Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 23 Desemba 2020 amejikita zaidi kuhusu Sherehe za Noeli: maana na umuhimu wake katika maisha ya waamini. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 23 Desemba 2020 amejikita zaidi kuhusu Sherehe za Noeli: maana na umuhimu wake katika maisha ya waamini. 

Baba Mtakatifu Francisko: Maana na Umuhimu wa Sherehe za Noeli!

Ni wakati wa kwenda kiroho mjini Berhelehemu. Ni muda wa kutafakari changamoto zinazoibuliwa katika historia ya mwanadamu aliyejeruhiwa kwa dhambi, ambaye kwa sasa anatafuta ukweli, huruma na wokovu. Ukweli huu ni chemchemi ya furaha na ujasiri. Waraka wa Kitume “Admirabile signum” uwasaidie waamini kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katakesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Sherehe za Noeli, iliyofanyika kwenye Maktaba ya Kitume mjini Vatican, tarehe 23 Desemba 2020 imeongozwa na Neno la Mungu, kutoka katika Injili ya Luka: “Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Yudea mpaka katika mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa ukoo na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.” Lk. 2:4-7. Baba Mtakatifu katika katekesi yake, amekazia mambo msingi yatakayowasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli. Ni wakati wa kuwaiga wachungaji, ili waamini nao waweze kwenda kiroho mjini Bethlehemu. Ni muda wa kutafakari changamoto zinazoibuliwa katika historia ya mwanadamu aliyejeruhiwa kwa dhambi, ambaye kwa sasa anatafuta ukweli, huruma na wokovu ili hatimaye, kukutana na Mwenyezi Mungu. Ukweli huu ni chemchemi ya furaha na ujasiri. Waraka wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” uwasaidie waamini kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli.

“Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe”. Huu ni ujumbe walioambiwa wachungaji waliokuwa wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanahimizwa kwenda mjini Bethlehemu kiroho na huko watamwona Bikira Maria na Mtoto Yesu akiwa amelazwa kwenye hori ya kulia ng’ombe kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Noeli ni sherehe ya watu wote, kwa wale wanaoamini na wasioamini. Lakini kwa Wakristo Noeli ni tukio la maana sana, moto angavu na endelevu wa Mungu umeshuka kutoka mbinguni na unajipambanua kiasi cha kutoweza kuchanganywa na mambo mengine. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Sherehe hii haigeuzwi na kuwa ni kwa ajili ya waamini kujisikia, watu kuzamishwa katika ulaji wa kupindukia, kupeana zawadi kubwa kubwa na kutakiana matashi mema, lakini inakuwa ni Sherehe ambayo haina mvuto wala mashiko katika imani ya Kikristo na inayoonesha umaskini wa binadamu.

Kiini cha imani ya Kikristo ni kwamba, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Yn. 1:14. Huu ndio Ukweli wa Noeli na wala hakuna ukweli mwingine zaidi ya huu! Baba Mtakatifu anasema, Sherehe za Noeli ni mwaliko wa kutafakari changamoto zinazoibuliwa kwenye historia kutokana na majeraha ya dhambi. Mwanadamu anatafuta ukweli wa mambo, huruma ya Mungu na wokovu. Kwa upande mwingine, Mwenyezi Mungu kutokana na wema wake mkuu amekuja kukutana na wanadamu, ili kuwatangazia Ukweli unao okoa maisha na hivyo kuwashirikisha katika urafiki na maisha yake ya Kimungu. Zawadi hii ya Kimungu, inapokelewa katika hali ya unyenyekevu unaofumbatwa katika maisha ya Mwenyezi Mungu, wakati wa Sherehe za Noeli. Mwenyezi Mungu anataka kuwakomboa watu kutoka katika changamoto mamboleo zinazotokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na mambo yote yanayousumbua moyo wa mwanadamu.

Mwanadamu anaweza kuokolewa kutoka katika hali ya kukosa dira na mwelekeo wa maisha, kwa kutambua kwamba, Mtoto Yesu, mnyenyekevu na maskini, aliyejificha ni Mungu mwenyewe aliyefanyika mwili kwa ajili ya binadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwa njia ya Fumbo la Umwilisho “Mwana wa Mungu amejiunga kwa namna fulani na kila mwanadamu. Alifanya kazi kwa mikono ya kibinadamu, alifikiri kwa akili ya kibinadamu, alitenda kwa utashi wa kibinadamu na alipenda kwa moyo wa kibinadamu. Akizaliwa na Bikira Maria alijifanya kweli mmoja kati yetu, akifanana nasi katika yote isipokuwa katika dhambi”. Gaudium et spes namba 22. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua akisema, ukweli huu ni chemchemi ya furaha na ujasiiri mkuu. Mwenyezi Mungu amepita akawaangalia watu wake, akaona udhaifu na mapungufu yao lakini bado akaamua kufanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Hiki ni kiini na maana ya imani ya Kikristo.

Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa katika hija yake ya wongofu wa ndani analielezea tukio hili kuwa ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu unaokita mizizi yake katika udhaifu wa binadamu ili kuwafunulia watu huruma na upendo wa Mungu. Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho, Upendo uliozaliwa kwa ajili ya binadamu katika Kristo Yesu. Huu ni mwanga angavu unaowaangazia wale wote wanaotembea katika giza la dhambi na uvuli wa mauti na hivyo kutoa maana kamili ya maisha na historia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, tafakari hii fupi iwasaidie waamini kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli. Iwe ni fursa ya kufanya tafakari katika ukimya mbele ya Pango la Mtoto Yesu. Huu ni mwaliko wa kurejea tena kusoma na kutafakari Waraka wake wa Kitume: “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”.

Katika shule ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, wote wanaweza kupata bahati ya kuwa kama watoto wadogo ili kujifunza tukio la Fumbo la Umwilisho kwa kushangaa jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu amethubutu kuja hapa duniani,  ili kuwa karibu naye pamoja na watu wengine wote, ili kupata huruma. Wanasayansi wanaoshughulikia akili bandia wanasema kwamba robot inaweza kufanya kazi mbalimbali, lakini kamwe haitaweza kutoa huruma kwa binadamu. Kumbe, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Katekesi ya Noeli kwa Mwaka 2020 kwa kusema kwamba, mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa na tishio la janga la Virusi vya Corona, CVID-19 anahitaji huruma na upendo wa Kimungu na kibinadamu. Janga la Corona, limewalazimisha watu kutunza umbali wa kijamii. Mtoto Yesu katika Pango la Noeli anawafunulia waja wake njia ya huruma kama chemchemi ya huruma kwa majirani, njia ya kuweza kuwa binadamu wa kweli. Hii ndiyo njia muafaka inayopaswa kufuatwa na wote!

Katekesi Noeli 2020
23 December 2020, 15:38