Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka waamini kujiandaa kikamilifu kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na sala zinazomwilishwa katika matendo ya huruma kama njia ya kumkaribisha na kumpokea Kristo Yesu. Papa Francisko anawataka waamini kujiandaa kikamilifu kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na sala zinazomwilishwa katika matendo ya huruma kama njia ya kumkaribisha na kumpokea Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Jiandaeni Kikamilifu Kwa Sherehe za Noeli

Kwenye Pango la Noeli mjini Bethlehemu kuna umaskini na upendo wa kweli, changamoto ya kuweza kujiandaa kikamilifu kumkaribisha na kumpokea Mwenyezi Mungu. Maneno ya Bikira Maria “Na iwe kwangu kama ulivyosema” yanafunga rasmi Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio, mwaliko wa kupiga hatua kubwa zaidi kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Noeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio Mwaka B wa Kanisa inamweka Bikira Maria na Malaika Gabrieli kuwa wahusika wakuu. Malaika Gabrieli anawakilisha ujumbe wa Mungu kwa Bikira Maria aliyekuwa ameposwa na Yosefu wa mbari ya Daudi. Salam Maria, tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Kwa haraka haraka mtu anaweza kudhani kwamba, salam hii ni chemchemi ambayo ingeleta furaha ya kweli kwa Bikira Maria. Katika hali na mazingira ya wakati ule, Je, ni mwanamke gani aliyekuwa na ndoto ya kuchukua mimba na kumzaa Masiha. Salam hii ilikuwa imesheheni pia majaribu makubwa katika maisha ya Bikira Maria. Hii inatokana na ukweli kwamba, alikuwa ameposwa na Yusufu. Katika muktadha huu, Sheria ya Musa ilikataza wachumba kuishi unyumba kabla ya kufunga ndoa. Kumbe, Bikira Maria kupata mimba kabla ya ndoa, ni tendo ambalo lilikuwa  ni uvunjifu wa Sheria ya Musa na adhabu yake ilikuwa ni kupigwa mawe hadi kufa! Haya ndiyo yalikuwa yanamsibu Bikira Maria. Bila shaka ujumbe wa Neno la Mungu uliujaza Moyo wa Bikira Maria mwanga wa nguvu! Hata hivyo, mbele yake kulikuwa na mtihani mkubwa katika maisha. Kwa kukubali na kuitikia “Ndiyo” kwa Mwenyezi Mungu, alikua anahatarisha hata maisha yake mwenyewe au angeweza kuamua kufuata njia yake ya maisha ya kawaida!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio, tarehe 20 Desemba 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema, Bikira Maria “alipiga moyo konde” na kuamua kujibu kwa ujasiri akisema, “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. “Fiat” yaani “Ndiyo” ya Bikira Maria inaonesha ari kuu ya kutaka kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake bila kupindisha maneno kama sehemu ya kukubali kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Bikira Maria alikuwa na uwezo wa kumwomba Mwenyezi Mungu nafasi ya kufanya tafakari ya kina na kisha kumpatia majibu muafaka. Bikira Maria hakuhitaji ufafanuzi wa yale ambayo yangeweza kujitokeza huko mbeleni na hivyo kuweka masharti kidogo juu ya uamuzi wake. Bikira Maria hakupoteza muda hata kidogo wala kumsubirisha Mwenyezi Mungu au kuhairisha maamuzi yake. Baba Mtakatifu amewageukiwa waamini na kuwahoji ni mara ngapi katika maisha hata yale ya kiroho yamekuwa yakipigwa “danadana?”. Waamini wanatambua umuhimu wa sala katika maisha, lakini mara ngapi wamejiwekea visingizio vinavyowafanya kushindwa kusali? Mara ngapi watu wameshindwa kuwasaidia jirani zao licha ya kutambua umuhimu wa msaada kwa watu hawa?

Baba Mtakatifu Francisko anasema, leo katika lango la Maadhimisho ya Sherehe za Noeli, Bikira Maria anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutokuhairisha, bali wajizatiti kusema “Ndiyo”. Lakini, ikumbukwe kwamba, kila “Ndiyo” ina gharama zake. “Ndiyo” ya Bikira Maria imemgharimu ujasiri na utayari wa kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake, uamuzi ambao umewawezesha watu wa Mungu kupata ukombozi. Baba Mtakatifu anasema hata kwa waamini wa nyakati hizi ambazo zimesheheni magumu na changamoto nyingi, bado wanaweza kusema “Ndiyo” badala ya kulalamikia mambo ambayo wanashindwa kutekeleza kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hii ni changamoto ya kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuwasaidia maskini. Zawadi za Noeli zisiwe tu ni kwa ajili ya marafiki, ndugu na jamaa, bali ziwe ni kwa ajili ya wale watu ambao hakuna anayewafikiria. Ili kumpatia nafasi murua ya Kristo Yesu kuweza kuzaliwa tena katika nyoyo za waja wake, waamini wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kusali na kupokea Sakramenri ya Upatanisho.

Zawadi za Noeli ni kitu kidogo sana, ikilinganishwa na maandalizi ya maisha ya kiroho. Ni kwa njia hii, hata mioyo ya waamini inaweza kufanana na Moyo Safi wa Bikira Maria, kwa kuwa huru dhidi ya dhambi; kwa kububujika ukarimu na tayari kuweza kumkirimia Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Kwenye Pango la Noeli mjini Bethlehemu kuna umaskini na upendo wa kweli, changamoto ya kuweza kujiandaa kikamilifu kumkaribisha na kumpokea Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maneno ya Bikira Maria “Na iwe kwangu kama ulivyosema” yanafunga rasmi Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio, mwaliko wa kupiga hatua kubwa zaidi kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Noeli. Hii inatokana na ukweli kwamba, ikiwa kama kuzaliwa kwake Kristo Yesu, hakugusi maisha, hata Sherehe za Noeli kwa mwaka 2020 zitapita tu kama “ndoto ya mchana”. Baba Mtakatifu amewaalika waamini wakati wa kusali Sala ya Malaika wa Bwana kusema: “Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Bikira Maria awasaidie waamini kuyasema haya kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Papa: Angelus

 

20 December 2020, 15:54