Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo Kwa Mwaka 2021: Wongofu wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa: Umoja na Ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo Kwa Mwaka 2021: Wongofu wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa: Umoja na Ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Wongofu wa Paulo!

Kutokana na sababu zilizoko nje ya uwezo wake, Baba Mtakatifu Francisko hataweza kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma. Na badala yake, Kardinali Kurt Koch ataongoza Ibada. Hii ni Sherehe ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa sanjari na kufunga Juma la 54 la Kuombea Umoja wa Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na sababu zilizoko nje ya uwezo wa Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 25 Januari 2021 kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya, hataweza kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma. Nabadala yake, amemteua Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kuongoza Ibada hii. Itakumbukwa kwamba,  hii ni sehemu ya sherehe ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa sanjari na kufunga Juma la 54 la Kuombea Umoja wa Wakristo. Kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho haya ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn 15-5-9. Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli ni ufafanuzi unaotolewa katika Injili ya Yohane 15:1-17. Jumuiya ya Wamonaki 50 kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo wa Grandchamp iliyoko nchini Uswisi ndiyo iliyopewa dhamana ya kuandaa masomo, sala na tafakari kwa mwaka 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” iliyoanzisha Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Tatu ya Mwaka wa Kanisa, anakazia umuhimu wa utambulisho wa Wakristo unaofumbatwa katika mahusiano na mafungamano yao ya dhati na Kristo Yesu, Mfufuka, Jumuiya ya Waamini pamoja na Maandiko Matakatifu kama njia muafaka ya kuelewa matukio ya maisha na utume wa Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake.

Dominika ya Neno la Mungu iwe ni chachu ya kukoleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiyahudi pamoja na kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo. Iwe ni nafasi ya kukazia usomaji bora wa Biblia. Kauli mbiu inayonogesha maadhimisho ya Juma la 54 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021 ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Changamoto nyingine inayoletwa na Maandiko Matakatifu inahusu mapendo. Neno la Mungu ni mwaliko wa daima kwenye upendo wa Mungu Baba uliojaa huruma na unaowadai watoto wake kuishi katika mapendo. Maisha ya Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utimilifu wa upendo wa Mungu kwa waja wake, upendo uliomsukuma kujitosa bila ya kujibakiza. Huu ndio upendo unaopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo makini cha ushuhuda wa uekumene wa huduma. Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo unaotawaliwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Neno la Mungu liyafungue macho ya waamini ili waweze kuachana na ubinafsi na uchoyo, ili kuanza kujikita katika mchakato wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa kujiaminisha katika Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa kiinjili kati yao na kati ya watu wa Mataifa, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu, alama yenye mvuto na mashiko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, na kama sehemu muhimu sana ya mapambano dhidi ya changamoto mamboleo. Wakristo kama ilivyokuwa kwa nyakati za Mtakatifu Paulo wanapaswa kujitahidi kuungana pamoja kwa njia ya mawazo na maneno na kwamba, umoja huu si mkakati wa kibinadamu bali ni changamoto kutoka kwa Kristo mwenyewe, anayewavuta wafuasi wake kuungana sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake yanayojikita katika upendo kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye kiini, sababu na kikolezo cha umoja miongoni mwa Wakristo. Utengano miongoni mwa Wakristo si jambo la kawaida anasema Baba Mtakatifu Francisko, linahitaji kufanyiwa marekebisho ya kina, kwani utengano kati ya Wakristo una madhara makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Unahatarisha ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo duniani.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo ndiye msingi wa Kanisa na urithi wa wakristo wote. Lakini inasikitisha kuona kwamba, bado Wakristo wenyewe wamegawanyika kinyume kabisa cha utashi wa Kristo mwenyewe na utengano huu unaendelea kuwa ni kielelezo cha kashfa ya ushuhuda wa utangazaji wa Injili duniani. Baba Mtakatifu anawatia shime Wakristo kufanya hija pamoja na kutegemezana ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo. Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, dhana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro imejidhihirisha wazi, mwaliko wa kuendelea kufahamiana zaidi kwa ajili ya majadiliano ya Kiekumene kwa kutambua utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata kwa siku za usoni. Changamoto na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza katika majadiliano ya Kiekumene ni mambo ambayo hayawezi kufichika, lakini kuna haja kwa Wakristo wapige moyo konde na kuanza kujivika utashi wa Kristo kwa ajili ya umoja miongoni mwa Wakristo. Wawe tayari kuvuka vikwazo vyote vinavyosababisha utengano na hivyo kujivika nguvu ya upendo inayotolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa.

Wongofu wa Paulo Mtume

 

23 January 2021, 14:48