Baba Mtakatifu Francisko, kufuatia kifo cha Askofu Anthony Banzi, ametuma salam za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga, salam zilizoandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, kufuatia kifo cha Askofu Anthony Banzi, ametuma salam za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga, salam zilizoandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. 

Maziko ya Askofu Banzi: Papa Francisko Atuma Salam za Rambirambi Tanga

Papa Francisko katika salam zake anasema, amepokea kwa majonzi mazito taarifa za kifo cha Askofu Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga. Anamtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre na hatimaye, Uaskofu aliyomkirimia Mtumishi wake mwaminifu Askofu Banzi. Anapenda sasa kuiweka roho ya Marehemu Askofu Banzi kwenye huruma ya upendo Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga, kufuatia kifo cha Askofu Anthony Mathias Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, kilichotokea Jumapili tarehe 20 Desemba 2020 kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Ibada ya Misa ya Mazishi ya Askofu Anthony Mathias Banzi imefanyika Jumanne tarehe 29 Desemba 2020 na kuongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Salam za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, zilisomwa na Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, katika Ibada ya Misa Takatifu ya Buriani kwa Askofu Banzi, iliyoadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuongozwa na Askofu Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake anasema, amepokea kwa majonzi mazito taarifa za kifo cha Askofu Anthony Mathias Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga. Anamtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre na hatimaye, Uaskofu aliyomkirimia Mtumishi wake mwaminifu Askofu Banzi. Anapenda sasa kuiweka roho ya Marehemu Askofu Banzi kwenye huruma ya upendo Kristo Yesu. Ametoa baraka zake za kitume kwa wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito, hasa kwa namna ya pekee kabisa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tanga. Wakati huo huo, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu pamoja na Askofu mkuu Novatus Rugambwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Samoa; Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga; New Zealand, Fiji, Palau na ambaye pia ni Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific wametuma salam zao za rambirambi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania.

Ibada ya Misa ya Mazishi ya Askofu Anthony Mathias Banzi imefanyika Jumanne tarehe 29 Desemba 2020 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua na kuongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, viongozi wa kidini na Serikali wametoa salam zao za rambirambi kwa familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Tanga. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limewashukuru watanzania wote kwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza Askofu Banzi katika safari yake ya mwisho hapa duniani. Hiki ni kielelezo cha upendo na matumaini katika kipindi hiki cha masikitiko na majonzi makubwa. Ni kiongozi ambaye alibahatika kuwa na karama nyingi ambazo amezitumia katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tanga.

Watanzania waendelee kumkumbuka na kumwombea Askofu Banzi huruma ya Mungu, ili aweze kumkirimia maisha ya uzima wa milele huko mbinguni. Katika pilika pilika za maisha, watu wa Mungu nchini Tanzania wasisahau wajibu wa kuwaombea jirani zao pamoja na kujiombea wenyewe. Viongozi wa Makanisa ya Kikristo wamemwelezea Askofu Banzi kuwa ni kiongozi aliyejipambanua akajitahidi kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene. Alionesha ushirikiano na mshikamano wa upendo wa kidugu wakati wa raha, shida na magumu ya watu wa Mungu Jimboni Tanga, wakati wa majanga asilia na pale hali hewa ilipochafuka kwenye mapango ya Amboni, Tanga. Kwa hakika amekuwa ni kiongozi bora wa Kanisa  na mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa watu wa Mungu. Amekuwa ni shuhuda wa unyenyekevu, Baba mwema na mpole, mvumilivu, aliyejijengea utamaduni wa kusikiliza kwa makini, wale wote waliomwendea kutaka ushauri, faraja na neno la matumaini.

Wananchi wa Tanga katika ujumla wao, watamkumbuka sana kwa jitihada zake za kutaka kuona Jiji la Tanga katika ujumla wake, linarejea tena katika ramani ya ustawi, tayari kuchangia maendeleo fungamani ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jiji la Tanga. Alitamani kuona kwamba, Tanga iliyokuwa imesheheni viwanda vingi na hivyo kutoa ajira kwa maelfu ya watu, vinafufuliwa ili kuchangia katika mchakato wa ukuaji wa wananchi na Tanzania katika ujumla wake. Bandari, Reli na Uwanja wa Ndege wa Tanga vilikuwa ni vichocheo vikuu vya maendeleo, lakini kwa miaka mingi vilidumaa na kushindwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Marehemu Askofu Banzi alitamani kuona kwamba, mambo yote haya yanarejeshwa tena katika ubora wake. Hizi ni changamoto ambazo zimevaliwa njuga na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli. Kina cha Bandari ya Tanga kimeongezwa ili meli ziweze kufika karibu na gati kushuhusha na kupandisha shehena mbalimbali za mizigo. Kiasi cha shilingi bilioni 170 kitatumika ili kufanikisha kazi hii kadiri ya taarifa ya Mamlaka ya Bandari Tanzania. Viongozi wa kidini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo wamekuwa ni msaada mkubwa katika kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa mkoani Tanga.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania katika salam zake za rambirambi kutokana na kifo cha Askofu Anthony Mathias Banzi, zilizosomwa kwa niaba yake na Kassim Majaliwa, Waziri mkuu wa Tanzania,  amempongeza Marehemu Askofu Banzi kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Tanga. Amekuwa ni kiongozi na mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kutoa huduma za: elimu, afya na maji. Alijipambanua kama kiongozi na mtetezi wa haki inayofumbatwa katika amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.Marehemu Askofu Banzi katika maisha na utume wake alikazia: Umoja, mshikamano na utengamano wa watanzania wote. Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa Marehemu Askofu Banzi katika kushiriki kuhamasisha mchakato wa amani, upendo, umoja na mshikamano wa Kitaifa. Alichangia huduma za kijamii, akajitahidi kuishi kwa upole na unyenyekevu, sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuzipokea kazi zake njema na kumstahilisha maisha na uzima wa milele.

Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki la Mtwara, tarehe 28 Desemba 2020 yaliongozwa na Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki la Mtwara na kuwatafakarisha watu wa Mungu waliokuwa wamehudhuria Ibada hii, kuhusu Fumbo la Kifo, Ufufuko na Maisha ya Uzima wa milele. “Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.” IKor. 15: 54-57. Huu ni ushauri wa mtu imara katika imani kwa Kristo Yesu, aliyezaliwa, akatekeswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kristo Yesu, ni ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, chemchemi ya upatanisho, haki na amani. Kristo Yesu awe ni nguvu inayoleta ukombozi na maisha ya uzima wa milele. Yesu mwenyewe bado anaendelea kujifunua katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Askofu Anthony Mathias Banzi katika maisha na utume wake alimpenda na kumtumikia Kristo Yesu kwa moyo wake wote; akawapenda upeo, wale wote aliokabidhwa kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza. Alikuwa ni mnyoofu na mchamungu, mpole na aliyebahatika kuwa na fadhila ya uvumilivu hata katika mateso makali. Alieleza na kukanya kwa upole na busara ya kichungaji. Alikuwa ni Baba msamehevu na mvuto wa huruma ya Mungu kwa wale wote walioteleza na kuanguka, ili aweze kuwainua tena kwa huruma ya Mungu. Alikuwa ni chombo na shuhuda a matumaini, alilitafakari na hatimaye kupambana na Fumbo la Kifo katika maisha yake kwa njia ya fadhila za Mungu alizokirimiwa. Askofu Titus Joseph Mdoe anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumkumbuka na kuendelea kumwombea Marehemu Askofu Banzi, ili aweze kutakaswa na hatimaye, kuingia kwenye Ufalme wa Mbinguni. Ni Baba ambaye alikiona kifo mbele ya macho yake, akajiandaa kikamilifu pasi na woga!

Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa Jumatatu, tarehe 28 Desemba 2020 kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuongozwa na Askofu Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, kwa namna ya pekee kabisa katika mahubri yake alikazia Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Aliwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuachana na ukatili unaofumbatwa katika uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka unaofisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Na badala yake, wawe ni vyombo na mashuhuda wa: huruma, upendo na faraja kwa watu wa Mungu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku! Askofu Banzi katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia: huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Aliwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, ili watubu na kumwongokea Mungu.

Kumbe, sasa ni zamu ya waamini kumkumbuka na kumwombea huruma na msamaha wa dhambi zake kama binadamu na kamwe wasipotoshwe na utandawazi, kwani dhambi ipo. Hii ni fursa ya kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo! Askofu Anthony Banzi alikuwa na Ibada ya pekee kwa Mtakatifu Athony wa Padua na amezikwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki la Tanga, Jumanne, tarehe 29 Desemba 2020. Ikumbukwe kwamba, kwa wale wenye Ibada kwa Mtakatifu Anthony wa Padua, huwa wana adhimisha kumbukumbu yake, kila siku ya Jumanne! Baba Askofu Banzi, sasa na apumzike wa amani.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Anthony Mathias Banzi alizaliwa tarehe 28 Oktoba 1946 kwenye Parokia ya Tawa, Jimbo Katoliki la Morogoro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Julai 1973 akapewa Daraja takatifu Upadre, Jimbo Katoliki la Morogoro. Mwaka 1976 aliteulia kuwa Msarifu wa Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba. Kati ya mwaka 1976 hadi mwaka 1981 alipelekwa nchini Austria kwa masomo ya juu na kufanikiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Falsafa. Kati ya mwaka 1981 hadi mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mandera na Mhudumu wa maisha kiroho kwenye Hospitali ya Turiani, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Kati ya Mwaka 1981 hadi mwaka 1985 aliteuliwa kuwa Mhasibu wa Jimbo Katoliki la Morogoro. Kati ya Mwaka 1985 hadi mwaka 1987 alikuwa ni Padre wa kiroho, Sekondari ya Masista Bigwa, Morogoro. Kati ya Mwaka 1988 hadi mwaka 1991 alikuwa Jalimu na mlezi, Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na baadaye akateuliwa kuwa Gambera. Kati ya mwaka 1992 hadi mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Gambera wa Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Tarehe 10 Juni 1994, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga na kuwekwa wakfu tarehe 15 Septemba 1994 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa muhtasari kabisa Askofu Banzi amefariki dunia akiwa na umri wa zaidi ya miaka 74 ya kuzaliwa, miaka 47 ya Daraja Takatifu ya Upadre na miaka 26 ya Uaskofu, utume ambao aliufanya kwa uaminifu mkubwa katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tanga.

Papa Mazishi Askofu Banzi

 

 

 

 

 

 

 

 

29 December 2020, 14:08