Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na machafuko ya hali ya kisiasa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na kuwataka wadau wote kujielekeza katika majadiliano yatakaloleta amani ya kudumu. Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na machafuko ya hali ya kisiasa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na kuwataka wadau wote kujielekeza katika majadiliano yatakaloleta amani ya kudumu. 

Papa Asikitishwa na Machafuko ya Kisiasa Afrika ya Kati: Ataka Amani

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wadau wote wanaohusika na machafuko ya kisiasa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kuweka tofauti zao kando na kuanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthamiana kama ndugu, ili kuepuka chuki, hasira pamoja na mifumo yote ya matumizi ya nguvu! Amani itawale zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2021 alionesha wasi wasi na majonzi makubwa kutokana na matukio mbalimbali yanayoendelea kujitokeza kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, iliyomaliza kufanya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, hapo tarehe 27 Desemba 2020 na mshindi kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Mchakato wa uchaguzi mkuu, umeonesha utashi wa wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wa kutaka kujizatiti zaidi katika njia ya amani. Baba Mtakatifu anawaalika wadau wote wanaohusika na machafuko ya kisiasa nchini humo, kuweka tofauti zao kando na kuanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthamiana kama ndugu, ili kuepuka chuki, hasira pamoja na mifumo yote ya matumizi ya nguvu! Bangassou ni kati ya miji yenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi, ulishambuliwa na kushikiliwa kwa muda wa saa kadhaa na waasi, Jumapili tarehe 3 Januari 2021 baada ya mapambano makali ya silaha.

Kulikuwa na njama za kuanzisha mapigano makali kwenye mji mkuu wa Bangui ili kuvuruga maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge uliopania kuimarisha amani, demokrasia, utulivu, upatanisho wa kitaifa pamoja na kujielekeza zaidi katika maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo! Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2021 zaidi ya wananchi milioni 2.8 kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, sawa na asilimia 57% ya watu milioni 4.9 watahitaji msaada wa kiutu, ulinzi, usalama na uhakika wa chakula. Zaidi ya watu milioni 1. 9 sawa na asilimia 39% wako hatarini kupoteza maisha kutokana na baa la njaa linalowapekenya kwa sasa! Hali hii inagumiswa zaidi na machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza baada ya Tume ya Uchaguzi nchini humo kumtangaza Rais Faustine Archange Touadera kuwa mshindi baada ya kumbwaga mpinzani wake mkuu Rais wa zamani Francois Bozize aliyetwaa madaraka kuanzia mwaka 2003.

Miaka 10 baadae utawala wake uliangushwa na Michel Djotodia, kiongozi wa kundi la Kiislamu la Seleka. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2013 Serikali ya Ufaransa iliingilia kati kijeshi kwa “kuwashikisha adabu” wanamgambo wa Seleka na kumaliza operesheni hiyo baada ya Faustine Archange Touadera kuchaguliwa kuwa rais mnamo mwaka 2016. Rais Touadera anaendelea kuongoza kutokana na kusaidiwa na jeshi kubwa la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Zaidi ya askari 13,000 wa Umoja wa Mataifa “MINUSCA” bado wako nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, Mkataba wa Amani na Upatanisho wa Kitaifa uliotiwa saini kunako mwaka 2019 unapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa na wadau wote ili kuondokana na chuki pamoja na tabia ya kutaka kulipizana kisasi.

Papa: Afrika ya Kati

 

07 January 2021, 15:36