Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2020 ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 84 tangu alipozaliwa! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2020 ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 84 tangu alipozaliwa! 

Papa Francisko Kumbukizi la Miaka 84 Tangu Alipozaliwa! Upendo!

Papa Francisko amewasihi waamini kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, watu ambao walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Kama sehemu ya kumbukumbu ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu ametoa zawadi ya mashine nne za kupumulia zitakazopelekwa nchini Venezuela ili kuwasaidia watoto wagonjwa wa mfumo wa hewa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2020 amefanya kumbukizi la miaka 84 tangu alipozaliwa katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu. Ni siku ambayo imesheheni, sala na tafakari pamoja na kushirikishana furaha hii na wakazi wa Hosteli wa Santa Martha iliyoko mjini Vatican ambayo kwa sasa ni makazi ya Baba Mtakatifu. Maskini kutoka sehemu mbalimbali za mji wa Roma wamemzawadia Baba Mtakatifu maua ambayo yamepamba Kikanisa cha Mtakatifu Martha. Baba Mtakatifu amewasihi waamini kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Kama sehemu ya kumbukumbu ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu ametoa zawadi ya mashine nne za kupumulia zitakazopelekwa nchini Venezuela ili kuwasaidia watoto wanaoteseka na magonjwa ya mfumo wa hewa! Baba Mtakatifu amepata pia nafasi ya kupokea salam na matashi mema kutoka ndani na nje ya Italia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika salam zake ambazo zimekazia upendo kati ya ndugu, utajiri ambao umechotwa katika Utenzi wa Upendo kama ulivyoandikwa na Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 13:1-13 wanakazia zaidi fadhila ya upendo, kwa kusema kwamba, upendo unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya waamini. Kamwe watu wasipende kuhatarisha upendo na kwamba, hatari kubwa kwa sasa ni kutokupenda! Katika maadhimisho ya miaka 84, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linapenda kutolea Mwenyezi Mungu sala, sifa na utenzi wa shukrani kwa jitihada zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika kukuza na kudumisha upendo na udugu wa kibinadamu, unaovuka na kuvunjilia mbali mipaka na hivyo kuwawezesha waamini kuwa na nyoyo huru kabisa!

Upendo ni kiini na msingi wa imani ya Kanisa. Ni kwa njia ya huruma na upendo wa dhati, Mwenyezi Mungu amejimwilisha katika historia na kuutwaa mwili wa binadamu. Kwa kusukumwa na upendo wa dhati, Kristo Yesu, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kuwakirimia binadamu amana na zawadi ya upendo. Waamini wanapaswa kushikamana kikamilufu na fadhila ya upendo ambao kimsingi ni dira na mwongozo wa maisha. Ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Upendo unaliwezesha Kanisa kufupisha umbali kati ya watu wa Mataifa; upendo unawavuta na kuwaunganisha watu na historia yao, hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, ili kwa njia ya upendo huu usiokuwa na mawaa, watu waweze kushikamana katika sala, wasaidiane kupambana na gonjwa hili, ili kwa pamoja waweze kuganga na kuponya madonda na majeraha ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwakumbusha watu wa Mungu umuhimu wa fadhila ya upendo katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wanapenda kumhakikishia sala zao, huku wakiwa wameungana na waamini katika Jumuiya zao. Maaskofu wanaahidi kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa moyo wa shukrani na matumaini yanayobubujika kutoka katika mafundisho na ushuhuda wa maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Upendo ni dira na mwongozo wa maisha! Kwa upande wake, Salvatore Martinez, Rais wa Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki Italia, amemmshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia Baba Mtakatifu Francisko zawadi ya maisha, unabii katika nyakati hizi na daraja la upatanisho wa kibinadamu na udugu unaomwilishwa katika matendo. Chama hiki cha kitume, kinaendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kwa njia ya sala, ili Roho Mtakatifu aweze kumwongoza na kumtegemeza; amlinde na kumhifadhi dhidi ya mabaya; amjalie na kumkirimia neema na baraka anazohitaji katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki na amani.

Itakumbukwa kwamba, Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Italia amemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko. Kwa upande wake, Giuseppe Conte, Waziri mkuu wa Italia katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, amemwambia Baba Mtakatifu kwamba, wanafuatilia kwa heshima na taadhima, utume wake unaopania kuliwezesha Kanisa kuwa jirani zaidi na watu, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wadogo na wanyonge katika jamii.

Papa Miaka 84

 

 

18 December 2020, 14:22