Tafuta

Kardinali Peter Turkson. Ujumbe kwa Siku ya 68 ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2021: Kauli mbiu: Pambana na Ukoma, Ondoa Unyanyapaa, Ragibisha Afya ya Akili! Kardinali Peter Turkson. Ujumbe kwa Siku ya 68 ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2021: Kauli mbiu: Pambana na Ukoma, Ondoa Unyanyapaa, Ragibisha Afya ya Akili! 

Ujumbe wa Siku ya Ukoma Duniani Kwa Mwaka 2021: Pambana na Ukoma!

Papa Francisko anasema, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki ya afya bora, hasa miongoni mwa maskini na dhaifu ndani ya jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wataunganisha nguvu zao, ili kufutilia mbali ugonjwa wa Ukoma, ili kuwawezesha waathirika kurejea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wadau mbali mbali kwa kushirikiana na Mfuko wa Afya wa Sasakawa kutoka Japan, Jeshi la Malta, Mfuko wa Raoul Follereau pamoja na Mfuko wa Msamaria mwema, wanaendelea kuhimiza umuhimu wa viongozi wa kidini kusaidia kuelimisha umma dhidi ya tatizo la kuwabagua na kuwanyanyapalia wagonjwa wa ukoma sehemu mbalimbali za dunia. #LeprosyIsCurable, join in the fight to #EndStigma, and advocate for the #MentalWellbeing. Siku ya Ukoma Duniani iliasisiwa na Raoul Follereau kutoka Ufaransa kunako mwaka 1953, kama kumbukumbu ya kifo cha Mahatma Ghandi, kilichotokea tarehe 30 Januari 1948. Kauli mbiu inayonogesha maadhimisho ya Siku ya 68 ya Ukoma Duniani tarehe 31 Januari 2021 ni “Pambana na ukoma, Ondoa unyanyapaa, Ragibisha afya ya akili”. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili tarehe 31 Januari 2021, kutoka kwenye Maktaba binafsi iliyoko mjini Vatican, ametumia fursa hii, kuonesha uwepo na ukaribu wake kwa wagonjwa na wale wote walioathirika kutokana na Ukoma, sehemu mbalimbali za dunia.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wamisionari, wafanyakazi katika sekta ya afya na watu wa kujitolea, kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa umakini zaidi. Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki ya afya bora, hasa miongoni mwa maskini na dhaifu ndani ya jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wataunganisha nguvu zao, ili kufutilia mbali ugonjwa wa Ukoma na hivyo kuwawezesha waathirika kurejea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii zao. Ugonjwa wa Ukoma unatibika, unganisha nguvu ili kupambana na unyanyapaa; unga mkono juhudi za kuragibisha afya ya akili kwa watu waliokwisha kuathirika kwa ugonjwa wa Ukoma pamoja na magonjwa mengine ya Ukanda wa Joto! Ugonjwa wa Ukoma bado upo na watu wanaendelea kupimwa na kugundulika kwamba wanasumbuliwa na ugonjwa wa Ukoma. Inaonekana kana kwamba, ugonjwa huu pamoja na wagonjwa wenyewe wamesahaulika, jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 68 ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2021 anahimiza mapambano dhidi ya Ukoma. Anasema, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma Duniani ni changamoto inayogusa kimsingi: tiba, mapambano dhidi ya unyanyapaa, ili hatimaye, wagonjwa na waathirika wa Ukoma waweze kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao kama binadamu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikutana na wagonjwa wa Ukoma, akawagusa, akawafariji na kuwaponya, kiasi kwamba, Msamaria mmoja tu kati ya wale wagonjwa kumi aliyethubutu kurejea kwa Kristo Yesu, ili kumpatia Mungu utukufu. Yesu alihitisha mkutano huu kwa kumwambia yule Msamaria, “Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.” Lk. 17:19. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, akawaganga na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa kimwili, ili kuwarejeshea tena ule utu, heshima na haki zao msingi.

Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya Wokovu, inayomwangalia mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kuwa na mwelekeo wa kijamii. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sayansi na tiba ya mwanadamu. Dawa zilizogunduliwa zinaonekana kuwa na ubora zaidi katika kutibu ugonjwa wa Ukoma na hivyo kuwarejeshea watu matumaini. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anaendelea kufafanua kwamba, mchakato mzima wa afya hauna budi kujielekeza zaidi katika: Kuzuia, kupima, kuganga na kutibu: kimwili na kisaikolojia; kwa kuangalia pia maisha ya kijamii na kiroho, ili kuweza kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Shirika la Afya Duniani, WHO linabainisha kwamba, unyanyapaa ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili wagonjwa na waaathirika wa Ukoma. Wagonjwa wengi wanaendelea kutengwa kijamii, kiasi hata cha kutumbukia katika ugonjwa wa sonona pamoja na kuathirika kiuchumi.

Kumbe, kuwashirikisha waathirika katika maisha ya kijamii ni kati ya vipaumbele vya Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Hawa ni watu wanaohitaji kuungwa mkono kiuchumi kwa ajili ya ustawi wao wenyewe pamoja na familia zao. Hii inatokana na ukweli kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa msukumo wa pekee kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Mchakato wa uragibishaji wa afya ya akili kwa wagonjwa wa Ukoma ni muhimu sana kwa wakati huu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Ukoma una athari kubwa katika viungo vya binadamu. Kumbe, wagonjwa hawa wanapaswa kusaidiwa, ili kuweza kujikimu pamoja na kuendelea kushirikiana na wenzao katika jamii, kwani kimsingi binadamu na kiumbe jamii, anapaswa kukutana na jirani zake. Wafanyakazi katika sekta ya afya na jamii katika ujumla wake, wanaweza kusaidia kufanikisha mchakato huu kwa ajili ya wagonjwa wa Ukoma pamoja na familia zao.

Kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kuganga na kutibu ugonjwa wa Ukoma, basi, waunge mkono juhudi za uragibishaji wa afya ya akili kwa wagonjwa wa Ukoma, kama sehemu ya mchakato wa kupambana na ugonjwa wa Ukoma duniani.   Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu anahitimisha ujumbe wake kwa  Siku ya 68 ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2021 ambayo imenogeshwa kwa kauli mbiu: “Pambana na ukoma, Ondoa unyanyapaa, Ragibisha afya ya akili” kwa kuwashukuru wadau wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Ukoma. Huu ni ugonjwa unaotibika, lakini unahitaji mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayoweza kusaidia kupambana na unyanyapaa, kama sehemu ya ujenzi wa jamii shirikishi na fungamani; muhimu sana katika mchakato wa kujenga na kudumisha afya bora zaidi.

Siku ya Ukoma
31 Januari 2021, 15:26