Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 12 hadi 15 Januari 2015 alifanya hija ya kitume nchini Sri Lanka kama sehemu ya mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 12 hadi 15 Januari 2015 alifanya hija ya kitume nchini Sri Lanka kama sehemu ya mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa. 

Kumbukizi la Hija ya Kitume ya Papa Francisko Sri Lanka 2015

Hija ya Kitume Nchini Sri Lanka: Kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini, kwa kuendelea kujikita katika utangazaji na ushuhuda wa amani na upatanisho wa kitaifa. Pili ilikuwa ni kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz, Mtume hodari na mwaminifu wa Sri Lanka kuwa Mtakatifu. Tatu ilikuwa ni kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene nchini Sri Lanka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lengo la hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Sri Lanka kuanzia tarehe 12 hadi 15 Januari 2015, miaka sita iliyopita kwanza kabisa: ilikuwa ni kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini, kwa kuendelea kujikita katika utangazaji na ushuhuda wa amani unaofumbatwa katika ukweli, uwazi, udugu wa kibinadamu na upatanisho wa kitaifa. Pili, ilikuwa ni kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz, Mtume hodari na mwaminifu wa Sri Lanka kuwa Mtakatifu, ndiyo maana hija ya Baba Mtakatifu nchini humo iilikuwa ni cheche za imani na matumaini kwa Kanisa na kwa watu wote wenye mapenzi mema. Sri Lanka kwa muda wa miaka mingi ilijikuta ikiogelea katika dimbwi la machafuko ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu takribani miaka 26 na hatima yake ilikuwa ni hapo tarehe 18 Mei 2009. Hiki kilikuwa ni kipindi cha mateso na mahangaiko makubwa, kumbe, watu walikuwa na kiu ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu akapenda kwenda kupandikiza mbegu ya majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; kwa kukazia msamaha, umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa, ambao unafumbatwa kwa namna ya pekee katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa nchini Sri Lanka katika hija hii, lilipenda kujipambanua kwa kukazia: umuhimu kwa watu wa Mungu nchini Sri Lanka kujikita katika uaminifu, ukweli na haki, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kama ambavyo Yesu mwenyewe anawataka wafuasi wake kufikiri na kutenda. Ni changamoto ya kuwa ni sauti ya wanyonge ndani ya jamii, ili kujenga na kudumisha amani ya kudumu kati ya watu. Itakumbukwa kwamba, Rais mstaafu Mahinda Rajapaksa ndiye aliyekuwa amemwalika rasmi Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Sri Lanka, lakini siku chache tu kabla ya kuwasili kwa Baba Mtakatifu nchini humo akashindwa kwenye uchaguzi mkuu.

Baba Mtakatifu aliwashukuru watu wa Mungu nchini Sri Lanka kwa maandalizi mazuri yaliyofanikisha hija yake ya kitume nchini humo lakini kwa namna ya pekee, amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa uliojionesha mara baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa rasmi. Tukio hili lilionesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia nchini Sri Lanka. Baba Mtakatifu katika hotuba alikazia umuhimu wa toba, wongofu wa ndani, udugu wa kibinadamu na upatanisho wa kweli. Lengo ni kuganga na kuponya madonda ya vita na mipasuko wa kisiasa, ili kujenga na kudumisha umoja na haki jamii; kwa kuheshimu na kuthamini tofauti zao msingi kama amana na urithi wa Sri Lanka. Aliwataka kutambua kwamba, wote katika umoja wao wanaunda familia ya watu wa Mungu nchini Sri Lanka na kwamba, tofauti zao msingi kisiwe ni kisingizio cha machafuko ya kisiasa, kidini na kitamaduni.

Mtakatifu Paulo VI alifanya hija ya Kitume nchini humo kuanzia tarehe 4-5 Desemba 1970 na Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea nchini humo kuanzia tarehe 20-21 Januari 1995. Viongozi hawa wa Kanisa, wakati wa hija zao za kichungaji nchini Sri Lanka hawakubahatika kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu wa Madhu, kielelezo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko alibahatika kutembelea na kusali katika Madhabahu haya yanayopendwa na waamini kutoka katika dini mbali mbali nchini Sri Lanka. Hapa ni mahali wanapojisikia kupendwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa. Katika Madhabahu haya, Baba Mtakatifu alitafakari kwa kina kuhusu umuhimu wa upatanisho, toba na msamaha wa kweli, ili kuvuka kinzani na migawanyiko inayotokana na tofauti za kidini, kisiasa, kitamaduni na kikabila. Haya ni Madhabahu ambayo mahujaji wanayatumia kukimbilia na kuambata: ulinzi na tunza ya Bikira Maria, huku wakimtolea: furaha na mateso yao; imani na matumaini yao! Ni mahali pa mwanga na faraja. Aliwataka watu wa Mungu nchini Sri Lanka kuendelea kujiaminisha kwa Bikira Maria, ili aweze kuwaombea msamaha na upatanisho.

Padre Joseph Vaz, Mtume hodari na mwaminifu wa Sri Lanka ataendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa kama chombo na shuhuda wa upendo wa huruma na upatanisho na Mwenyezi Mungu. Alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Sri Lanka bila ubaguzi wowote. Akajipambanua kwa huduma ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Akasimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, huku akionesha uzuri na utakatifu wa Injili kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Baba Mtakatifu alikazia sana mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kanisa Katoliki linaheshimu na kuthamini yaliyo ya kweli na matakatifu kutoka katika dini mbalimbali. Linawahimiza wanawe ili kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene, waweze kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ilichangia kwa kiasi kikubwa mchakato wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, tayari kujielekeza zaidi katika udugu wa kibinadamu na upatanisho wa kitaifa. Kanisa Katoliki nchini Sri Lanka lilionesha umahiri mkubwa katika kuandaa na kutekeleza hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu nchini humo na kwamba, Baba Mtakatifu akaridhika na mapokezi makubwa yaliyofanywa kwake, jambo ambalo liliwasha cheche za imani, matumaini na upatanisho wa kitaifa! Changamoto kubwa kwa sasa ni misimamo mikali ya kidini na kiitikadi inayopaswa kushughulikiwa barabara ili, haki, amani na maridhiano yaweze kushika mkondo wake. Watu wa Mungu nchini Sri Lanka wajielekeze katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana, ili kuimarisha utamaduni wa udugu wa kibinadamu pamoja na kusaidiana. Hizi ni changamoto pevu, lakini penye nia pana njia, ndivyo wanavyosema na kuamini Waswahili!

Papa: Sri Lanka

 

17 January 2021, 16:06