Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Mahubiri ya Mkesha wa Noeli 2020: Kwa ajili yenu Mtoto Yesu amezaliwa! Baba Mtakatifu Francisko Mahubiri ya Mkesha wa Noeli 2020: Kwa ajili yenu Mtoto Yesu amezaliwa! 

Papa Francisko: Mahubiri Kesha la Noeli 2020: Mtoto Yesu Amezaliwa!

Mkesha wa Noeli amekazia furaha ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu ambayo ni neema ya Mungu, chemchemi ya maisha na matumaini mapya, upendo unaoganga na kuponya madonda ya binadamu. Amezaliwa katika hali ya umaskini na kati ya maskini, ili kumkomboa mwanadamu. Hii ni changamoto ya kupenda na kupendwa, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja katika Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Desemba, 2020 ameongoza na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika mkesha wa Sherehe ya Noeli, katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada ya Misa Takatifu imetanguliwa na wimbo wa Kalenda unaotangaza Fumbo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliyetabiriwa na Manabii tangu Agano la Kale. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awajalie watu wote neema ya kuishi ujumbe wa Noeli, ambao kimsingi ni chemchemi ya amani ya kweli, furaha na maisha mapya. Sherehe za Noeli zinapata umuhimu wa pekee, ikiwa kama zinaadhimishwa katika upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu: kwa kuwakumbuka, kuwafariji na kuwasaidia wagonjwa, maskini, wahitaji na wale wote wanaoelemewa na upweke. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye mkesha wa Sherehe ya Noeli amekazia furaha ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu ambayo ni kwa ajili ya watu wote, ni neema ya Mungu, chemchemi ya maisha na matumaini mapya, upendo unaoganga na kuponya madonda ya binadamu. Amezaliwa katika hali ya umaskini na kati ya maskini, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa kukazia mambo msingi katika maisha.

Hii ni changamoto ya kupenda na kupendwa, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja! Baba Mtakatifu anasema, katika mkesha wa Noeli, utabiri wa Nabii Isaya: “maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto”. Isa. 9:6. Unatimilika na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha kuu katika maisha. Noeli ni Sherehe ya Fumbo la kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kuzaliwa upya kutoka katika undani wa mtu. Huyu ni Mtoto ambaye amezaliwa kwa ajili ya wote, asili ya baraka anayekuja kuwakirimia watu neema ya kuwa ni watoto wateule wa Mungu, zawadi kubwa na yenye kushangaza sana kwani hata katika udhaifu na mapungufu ya kibinadamu, bado Mwenyezi Mungu anathubutu kumwita mwanadamu, mtoto wake mpendwa, kiasi cha kumpatia ujasiri wa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Jambo la msingi ni kwa kila binadamu kujitambua kwamba yeye ni mtoto mpendwa wa Mungu, chanzo cha matumaini mapya yanayorekebisha, yanayoganga na kuponya udhaifu na mapungufu yaliyoyojitokeza katika historia ya maisha ya mwanadamu.

Wakati mwingine hii ni hofu, lakini Mwenyezi Mungu anapenda kuwakumbusha waja wake, kwamba, wao ni watoto wake wapendwa na Yeye ni chanzo cha upendo wa bure kabisa! Mkesha wa Noeli unafafanua na kubainisha neema hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa mastahili au jeuri ya kibinadamu. Watu wote ni mali ya Mungu: “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa” Tit. 2:11. Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu Mtoto wake mpendwa, kiini cha furaha yake, hata ikiwa kama bado kuna ukosefu wa haki kumwelekea Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Hii ni kutokana na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, kinyume kabisa na maelekeo ya kibinadamu. Mwenyezi Mungu anawapenda binadamu upeo, kuliko hata wanavyojipenda wenyewe, hii ndiyo siri ya Mungu kuweza kupenya katika moyo wa mwanadamu. Lengo la Mungu ni upendo unaobubujika kutoka katika undani wa moyo wake, unaogeuka na kuwa ni chemchemi ya wokovu na upendo wa Mungu.

Huu ni upendo usiochoka hata kidogo. Upendo wa Yesu unapyaisha maisha, unaganga na kuponya madonda ya maisha ya mwanadamu; inawaokoa waamini kutoka katika mizizi ya dhambi, hali ya kutoridhika, chuki na hasira pamoja na “litania” ya malalamiko. Mtoto Yesu amezaliwa katika hori ya kulishia wanyama na katika hali ya umaskini hii ni kutokana na ukweli kwamba, hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu amejitwalia hali ya kibinadamu, ili kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka, ili asiwepo tena mtu anayesukumizwa pembeni mwa jamii kutokana na hali yake ya maisha. Kama ilivyokuwa mjini Bethlehemu, Mwenyezi Mungu anapenda kufanya mambo makubwa kupitia katika mambo dhaifu. Akaweka wokovu wa binadamu katika hori ya kulishia wanyama na wala hakuogopa umaskini na udhaifu wa binadamu, bali akapenda huruma na upendo wake wa daima, viweze kupyaisha tena hali na mapungufu ya maisha ya binadamu.

Mwinjili Luka anasema Malaika aliwaambia wale wachungaji waliokuwa wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu ya usiku: “Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.” Lk. 2:12. Ishara hii ni mwelekeo na dira ya maisha. Bethlehemu maana yake ni “Nyumba ya mkate”, Kristo Yesu aliyezaliwa na kulazwa kwenye hori ya kulishia wanyama ni mkate wa uzima na maisha ya milele. Huu ndio Mkate ulioshuka kutoka mbinguni unazima kiu ya mambo msingi katika maisha. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, watu wanapojiachia na hatimaye, kumezwa na malimwengu wanabaki na utupu katika maisha yao. Changamoto kwa waamini ni kumtambua Mwenyezi Mungu kuwa ni chemchemi ya maisha yao na kwamba, wajitahidi kuzima kiu na njaa ya maisha ya kiroho kutoka kwa Kristo Yesu, kwa kushibishwa na upendo wake wa dhati, tayari kuwapenda jirani kama utekelezaji wa Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Neno wa Mungu ana sadaka maisha yake kwa ajili ya waja wake. Mwanadamu amepewa Mtoto wa Mungu, anayehitaji kupendwa, kulindwa na kuhudumiwa kikamilifu.

Mtoto akipendwa, ataweza pia kuwashirikisha wengine upendo huo. Mwenyezi Mungu amependa kuzaliwa kama Mtoto mdogo, ili kumsukuma mwanadamu kupenda kama anavyopenda yeye. Huu ni muda muafaka wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili. Kwa kuwahudumia maskini, watu wanaonesha pia upendo kwa Mungu. Mwenyezi Mungu anampenda kila mtu jinsi alivyo. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake ya kesha la Noeli 2020 kwa kuwaalika waamini kumpokea na kumkumbatia Mtoto Yesu aliyezaliwa kwenye hori kulia wanyama, ili kukumbatia maisha yao. Wampokee Mtoto Yesu, Mkate wa uzima, tayari kujisaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani. Waamini wajifunze kuhudumia kwa moyo wa upendo, wakiwa tayari kuwafariji wale wote wanaoteseka, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja!

Papa: Kesha Noeli 2020
25 December 2020, 15:26