Tafuta

Maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya XXXVIII ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanaendelea vyema licha ya changamoto ya Virusi vya Corona, COVID-19 kupamba moto! Maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya XXXVIII ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanaendelea vyema licha ya changamoto ya Virusi vya Corona, COVID-19 kupamba moto! 

Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni 2023: Changamoto ya COVID-19:

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Viongozi wakuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno, CEP, mintarafu maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya XXVIII ya Vijana Ulimwenguni, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno mwaka 2023. Wamegusia changamoto ya COVID-19 nchini Ureno na athari zake katika maisha na utume wa Kanisa, Ureno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini na mapendo na kwamba, hii ni zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa. Matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake!  Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi. Hili ni Kanisa ambalo linawasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wamekuwa kweli ni wadau wa Heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi na vyombo vya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Vijana watambue kwamba, Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni; ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Hapa ni mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa!  Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana. Hii ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya XXXVIII ya Vijana Ulimwenguni yatakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, mwezi Agosti 2023 yanaongozwa na kauli mbiu: “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Viongozi wakuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno, CEP, mintarafu maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya XXXVIII ya Vijana Ulimwenguni, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno mwaka 2023.

Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Maaskofu wa Ureno, yamefanyika katika hali ya udugu na urafiki, kwa kuangalia changamoto kubwa zinazojitokeza katika maisha ya watu wa Mungu nchini Ureno na sehemu mbalimbali za dunia kutokana na athari za maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 hasa miongoni mwa vijana, watoto na wazee. Baba Mtakatifu amelitaka Kanisa nchini Ureno kuendelea kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, kwa kusoma alama za nyakati na kutafuta majibu muafaka ili kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu kinachotokana na athari kubwa za ugonjwa wa Corona, COVID-19. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu ameonesha umoja na uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Ureno. Amesema, anaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya XXXVIII ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023. Kwa hakika, gonjwa hatari la Corona, COVID-19 linaendelea kusababisha madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linasema, linaungana na Baba Mtakatifu Francisko anayewasihi viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na Kitaifa kujielekeza zaidi katika majadiliano, umoja na mshikamano wa kidugu katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Madaktari, wataalam wa tiba ya afya ya mwanadamu pamoja na watafiti mbalimbali waunganishe nguvu ili waweze kupata majibu muafaka yatakayoisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana na hatimaye, kulitokomeza janga la Virusi vya Corona, COVID-19, huku kipaumbele cha kwanza kikitolewa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama vile wakimbizi na wahamiaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno, limechapisha mwongozo unaopania kuwa ni dira katika mchakato wa ujenzi mpya wa Ureno na mapambano ya changamoto za shughuli, sera na mikakati ya kichungaji inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu amewataka Maaskofu Katoliki Ureno kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya, ili wazee waweze kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za maisha ya: kiroho, kiutu, kitamaduni na kijamii. Huu ni urithi mkubwa ambao vijana wanapaswa kuutafuta na kuuambata katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno kwamba, maadhimisho ya Siku ya XXXVIII ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023 yataweza kufanyika, licha ya wasi wasi na hofu kubwa ambayo kwa sasa imetanda kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Wakati wanaagana, Baba Mtakatifu Francisko amedokezea kuhusu nia yake ya kufanya hija ya kitume nchini Iraq na hivyo kuwaomba waendelee kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili yote haya yaweze kutekelezwa kadiri ya mpango wa Mungu.

Papa: Siku 38 ya Vijana

 

 

 

14 January 2021, 15:41