Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Wazazi na walezi wanahimizwa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wao, ili kujenga jamii inayojaliana na kuwajibikiana. Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Wazazi na walezi wanahimizwa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wao, ili kujenga jamii inayojaliana na kuwajibikiana. 

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Wazazi Wekezeni Katika Malezi

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu iwe ni fursa kwa wazazi kukaa na kutafakari kuhusu dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto wao! Pale wanapochelea kwamba, bado hawajafanya vyema, waanze kujizatiti kikamilifu kuanzia sasa! Huu ni wakati muafaka kwa wazazi na walezi kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi kwa watoto wao, ili kuwajenga kimaadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa tarehe 8 Desemba 2020 na utahitimishwa tarehe 8 Desemba 2021. Waraka wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu”: Papa Francisko anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Hivi karibuni, Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Mtakatifu Yosefu na kuelekeza mahubiri yake kuhusu dhamana na wajibu wa wazazi katika malezi na makuzi ya watoto wao.

Wazazi wakumbuke kwamba, watoto ni zawadi bora ya ndoa na wanachangia sana mema ya wazazi wenyewe kama inavyofafanuliwa katika Maandiko Matakatifu, kwani wazazi wanashiriki kwa ujasiri mapendo ya Mungu Muumbaji na Mwokozi ambaye kwa njia ya wazazi hawa anataka kuongeza na kuitajirisha familia yake bika kuchoka. Wazazi watambue kwamba, wao ni walezi wakuu na wa kwanza wa watoto wao. Kumbe, wao ni walinzi na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Patriaki Cyril anakaza kusema, wazazi wawe mstari wa mbele katika kurithisha imani, maadili na utu wema kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Dhamana hii itekelezwe kwa ujasiri mkubwa wakati watoto hawa wangali wadogo na wanapokaribia umri wa kuanza “kuogelea” katika maisha ya ujana. Wazazi wawe mstari wa mbele kuwasikiliza watoto wao, kuwapatia ushauri makini, kuwasindikiza kwa upendo na kuwakaripia pale wanapo potoka na kukengeuka.

Patriaki Cyril anaendelea kusema kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii yanayojidhihirisha kwa namna ya pekee katika: luninga, internet pamoja na mitandao ya kijamii, yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kulea dhamiri za watoto wadogo na vijana. Matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ni hatari sana katika kuunda dhamiri za watoto na vijana. Wazazi wawe karibu sana na watoto wao hasa wale ambao wanatumia muda mrefu zaidi wakiwa nje ya familia kwa sababu ya masomo; wawafahamu vyema marafiki wa watoto wao, ili waweze kuwasaidia kukua katika njia njema inayozingatia kanuni maadili na utu wema! Wazazi wawe mstari wa mbele kuwarithisha watoto wao tunu msingi za Kiinjili, Imani na Mafundisho makuu ya Kanisa.

Wazazi wakumbuke kusali na kuwaombea watoto wao kwa Mwenyezi Mungu ili waweze kuwa ni watu wema; wawafundishe pia kusali kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki, amani, upendo, msamaha na maridhiano. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walichangia kwa kiasi kikubwa malezi na makuzi ya Mtoto Yesu, dhamana na wajibu unaopaswa kuendelezwa na kutekelezwa na wazazi hata katika ulimwengu mamboleo. Mtoto Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli, kumbe alihitaji malezi ya kiutu katika ubinadamu wake. Kumbe, wazazi na walezi wanapaswa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wao wangali wadogo, kwani waswahili husema, “Samaki mkunje angali mbichi, akikauka hakunjiki tena”. Wazazi na walezi wakiwekeza vyema kwa watoto wao hapana shaka kwamba, hata maisha yao huko mbeleni, yatakuwa ni ya heri na baraka tele!

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu iwe ni fursa kwa wazazi kukaa na kutafakari kuhusu dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto wao! Pale wanapochelea kwamba, bado hawajafanya vyema, waanze kujizatiti kikamilifu kuanzia sasa! Mwishoni mwa mahubiri yake, Patriaki Cyril amewaweka wazazi wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, ili awasaidie kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao sanjari na kukoleza furaha ya upendo ndani ya familia. Itakumbukwa kwamba, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, hapo tarehe 19 Machi 2021 ametangaza kwamba, itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: yaani: “Famiglia Amoris Laetitia”. Mwaka huu utahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayokuwa inatimua vumbi mjini Roma tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la kuchagua tema hii ni kutaka kukazia mchakato wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika uhalisia wa kila siku wa mahusiano ndani ya familia.Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia. Tamko hili limetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Maktaba ya Kitume, mjini Vatican wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Jumapili tarehe 27 Desemba 2020. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia kuanzia sasa yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Baba Mtakatifu anapenda kuyaweka maandalizi ya Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; kwani maadhimisho haya yanazishirikisha familia zote duniani. Bikira Maria, azisaidie familia zote ziweze kuvutwa na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kutoka kwenye Familia Takatifu na kwa njia hii, ziweze kuwa ni chachu ya kupyaisha ubinadamu na ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Katika kuta za Nyumba ya Nazareti, Mtoto Yesu aliweza kuonja furaha ya maisha ya utotoni, akiwa amezungukwa na upendo thabiti wa Bikira Maria na ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, mambo yaliyomwezesha kuona huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kugundua umuhimu wa elimu, malezi na makuzi ndani ya familia yanayokita mizizi yake katika upendo, unaojenga mahusiano na mafungamano yanayofungua mwelekeo wa matumaini. Ndani ya familia, watu wanaweza kuonja umoja na mshikamano, ikiwa kama familia hii ni kielelezo cha sala, toba na msamaha; unyenyekevu, huruma na utulivu kama sehemu ya kutafuta, kuambata na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Ni katika hali na mazingira kama haya, familia zinafungua malango ya furaha ya Mungu anayewakirimia wote wanaotambua jinsi ya kuwashirikisha wengine furaha ya kweli!

Kwa njia hii, familia pia inapata nguvu za maisha ya kiroho na hivyo kuweza kujiweka wazi kwa ajili ya wengine, ili kutoa huduma kwa jirani pamoja na kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu mpya ulio bora zaidi, lakini kwa kuhakikisha kwamba, familia zinakita maisha na utume wake katika mwelekeo chanya na katika mchakato wa uinjilishaji mpya, unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Familia iwe ni kitovu cha msamaha wa kweli, kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya udhaifu wa kibinadamu, kutubu, kusamehe na kupatana ni mwanzo wa utakatifu wa maisha. Wanafamilia wajifunze kusema: Naomba, Asante na Samahani; maneno yanayoweza kuisaidia familia kuishi kwa amani na utulivu.

Mtakatifu Yosefu

 

12 January 2021, 14:56