Tafuta

Papa Francisko Ujumbe na Baraka za Noeli "Urbi et Orbi" kwa Mwaka 2020: Ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na changamoto mamboleo! Papa Francisko Ujumbe na Baraka za Noeli "Urbi et Orbi" kwa Mwaka 2020: Ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na changamoto mamboleo! 

Papa Francisko: Ujumbe wa "Urbi et Orbi:2020": Upendo na Udugu wa Kibinadamu

Urbi et Orbi: Yesu ni ufunuo wa Uso wa Baba wa milele na kwa njia yake, binadamu wote wanaweza kuitana na kuwa ni ndugu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, lugha, tamaduni, utambulisho na utofauti, lakini wote ni ndugu wamoja! Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtafakari Mtoto Yesu aliyewawezesha kuwa ndugu wamoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, Mama Kanisa anatangaza Habari Njema ya Wokovu kwamba, “maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto”. Isa. 9:6. Kuzaliwa kwa mtoto, daima imekuwa ni chemchemi ya matumaini na maisha mapya kwa siku za mbeleni. Kristo Yesu amezaliwa kwa ajili ya binadamu wote na wala hakuna mipaka, upendeleo wala mtu awaye yote kutengwa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria mjini Bethlehemu ni kwa ajili ya wote kwani ametolewa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya familia yote ya binadamu. Ni kwa njia ya Kristo Yesu, watu wote wanaweza kuthubutu kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba”. Kristo Yesu ni Mwana mzaliwa wa kwanza wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa Baba wa milele na kwa njia yake, binadamu wote wanaweza kuitana na kuwa ni ndugu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, lugha, tamaduni, utambulisho na utofauti, lakini wote ni ndugu wamoja! Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli tarehe 25 Desemba 2020 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtafakari Mtoto Yesu aliyewawezesha kuwa ndugu wamoja.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi hiki cha historia ya mwanadamu, kimeguswa na kutikiswa kwa namna ya pekee kabisa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa uchumi na hivyo kusababisha mwelekeo tenge katika jamii, hali inayodai ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Mwenyezi Mungu amewapatia Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu, ili aweze kuwa ndugu yao. Huu ni undugu unaofumbatwa katika upendo unaomwezesha mtu kukutana na jirani zake, licha ya tofauti zao msingi. Kwa njia hii, ataweza kuguswa na mateso na mahangaiko yake, tayari kumkaribia, ili kuweza kumhudumia kama alivyofanya yule Msamaria mwema. Haijalishi kama mtu huyu anatoka katika familia, kabila au dini yake, lakini ni ndugu yake. Mwelekeo huu ndio unaopaswa kuzingatiwa hata katika mahusiano na mafungamano kati ya watu na Mataifa. Nyota angavu ya Bethlehemu iwe ni chanzo cha matumaini mapya na ushirikiano wa Kimataifa, ili watu wengi zaidi waweze kupata chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuondokana na uchoyo na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko.

Haki ya huduma bora ya afya, iwe ni kipimo cha upendo unaopaswa kushuhudiwa na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni wakati wa kushirikiana na kushikamana na wala si kufanya mashindano. Ni muda wa kutafuta suluhu ya kudumu, itakayowawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Maskini na wahitaji zaidi wapewe kipaumbele cha kwanza.  Mtoto Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu awasaidie watu kuwajibika barabara, kwa kuonesha ukarimu na mshikamano hasa kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii; maskini, watu wasiokuwa na ajira na wale wote wanaoteseka kutokana na athari za ugonjwa wa Corona, COVID-19, bila kuwasahau wanawake na wasichana ambao katika kipindi hiki wamekumbana na nyanyaso za kijinsia katika maisha yao. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu awawezeshe viongozi wa kisiasa na wale wote wenye dhamana ya kuongoza jamii, umuhimu wa kugundua tena upyaisho wa ushirikiano kimataifa, huku wakianzia kwenye sekta ya afya, ili watu wote waweze kupata fursa ya chanjo na huduma msingi za afya.

Katika changamoto hii ambayo haitambui mipaka, hakuna sababu msingi ya kuweka vizuizi, kwa sababu binadamu wote wamejikuta wakiwa wamepanda “boti moja” ambayo kwa sasa imekumbwa na dhoruba ya gonjwa la Corona, COVID-19. Watu wote wajisikie kuwa ni ndugu wamoja; watu wanaoakisi Sura ya Mungu hasa wale wanaoteseka na kwamba, Mwenyezi Mungu anaomba msaada kwa ajili yao. Watu wajitahidi kumwona Mwenyezi Mungu kati ya wagonjwa, maskini, wasiokuwa na ajira, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wamwone Mungu kati ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, katika Sherehe za Noeli, Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kuzaliwa kama Mtoto mchanga, Mama Kanisa anapenda kuyaelekeza macho yake kwa umati wa watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia, lakini zaidi kutoka Siria, Iraq na Yemen wanaoteseka kwa kulipia gharama za vita na machafuko ya kisiasa. Nyuso zao zinawasuta watu wenye dhamiri nyofu, ili waweze kujizatiti kubainisha na hatimaye, kupambana fika na mambo yote yale yanayosababisha vita na kinzani, ili kwa ujasiri mkubwa waweze kujenga leo na kesho inayosimikwa katika misingi ya amani. Huu ni muda muafaka wa kusitisha kinzani huko Mashariki ya Kati na katika Ukanda wa Mediterrania ya Mashariki.

Baba Mtakatifu anamwomba Mtoto Yesu ili aweze kuganga na kuponya madonda ya Siria ambayo kwa muda wa takribani miaka kumi, imetumbukia katika vita ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, hali ambayo inagumishwa pia na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Corona, COVID-19. Mtoto Yesu awe ni faraja kwa watu wa Mungu nchini Iraq na kwa wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa upatanisho wa kitaifa, lakini kwa namna ya pekee kabisa kwa jamii ya Wayazid ambao wameathirika sana kutokana na vita ya miaka ya hivi karibuni. Mtoto Yesu alete amani nchini Libya na hivyo kuwezesha awamu mpya ya majadiliano yanayoendelea kwa wakati huu yaweze kusitisha chuki na uhasama nchini Libya. Mtoto Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu awakirimie udugu wa kibinadamu, watu wa Mungu katika Nchi Takatifu, iliyoshuhudia kuzaliwa kwake. Waisraeli na Wapalestina, waaminiane, ili kwa pamoja waweze kutafuta na hatimaye kuambata amani yenye mwelekeo mpana zaidi, amani inayosimikwa katika misingi ya haki; amani inayodumu kwa sababu imekita mizizi yake katika majadiliano, ili kuvunjilia mbali vita na hivyo kuvuka mawazo ya uadui, ili mwisho wa siku, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uzuri wa udugu ulimwenguni.

Nyota angavu iliyofukuza giza la Usiku wa Noeli, iwe ni mwongozo unaowatia shime watu wa Mungu nchini Lebanon, katika magumu wanayokabiliana nayo, kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa wasikate tamaa. Mfalme wa amani, awawezeshe viongozi nchini humo, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Lebaoni, huku wakiongozwa na kanuni ya ukweli, uwazi na uaminifu, ili kuleta mageuzi makubwa yanayohitajika nchini humo, ili hatimaye kudumisha uhuru na maridhiano kati ya watu. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu, asaidie juhudi za Jumuiya ya Kimataifa na hasa kwa nchi zile  ambazo zimekumbwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, ili ziweze kusitisha vita na hatimaye, amani iweze kutawala tena hasa huko Nagorno-Karabakh, huko Mashariki wa nchi ya Ukraine, ili kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani na upatanisho wa kitaifa. Mwana wa Mungu aliyezaliwa mjini Bethlehemu awaondolee mateso watu wa Mungu nchini Burkina Faso, Mali na Niger, ambazo zimeathirika vibaya sana na kinzani mbalimbali ambazo msingi wake ni misimamo mikali ya kidini, mapambano ya silaha pamoja na maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, bila kusahau majanga asilia.

Baba Mtakatifu anaiombea Ethiopia ambayo imetumbukia tena kwenye vita ya wenyewe kwa wenyew na hivyo kusababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao; Kristo Yesu, alete faraja kwa wananchi wanaoishi katika Jimbo la Cabo Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji; ambako watu wanateseka sana kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Mtoto Yesu awaguse viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini, Nigeria na Cameroon waweze kuanza mchakato wa udugu na majadiliano katika ukweli na uwazi, waliyoyaanza hivi karibuni. Neno wa Baba wa Milele awe ni chemchemi ya matumaini kwa wananchi wa Amerika ya Kusini, ambao wameathirika sana kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Gonjwa hili hatari limechochea pia rushwa, ufisadi pamoja na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Asaidie kuganga na kuponya mipasuko ya kijamii iliyojitokeza hivi karibuni nchini Chile na hatimaye, alete nafuu ya maisha kwa wananchi wa Venezuela. Mfalme wa mbingu awalinde na kuwatunza watu walioathirika kutokana na majanga asilia Barani Asia na kwa namna ya pekee kabisa nchini Ufilippini na Vietnam ambazo zimekumbwa na dhoruba kali ambazo zimesababisha mafuriko na hivyo kuleta maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao; uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na shughuli za uchumi mahalia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapolikumbuka Bara la Asia, kamwe hawezi kuwasahau watu wa Rohingya: Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele alizaliwa katika mazingira duni na kati ya watu maskini, awe ni chemchemi ya matumaini katika shida na mahangaiko yao. Mtoto aliyezaliwa kwa ajili yenu, amekuja ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na uvuli wa mauti. Anapenda kuwatangazia watu kwamba, mateso na machungu ya dhambi, hayana usemi wa mwisho. Hakuna sababu ya kukata tamaa kutokana na vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu unaoendelea sehemu mbalimbali za dunia, kwani kwa kufanya hivyo kungemaanisha kukataa na “kusigina” furaha na matumaini ya Sherehe ya Noeli. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” amewakumbuka wale wote ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwapatia jirani zao matumaini, faraja na msaada; kwa kuendelea kuwasaidia na kuwahudumia watu wanaoishi upweke licha ya hatari kubwa ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Kristo Yesu alizaliwa katika hori ya kulishia wanyama, lakini akazungushiwa upendo uliokuwa unabubujika kutoka kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Kwa Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu amebariki na kuweka wakfu upendo wa kifamilia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea wale wote ambao kutokana na sababu mbalimbali hawataweza kuungana na familia zao; wale ambao wamelazimika kubaki wakiwa wamejifungia majumbani mwao kwa sababu mbalimbali. Kwa watu wote hawa, Sherehe za Noeli ni muda muafaka wa kutambua na kugundua kwamba familia ni chemchemi ya Injili ya uhai na imani; mahali pa upendo wenye ukarimu; mahali pa majadiliano katika ukweli na uwazi; msamaha, mshikamano wa kidugu na furaha shirikishi; familia ni chemchemi ya amani kwa ajili ya binadamu wote! Na kwa maneno haya, Baba Mtakatifu amehitimisha ujumbe wake, na kuwatakia wote heri na baraka za Noeli kwa Mwaka 2020.

Urbi et Orbi 2020
25 December 2020, 15:53