani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Jumapili tarehe 10 Januari 2021; wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana na katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Mediaset Italia, “Tg, Canale 5”, amesema anaendelea kusali kwa ajili ya Amerika, ambayo hivi karibuni wananchi walivamia makao makuu ya Bunge la Marekani na hivyo kupelekea watu 5 kupoteza maisha pamoja na uharibifu mkubwa wa mali. Kimsingi, ghasia ni jambo linalosababisha maafa kwa wahusika. Baba Mtakatifu anawasihi watu wa Mungu nchini Marekani kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, huku wakijizatiti kukukuza ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Anawaalika waamini kugundua zawadi ya imani, ili kuitolea ushuhuda katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Mediaset Italia, “Tg, Canale 5”, anawasihi watu wa Mungu nchini Marekani kulitafakari kwa kina tukio hili, ili lisijirudie tena na kwamba, kuna haja ya kujifunza kutoka katika historia. Kutokana na maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, inawezekana kutumia chanzo zote zinazotolewa na wataalam wa sayansi na tiba ya mwanadamu, ikiwa kama zimethibitishwa kuwa ni salama na zenye ufanisi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amesema hadharani kwamba, tayari amejiandikisha kushiriki katika chanjo hii itakapoanza kutolewa mjini Vatican wakati wowote kuanzia sasa. Huu ni uamuzi wa kimaadili na anatumaini kwamba, watu wengi zaidi wataridhia kufanya chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hii inatokana na ukweli kwamba, hatari kubwa hapa ni zawadi ya uhai, kwa mtu husika na kwa jirani zake. Ikiwa kama madaktari na wataalam wa afya ya binadamu wanashauri kwamba chanjo hii ni salama na ina ufanisi katika kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, kwa nini watu wawe na mashaka ya kupatiwa chanjo?

Chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii, watu wanajenga udugu na ujirani mwema kwa njia ya chanjo, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza, ili hatimaye, kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Huu ni utamaduni unaosababisha maafa na utengano! Ujirani mwema ni dhana inayopaswa kufanyiwa kazi ili kujenga umoja na mafungamano ya kijamii, Kitaifa na ndani ya Kanisa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba pamoja na tabia ya kutowajali wala kuwathamini wengine, umeendelea kukuzwa kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Maskini, wazee, wakimbizi na wahamiaji wameendelea kuteseka sana kutokana na ugonjwa wa Corona, COVID-19. Kumekuwepo na ongezeko la utoaji mimba kwa madai ya kuwepo na mimba zisizotarajiwa. Tatizo la utoaji mimba ni sehemu ya maisha adili linalogusa utu, heshima na haki msingi za binadamu na hatimaye, inakuwa ni changamoto ya maisha ya kidini kwa kuongozwa na dhamiri nyofu. Haiwezekani kutumia utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba kuwa ni suluhu ya kumaliza matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu kila kukicha!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano hayo anasema, alishangazwa sana kuona umati wa watu unavamia makao makuu ya Bunge la Marekani kwa sababu, kimsingi Wamarekani ni watu wenye nidhamu ya hali ya juu katika demokrasia. Lakini katika ukweli wa mambo, kuna vitu ambavyo haviendi sawi katika hali na mazingira kama haya. Hapa kuna baadhi ya watu wanaochukua maamuzi dhidi ya jumuiya, ni watu wanaokwenda kinyume cha demokrasia, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ghasia na uvunjaji wa sheria ni mambo yanayopaswa kushutumiwa na wapenda amani duniani. Lakini hakuna mtu awaye yote anayeweza kujinasibu kwamba, hajawahi kufanya ghasia hata siku moja katika maisha yake. Kumbe, hapa Baba Mtakatifu Francisko anawasihi watu wa Mungu nchini Marekani kulitafakari kwa kina tukio hili, ili lisijirudie tena na kwamba, kuna haja ya kujifunza kutoka katika historia. Kulitafakari na hatimaye, kulifahamu fika tukio hili, litawasaidia watu wa Mungu nchini Marekani kuweza kufanya marekebisho.

Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, tarehe 10 Januari 2021, amewashauri viongozi wa Serikali ya Marekani na wananchi wote katika ujumla wao, kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa, kwa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kidemokrasia zinazokita mizizi yake miongoni mwa wananchi wa Marekani. Waendelee kupyaisha utamaduni wa watu kukutana sanjari na utamaduni wa huduma, ili kwa pamoja waweze kujenga na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; na hii iwe ni changamoto kwa walimwengu wote! Imani ni fadhila ya Kimungu ambayo kwayo mwamini anamsadiki Mwenyezi Mungu, kile alichosema, alichowafunulia na yale mambo msingi ambayo Mama Kanisa anasadiki na kufundisha. Ni kwa kwa sababu hii, mwamini hutafuta kujua na kufanya mapenzi ya Mungu. Mwenye haki ataishi kwa imani na imani hai, hutenda kazi kwa upendo. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, anajisikia kana kwamba, “amefungwa” kwani hija za kitume zimesitishwa, lakini hata hivyo bado ana matumaini makubwa ya kutembelea Iraq, Mwenyezi Mungu akipenda!

Baba Mtakatifu anasema, anakitumia kipindi hiki cha karantini kwa kusali na kutafakari zaidi Neno la Mungu pamoja na kuwasiliana na watu sehemu mbalimbali za dunia, ili kuwatia shime, imani na matumaini zaidi. Baba Mtakatifu anasema, kamwe hataweza kusahau tarehe 27 Machi 2020 alipokuwa anasali kwa ajili ya watu wote wa Mungu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican “Statio Oribis”. Hiki kilikuwa ni kielelezo cha upendo wa udugu wa kibinadamu kwa watu wote, umoja na mshikamano katika imani, zawadi kubwa sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga ukaribu zaidi na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mwaka 2021 utakuwa ni mwaka wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili “kufyekelea mbali: ubinafsi na uchoyo, kinzani na mipasuko sehemu mbalimbali za dunia”.

Papa: Umoja na Udugu

 

 

 

 

 

 

11 January 2021, 14:06