Tafuta

Tetemeko la ardhi Kroatia,Papa aonesha ukaribu na kuomba msaada upelekwe

Mara baada ya katekesi ikiwa ni ya mwisho kwa mwaka 2020,Papa Francisko mawazo yake maalum ni kwa ajili ya nchi ya Kroatia ambayo tarehe 29 Desemba wamekumbwa na tetemeko la ardhi.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Jumatano tarehe 30 Desemba 2020, mara baada ya katekesi ya mwisho  kwa mwaka huu Papa Francisko mawazo yake yamewaendea nchi ya Kroatia ambayo siku ya Jumanne tarehe 29 Desemba, tetemeko la ardhi liliwakumba na kusababisha uhalibifu mkubwa na kwa njia hiyo ametoa wito wa kuwa na mshikamano na msaada kwa watu hao. Katika maneno ya Papa amesema: “Jana tetemeko la ardhi, limesababisha wathirika na uharibifu mkubwa huko Kroatia. Ninaonesha ukaribu wangu kwa majeruhi na  wote ambao wamekumbwa na tetemeko hilo na ninasali kwa namna ya pekee kwa wale ambao wamepoteza maisha na kwa ajili ya familia zao. Ni mategemeo yangu kuwa Mamlaka ya Nchi na msaada wa Jumuiya ya kimataifa, vinaweza kuwafikia haraka ili kutoa faraja ya mateso ya watu wapendwa wa Kroatia”.

Takwimu kamili bado lakini vipo vifo na majeruhi 

Takwimu za tetemeko hilo bado hazijatolewa lakini inasadikika watu saba wamekufa na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Caritas kwa sasa iko mstari wa mbele kutoa msaada na ahadi za Umoja wa Ulaya za kutoa msaada pia  lakini bado nchi ya Kroatia inaendelea kutetemeka japokuwa kuna matumaini ya kupata hata watu wakiwa hai ambao wamefunikwa na vifusi vya tetemeko la ardhi. Utafutaji huo ulidumu usiku kucha na hadi sasa wameokoa watu sita huko Petrinja, kitovu cha tetemeko la ardhi, karibu kilomita hamsini, kusini mashariki mwa mji mkuu Zagreb. Hivi sasa idadi ya watu wasiopungua saba wamekufa na kadhaa wamejeruhiwa, wengine wao wakiwa katika hali mbaya. Kuna uharibifu mwingi huko Zagreb, katika hospitali, shule za watoto, majengo ya wizara na hata majengo ya kidini pia yameharibiwa vibaya.

Msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa

Kiukweli, mashine ya uokoaji ya kimataifa tayari iko katika mchakato. Waziri Mkuu wa Kroatia Andrej Plenkovic alitangaza mgawanyo wa awali wa euro milioni 16 ili kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi, wakati Rais wa Tume ya Ulaya, Bi. Ursula von der Leyen, alielezea utayari kamili wa Umoja wa (EU) wa kutoa msaada kwa Kroatia. Italia pia, kupitia mkuu wa nchi Rais Mattarella na Waziri Mkuu Conte, wameonesha mshikamano kamili wa msaada kwa watu wa Kroatia wote unaohitajika.

Wito wa askofu wa Sisak

Caritas ya Italia pia ikishirikiana mara moja na ile ya Kikroeshia inajaribu kuandaa msaada wa kwanza kupelekwa kwa waathirika, katika maeneo ambayo hata hivyo ukosefu wa umeme na mawasilianoya  simu  yanafanya kila kitu kuwa kigumu zaidi. Mkurugenzi wa Caritas jimbo la Sisak, Kristina Radic, ametangaza kuwa hali ni mbaya na askofu wa Sisak, Vlado Kosic, ametoa ombi kwamba: “tuwaombee wale wote ambao wameathirika. Tujaribu pia kubaki na umoja katika mkasa huu ambao umehusisha Kroatia yote na hasa jimbo letu la Sisak, kama vile ambavyo tumekuwa pamoja katika majanga mengine mengi ambayo yameathiri jumuiya yetu katika siku za hivi karibuni, kama vile vita na janga linaloendelea”.

30 December 2020, 12:08